Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujenzi mpya wa Gaza unahitaji zaidi ya nondo na kokoto: Guterres

Mtazamo wa eneo la mijini lililoharibiwa huko Gaza lenye vifusi na uchafu. Watu wawili wanatembea kwenye vifusi.
© UNICEF/Mohammed Nateel Raia wa Gazwanaendelea kurejea kwenye nyumba zao zilizosambaratika

Ujenzi mpya wa Gaza unahitaji zaidi ya nondo na kokoto: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo amesisitiza kuwa “msingi wa kweli wa ujenzi mpya na kujikwamua kwa Gaza lazima uwe msingi wa mfumo wa kisiasa ulio wazi na uliokubaliwa, si tu matofali na saruji.”

Akizungumza katika mkutano wa dharura wa mataifa ya nchi za Kiarabu kuhusu hali ya Mashariki ya Kati na ujenzi wa Gaza mjini Cairo Misri, António Guterres amekaribisha juhudi zinazoongozwa na Waarabu za kuchochea msaada wa ujenzi mpya wa Gaza.
Amesisitiza kuwa ujenzi upya wa eneo hilo lililoathirika vibaya na vita lazima uongozwe na misingi inayoheshimu sheria za kimataifa na kuzuia duru nyingine za ghasia.
“Msingi wa kweli wa ujenzi mpya wa Gaza utakuwa zaidi ya nondo na kokoto” amesema akiongeza kuwa “Utakuwa ni heshima, haki ya kujitawala, na usalama. Hii inamaanisha kushikamana na msingi wa sheria za kimataifa, kukataa aina yoyote ya usafishaji wa kikabila, na kuunda suluhisho la kisiasa.”
Kijana Mpalestina ameketi katikati ya vifusi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Mohammed Nateel Mtoto akiwa katika kifusi kilichotokana na vita Gaza

Mfumo wa kisiasa ni muhimu

Bwana Guterres ameonyesha kuwa juhudi za ujenzi mpya haziwezi kutenganishwa na hali ya kisiasa kwa ujumla.
Amesema “Kumaliza mzozo wa sasa pekee haitoshi. Tunahitaji mfumo wa kisiasa ulio wazi ambao utaweka msingi wa kujikwamua, ujenzi mpya na utulivu wa kudumu wa Gaza.”
Akikiri kuhusu wasiwasi wa usalama wa Israeli, ameongeza kuwa hakutakiwi kuwa na uwepo wa muda mrefu wa kijeshi wa Israeli ndani ya Gaza.

Uharibifu wa kiwango cha juu

Vita vya Gaza vimeacha kiwango cha uharibifu kisicho na kifani, huku takriban tani milioni 51 za vifusi zikifunika mandhari ambapo kulikuwa na mitaa yenye shughuli nyingi hapo awali.
Kulingana na ripoti mpya ya tathmini ya uharibifu na mahitaji ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 60 ya nyumba sawa na nyumba 292,000 na asilimia 65 ya barabara zimeharibiwa katika eneo lenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 360.
Kwa kushirikiana na mamlaka za Palestina, mashirika ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya mazingira, na mashirika yasiyo ya kiserikali wanasaka njia za kuondoa vifusi kwa usalama ili familia ziweze kujenga upya.
Timu za Umoja wa Mataifa zinatumia uzoefu kama huo kutoka Mosul, Iraq, na miji ya Syria ya Aleppo na Latakia, yote ikiwa imeharibiwa na vita.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, pamoja na washirika kama Benki ya Dunia, wanakadiria kuwa dola bilioni 53 zitahitajika kwa kujikwamua na ujenzi mpya.
Mwanamume ameketi kwenye matofali ya zege katikati ya vifusi vya jengo lililoharibiwa huko Jabalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
UN News Ramadan Kutkut akiwa ameketi kwenye kifusi kwenye nyumba yake huko Jabalia, kaskazini mwa Gaza.

Usitishaji mapigano lazima udumishwe

Hali ya kibinadamu ikiwa bado mbaya, Bwana Guterres ameonya kuwa kuanza tena kwa mapigano kutawasukuma mamilioni tena katika mateso na kudhoofisha zaidi kanda hiyo.
“Lazima tuepuke kwa gharama yoyote kurejea kwa mapigano,” amesisitiza Guterres akizitaka pande zote mbili kuheshimu ahadi zao chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano na mpango wa mateka, na kurejea kwenye mazungumzo bila kuchelewa.
“Mateka wote lazima waachiliwe mara moja, bila masharti na kwa njia ya heshima,” amesema, akiongeza kuwa kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina kunapaswa kufanywa kulingana na masharti ya mpango huo na pia kwa njia ya heshima.
Amesisitiza kuwa “Pande zote lazima zihakikishe kutendewa kibinadamu kwa wale wote walioko chini ya mamlaka yao.”


Kuhakikisha misaada inatolewa bila vizuizi

Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa misaada ya kibinadamu kwa raia wanaohitaji Gaza, akitaka kuondolewa kwa vizuizi vyote vya utoaji wa misaada.
“Misaada ya kibinadamu si jambo la kujadiliana. Lazima itolewe bila kikwazo,” amesema, akiwahimiza wafadhili kuhakikisha ufadhili wa kutosha.
Amewashukuru wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wahudumu wote wa kibinadamu kwa kujitolea kutoa huduma muhimu katika mazingira magumu zaidi, akitaka msaada wa haraka na kamili kwa kazi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), ikiwemo msaada wa kifedha.
Taa na vinyago vya sherehe vyenye rangi mbalimbali vinaonyeshwa katikati ya vifusi na majengo yaliyoharibiwa huko Gaza wakati wa Ramadhani.
UN News Wakati wa Ramadhan watu wa Gaza wako katika hali ambayo hawajawahi kuishuhudia kabla

Kuongezeka kwa ghasia katika Ukingo wa Magharibi

Zaidi ya Gaza, Bwana Guterres ameeleza wasiwasi wake juu ya ongezeko la ghasia katika Ukingo wa Magharibi, ambapo vikosi vya usalama vya Israeli vimeanzisha operesheni kubwa, zikiwemo mashambulizi ya anga na kupelekwa kwa mizinga.
Amebainisha kuwa “Zaidi ya Wapalestina 40,000 wamefurushwa katika mwezi uliopita, ikiwa ni kuhama kwa kiwango kikubwa zaidi katika Ukingo wa Magharibi katika miongo kadhaa.
Wakati huo huo, ubomoaji, kuffurushwa na upanuzi wa makazi vinaendelea, huku ghasia za walowezi zikiongezeka.”
Ameytoa wito wa hali hiyo kutulizwa haraka na kusitishwa kwa hatua za upande mmoja, zikiwemo upanuzi wa makazi na vitisho vya kunyakua ardhi.
“Israeli, kama mamlaka inayokalia kwa mabavu, lazima itimize wajibu wake wote chini ya sheria za kimataifa, zikiwemo sheria za kimataifa za kibinadamu,” amesema Bwana Guterres.
Aidha, Mamlaka ya Palestina lazima iungwe mkono ili kutawala kwa ufanisi, na “ifanye hivyo kwa kufuata wajibu wake chini ya sheria za kimataifa.”
Wakazi hutembea na kuendesha baiskeli katika barabara ya Kaskazini mwa Gaza iliyojaa vifusi kutoka kwa majengo yaliyoharibiwa.
© UNICEF/Mohammed Nateel Watu wanarejea katika vitongoji vilivyoharibiwa kaskazini mwa Gaza. Takriban asilimia 90 ya nyumba za ukanda huo zimeharibika.

Suluhisho la nchi mbili ndilo njia pekee

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa suluhisho la nchi mbili ndilo njia pekee inayowezekana ya amani ya kudumu.
“Njia pekee ya amani ya kudumu ni ile ambapo nchi mbili Israeli na Palestina zinaishi bega kwa bega kwa amani na usalama, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, huku Yerusalemu ikiwa mji mkuu wa nchi zote mbili,” amesema.