Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto ni waathirika wa ubakaji wakati mgogoro wa kikatili ukiendelea Sudan: UNICEF

Watoto watatu wanachungulia kupitia skrini ya matundu kwenye hema UNICEF katika eneo linalofaa watoto katika kambi ya wakimbizi katika jimbo la Kassala, Sudan.
© UNICEF/Tess Ingram Watoto wakichungulia kwenye hema la UNHCR katika jimbo la Kassala Sudan

Watoto ni waathirika wa ubakaji wakati mgogoro wa kikatili ukiendelea Sudan: UNICEF

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ripoti ikionesha kuwa wanaume waliojihami kwa silaha wanabaka na kuwanyanyasa kingono watoto, wakiwemo watoto wadogo wenye  umri wa mwaka mmoja, wakati huu ambapo mapigano yanazidi kushamiri nchini humo.

UNICEF imesema  takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa visa 221 vya ubakaji dhidi ya watoto vilitekelezwa, ingawa idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi kwani wengi wa waathirika hawawezi au wanaogopa kutoa ripoti za uhalifu huu, na hivyo limeitaka jumuiya ya kimataifa ichukue hatua haraka.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amesema, "Watoto wadogo wa umri wa mwaka mmoja kubakwa na wanaume wenye silaha inapaswa kushangaza kila mtu na kuchochea hatua za haraka. Mamilioni ya watoto nchini Sudan wako katika hatari ya kubakwa na aina nyingine za ukatili wa kijinsia, ambazo zinatumiwa kama mbinu ya vita. Hili ni jambo la kuchukiza na ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na linaweza kuleta uhalifu wa kivita. Lazima likomeshwe."

Kati ya ripoti iliyotolewa na shirika hilo, asilimia 66 ya waliobakwa walikuwa wasichana, huku asilimia 33 wakiwa wavulana, ikionesha wigo mpana wa unyanyasaji huu.

Baadhi ya unyanyasaji huu umehusisha watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano limesema shirika la UNICEF na kuongeza kuwa ukatili huu umewalazimu familia nyingi, hasa wanawake na wasichana, kutoroka na kuhamia miji au maeneo yasiyo rasmi, ambapo unyanyasaji wa kijinsia unabaki kuwa tishio la kila wakati.

Watoto wawili wadogo, waliokimbia makazi yao wameketi kwenye ukuta mdogo katika kituo cha mikusanyiko huko Madani, Sudan. Mwanamke anaonekana nyuma.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdeen Mzozo nchini Sudan umewakosesha makazi maelfu ya watoto na familia zao.

Mchango wa UNICEF katika kutokomeza ukatili huu

UNICEF, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imesema inafanya kazi kutoa msaada kwa waathirika, ikiwa ni pamoja na maeneo salama, huduma za matibabu, na msaada wa kisaikolojia.

Wanatoa pia mafunzo kwa wahudumu wa ndani ili kuwasaidia waathirika kupata huduma. UNICEF inasisitiza kwamba pande zote zinazohusika katika mgogoro huu ziache ukiukaji huu na kuheshimu sheria za kimataifa zinazolinda watoto.

Catherine Russell ameongezea kuwa "Ukatili wa kingono unaoenea nchini Sudan umeleta hofu kwa watu, hasa watoto. Pande zinazohusika katika mzozo huu, pamoja na wale wanaoathirika zaidi, wanapaswa kufanya kila juhudi kukomesha ukiukaji huu mkubwa dhidi ya watoto. Makovu haya ya vita hayaelezeki na yatadumu kwa muda mrefu."

Wavulana watano wadogo, ambao huenda ni watoto waliohamishwa, wamesimama katika eneo lenye vumbi nje huko Atbara, Sudan. Wameshikilia au wamesimama karibu na vyombo vikubwa vya maji vya plastiki.
© UNICEF/Abdulazeem Mohamed Watoto waliokimbia makazi yao kutokana na vita nchini Sudan sasa wanaishi Atbara.

UNICEF inahimiza kwamba:

·        Serikali ya Sudan na pande zote katika mzozo zinapaswa kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu ili kulinda raia, na hasa watoto.

·        Ukatili wa kijinsia na ukatili wa kingono unapaswa kukomeshwa mara moja.

·        Miundombinu ya huduma muhimu na watoa huduma wanapaswa kulindwa ili kazi yao ya kuokoa maisha iendelee.

·        Wahudumu wa misaada ya kibinadamu wanapaswa kuwa na uwezo wa kutoa misaada na huduma za kuokoa maisha kwa usalama, na familia zinapaswa kuwa na uwezo wa kupata msaada wanaohitaji bila hatari.

·        Mifumo salama na ya kimaadili ya ukusanyaji wa takwimu inapaswa kuwa kipaumbele, ili kusaidia kuimarisha hatua za kibinadamu na kuwa sehemu ya juhudi pana za kuwawajibisha wahalifu.

·        Katika maamuzi ya ufadhili, programu za kukabiliana na ukatili wa kijinsia zinapaswa kupewa kipaumbele na wafadhili kama huduma za kuokoa maisha.