Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila siku UNICEF yafikishia watoto 364,000 mjini Goma na huduma za maji safi na za kujisafi

Familia zinasafiri kwenye barabara ya vumbi zikiwa zimebeba mali zao wanapohama kutoka kambi za watu waliokimbia makazi yao karibu na Goma hadi kijiji cha Shasha huko Kivu Kaskazini, DR Congo.
UNICEF/Jospin Benekire Familia zilizokuwa zinaishi kwenye kambi za wakimbizi eneo la Goma, jimboni Kivu Kaskazini zikielekea kijiji cha Shasha jimboni humo humo.

Kila siku UNICEF yafikishia watoto 364,000 mjini Goma na huduma za maji safi na za kujisafi

Afya

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hususan katika mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini ambako mashambulizi ya waasi wa M23 yalifurusha raia na kusambaratisha huduma, shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto, UNICEF linasema kwa sasa limerejesha huduma na linaweza kufikisha huduma ya maji na za kujisafi kwa watu 700,000 wakiwemo watoto 364,000.

Hii ni baada ya sitisho la huduma hizo wakati wa mapigano yaliyoanza mwishoni mwa mwezi Januari na mji wa Goma, kutwaliwa na waasi wa M23.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Goma, inasema mapigano  makali mwishoni mwa mwezi Januari yaliacha wakazi milioni 2 mjini humo, bila huduma za majisafi, kujisafji au umeme.

UNICEF na MONUSCO wamefanikisha matumizi ya nishati kupampu maji

Huduma hiyo ya maji inawezekana kupitia mtambo wa maji wa kampuni ya REGIDESO baada ya UNICEF na Ujumbe wa  Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO kuipatia lita 77,000 za dizeli ili kuendesha pampu tano kuanza kufanya kazi. Pampu ziliacha kufanya kazi baada ya umeme kukatwa wakati wa mashambulizi.

Mashariki mwa Goma, watu wengine 30,000 wanapata huduma yam aji kupitia mtandao wa maji uliofungwa na UNICEF huko eneo la Bushara-Kayarutshiyna.

Hofu ya kipindupindu kwani kuna wanaotumia maji ya Ziwa Kivu

Hata hivyo amesema bado wengi wanategemea maji yasiyo safi na salama kutoka Ziwa Kivu. “UNICEF na wadau wameweka zaidi ya vituo 50 vya kutakatisha maji kwenye mwalo wa ziwa hilo, ili kuhakikisha maji ni salama. Huduma hiyo inafikia watu 56,000 kila siku ili kudhibiti mlipuko wa kipindupindu.”

“Tayari tunaona dalili za kutia hofu za wagonjwa wa kipindupindu, ikihusisha ukimbizi na watu kutegemea maji yasiyo safi na salama,” amesema Basse, akiongeza kuwa msimu wa mvua ukijongea, wana hofu kubwa ya mlipuko.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kipindupindu kimeua watu zaidi ya 5,500 nchini DRC, ambako ni asilimia 43 tu ya raia ndio wana huduma ya uhakika ya maji safi na salama n ani asilimia 15 tu wanafikiwa na huduma za msingi za kujisafi

Janga la kibinadamu limeongeza shinikizo kwenye mahitaji. Mamia ya maelfu ya watu kwa sasa wanahama kutoka walikokimbilia awali mjini Goma na kurejea kwenye maeneo ya awali ambako huduma za maji safi na za kujisafi hazitoshelezi.

Mapigano pia yaliharibu miundombinu ya maji inayotumika mara kwa mara.

“Maji safi na salama ni uhai. Wakati huu ambapo milipuko ya kipindupindu na mpox inatishia mashariki mwa DRC, watoto na familia zao wanahitaji maji safi kuliko wakati wowote ule, ili kuwalinda dhidi ya  janga la afya,” amesema Jean Francois Basse, Kaimu Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC.

Amesema duniani kote, watoto walioko kwenye mizozo ya muda mrefu, wana nafasi mara tatu zaidi ya kufa kwa magonjwa yanayohusiana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama kuliko vita.

“Kurejesha huduma muhimu ya maji ni suala linalotakiwa kupatiwa kipaumbele, la sivyo tunaweka hatarini maisha mengi zaidi,” amesema Afisa huyo.

Licha ya kuzorota kwa hali ya usalama, UNICEF imechukua hatua kwa kupeleka maboza ya maji kwenye vituo vitatu vya afya, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Virunga, ambayo ilitibu takribani majeruhi 3,000. Vikasha vya huduma za afya vya kutibu wagonjwa 50,000 vilipelekwa kwenye vituo vya afya vilivyokuwa vimezidiwa wagonjwa.