UNICEF Kenya yatekeleza kwa vitendo kujengea wasichana hamasa kwenye STEM
UNICEF Kenya yatekeleza kwa vitendo kujengea wasichana hamasa kwenye STEM
Nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na wadau wengine wanafanikisha mpango wa kuhamasisha wasichana kuingia katika masomo ya STEM yaani Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.
Baadhi ya wasichana wakimbizi katika kambi ya Dadaab iliyoko jimbo la Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya ni wanufaika wa mpango huu na miongoni mwao ni Zamzam Hussein.
Zamzam alikuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Hagadera na ni mkimbizi mwenye asili ya Somalia na sasa anaishi katika kambi ya wakimbizi ya Daadab nchini Kenya akiwa na ndoto ya kuwa daktari.
Kupitia mpango huu ambao ni sehemu ya programu ya PROSPECTS ambao ni ushirikiano wa kimataifa unaojumuisha mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa ukilenga kuboresha upatikanaji wa elimu, ulinzi wa jamii, na ajira yenye hadhi kwa jamii zinazowakaribisha wakimbizi na watu waliolazimika kuhama makazi yao Zamzam Hussein ameweza kukumbatia sayansi.
Maktaba na maabara ya sayansi kichocheo cha Zamzam kwenye STEM
Zamzam anasema, “nilikuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Hagadera na nikahitimu elimu yangu mwaka wa 2024. Nilijiunga na shule hiyo Agosti 2021. Nilichopenda zaidi nikiwa shuleni ni maktaba, maabara ya sayansi na maabara ya kompyuta.”
Anasema pia anapenda kuwashauri wasichana wadogo wanaosoma shuleni na walio wakimbizi wafanye kazi kwa bidii bila kujali changamoto wanazokabiliana nazo, akisema, “watatimiza ndoto zao na waweze kufanikiwa katika siku za usoni. Nataka kuwa daktari kwa sababu nilipokuwa shule ya sekondari nilijifunza mambo mengi kuhusiana na matibabu. Ningependa kuwashukuru wafadhili wetu kwa sababu bila wao nisingekuwa hapa.”
PROSPECT imewezesha kuajiri walimu na kupatikana kwa vifaa
Mpango huu wa STEM umetoa msaada wa rasilimali kama vile kuajiri walimu zaidi wa sayansi, kutoa mafunzo kwa walimu, kutoa vifaa vya sayansi kwa ajili ya maabara ya shule na kuanzisha programu ya maabara ya mtandaoni ambapo wanafunzi wanaweza kufanya majaribio ya sayansi kwenye mtandao wa intaneti.
Kupitia video iliyorekodiwa na UNICEF, Patrick Njogu, Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari ya Hagadera anasema, “nimemfundisha Zamzam na wasichana wengine ili waweze kutimiza ndoto na malengo yao. Wasichana wamekuwa wakikabiliana na changamoto kama vile ndoa za mapema.”
Mwalimu Njogu anakiri kuwa UNICEF imekuwa ya manufaa zaidi kwa wasichana kwani kwa sasa walimu wawili zaidi wa sayansi wameajiriwa. Mbali na hayo imekuwa ikiendesha mafunzo ya walimu, imetoa vifaa vya sayansi kwa ajili ya maabara ya shule na kuanzisha programu ya maabara ya mtandaoni Programu hii ya mtandao imetengeneza uhusiano nzuri wa wanafunzi katika masomo ya sayansi.