Wakimbizi wa DRC walioingia Burundi wahamia eneo salama zaidi
Wakimbizi wa DRC walioingia Burundi wahamia eneo salama zaidi
Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC waliokuwa wamepata hifadhi ya muda kwenye kituo cha Kaburantwa ndani ya Burundi, mpakani na DRC wamehamishiwa jimbo la Rutana.
Miongoni mwao ni Kasigwa Antoinette, mkimbizi kutoka DRC ambaye katika video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Burundi anaonekana akifungasha virago vyake, tayari kuhamia eneo salama zaidi baada ya mashambulizi kutoka waasi wa M23 kumfurusha kutoka nchini mwake.
Bi. Kasigwa anasema, “tulikimbia mapigano, kulikuwa na milio ya risasi na baadhi ya watu waliuawa, lakini sisi tuliweza kukimbia. Tulikimbia hadi hapa Kaburantwa.”
Ripoti ya kwamba wanahamishiwa eneo salama zikampatia ahueni kwani anasema, “sasa sina tena wasiwasi. Jana nilikuwa nina hofu sana ya kunasa katikati ya mapigano au hata kushambuliwa hapa tulipo ambako wengi wetu tumesaka hifadhi. Tulikuwa tuna wasiwasi sana lakini Mungu ametusaidia kwamba sasa tutasafirishwa kwenda eneo lililo salama zaidi.”
Maafisa wa UNHCR waliwaita wakimbizi majina mmoja baada ya mwingine tayari kuanza kujongea kwenye mabasi yaliyowasili hapa Kaburantwa.
Mwakilishi wa UNHCR nchini Burundi Brigitte Mukanga-Eno, alitumia fursa ya tukio hili kuzungumza na wakimbizi wakiwemo watoto na kisha akaeleza kwamba “tumekuwa tunapokea wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kwa wiki chache zilizopita, lakini idadi kubwa wameanza kuwasili tarehe 14 mwezi wa Februari, ambapo tulipata idadi kubwa ya wakimbizi wakiingia Burundi kwa kuvuka mto Rusizi.”
Mabasi matano ya kusafirisha wakimbizi yakasogea karibu na mmoja baada ya mwingine akaanza kuingia na ndipo Bi. Mukanga-Eno akaelezea wanakoelekea.
“Tunaanza kusafirisha wakimbizi kutoka hapa kwenda eneo ambalo serikali ya Burundi imetupatia, lililoko makazi ya Musenyi. Musenyi iko jimbo la Rutana mbali na mpakani ambako ni salama kwa kila mtu.”