Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaonya juu ya janga la kibinadamu wakati vivuko vya Gaza vikiendelea kufungwa

Wafanyakazi wa misaada wa WHO na WFP wakipakia mafuta na vifaa kwenye lori katika hospitali ya Kamal Adwan huko Gaza.
© WHO Umoja wa Mataifa wafikisha msaada Hospitali ya Kamal Adwan Gaza

UN yaonya juu ya janga la kibinadamu wakati vivuko vya Gaza vikiendelea kufungwa

Amani na Usalama

Kufungwa kwa vivuko Gaza kutasitisha ugawaji wa msaada muhimu wa kibinadamu umeonya leo Umoja wa Mataifa juu ya kufungwa kwa vivuko vya Kerem Shalom, Erez, na Zikim vinavyoelekea Gaza, ambavyo vimesitisha usafirishaji wa mizigo ya msaada muhimu wa kibinadamu.

Kulingana na Msemaji wa Umoja wa Mataifa , maelfu ya mahema na vifaa vya kuokoa maisha bado havijawasilishwa Gaza, na hivyo kuzidisha hali mbaya ambayo tayari ilikuwepo Gaza.
Ameongeza kuwa Kufungwa huko kumetatiza kwa kiasi kikubwa utoaji wa msaada wa kibinadamu, ambao ulikuwa umeongezeka wakati wa kusitishwa kwa mapigano hivi karibuni.

Athari kwa usambazaji wa chakula na maji

Ofisi ya Kuratibu masuala  ya Kibinadamu na misaada ya dharura (OCHA) imeripoti kwamba kusitishwa kwa mapigano kuliruhusu washirika wa kibinadamu kusambaza pakiti za chakula, maji, na msaada wa makazi kote Gaza.
Karibu kila mtu Gaza alikuwa amepokea msaada wa chakula kabla ya vivuko kufungwa.
Hata hivyo, kufungwa huko kwa mujibu wa OCHA, kumesababisha ongezeko kubwa la bei, ambapo gharama za unga na mboga zimeongezeka zaidi ya mara 100.
Washirika wa msaada kwa sasa wanatathimini akiba ya chakula iliyopo ndani ya Gaza.
Kiwanda cha Kuoka cha Zadna huko Deir al Balah, Gaza, kikiwa na umati mkubwa wa watu waliokusanyika nje mnamo Januari 4, 2024.
WFP Duka la kuoka mikate lafunguliwa Gaza baada ya siku 50 za kufungwa

UNICEF yaonya kuhusu hatari kwa watoto na familia

UNICEF imeonya kuwa kusitishwa kwa usambazaji wa misaada kutasababisha athari mbaya kwa watoto na familia zinazojitahidi msaada huo ili kuishi.
Shirika hilo limeripoti kwamba karibu malori 1,000 yaliyobeba maji safi, vifaa vya matibabu, chanjo, chakula cha matibabu na vifaa vingine yalivuka kuingia Gaza tangu Januari 19. Kusitishwa kwa mapigano kuliwezesha UNICEF kutoa nguo za joto kwa watoto 150,000 na kusambaza maji kwa karibu nusu milioni ya watu katika maeneo ya mbali.

Msaada wa lishe na afya uko hatarini

Kwa mujibu wa UNICEF washirika wa kibinadamu wametoa virutubisho vya lishe kwa karibu robo milioni ya watoto na maelfu ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wakati wa kusitishwa kwa mapigano.
Kuimarika kwa utoaji wa msaada kumesababisha watoto wachache kuhitaji matibabu ya utapiamlo.
Hata hivyo, shirika hilo limesema  kufungwa kwa vivuko kunatishia kubatilisha mafanikio haya, na kuwaacha watu walio hatarini bila msaada muhimu wa lishe.

Juhudi za kuimarisha uzalishaji wa chakula wa ndani

Katika wiki za hivi karibuni, washirika wa msaada wamesambaza vifaa vya mbegu za mboga huko Rafah, Khan Younis, na Deir al Balah kusaidia familia kulima chakula chao wenyewe. 
Mpango huu unalenga kukuza lishe yenye mseto zaidi na kuimarisha uhakika wa chakula. 
Idadi ya vituo vya usambazaji maji kote Gaza pia imeongezeka mara mbili tangu kuanza kwa kusitishwa kwa mapigano, lakini vifaa vya mabomba na vipuri vinahitajika kwa dharura ili kudumisha mfumo huo.
Kundi kubwa la watu, wakiwemo watoto na wanawake, wakipanga foleni kutafuta maji ya kunywa kutoka kwenye tanki linaloungwa mkono na UNICEF huko Deir al-Balah, Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba Familia zikipokea msaada wa maji kutoka UNICEF katika kituo cha Deir al-Balah,Ukanda wa Gaza

Jamii zilizofurushwa zina mahitaji ya dharura

Umoja wa Mataifa  umeripoti kwamba zaidi ya watu 1,200 waliofurushwa kwa sasa wanahifadhiwa katika eneo la Khan Younis, kwani hawajaruhusiwa kurudi kwenye nyumba zao katika eneo la buffer.
Timu za OCHA zinafanya kazi kuhamasisha msaada, ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, na msaada wa maji, usafi na usafi wa mazingira.
Shule za umma zimefunguliwa tena kote Gaza, zikihifadhi takriban wanafunzi 100,000, huku maeneo ya kujifunzia ya muda yakianzishwa kwa kutumia mahema na vifaa vya kurejelezwa.