Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho la usaidizi wa kifedha wa Marekani kwa UNFPA lathibitishwa

Mwanamke mjamzito anafanyiwa uchunguzi wa ultrasound kutoka kwa mkunga katika kituo cha afya nchini DR Congo, akitazama picha hiyo kwenye simu janja.
© UNFPA DRC/Junior Mayindu Mwanamke anapimwa uchunguzi wa afya ya uzazi katika kituo cha afya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Sitisho la usaidizi wa kifedha wa Marekani kwa UNFPA lathibitishwa

Afya
  • Ni kwa miradi takribani 48 inayofadhiliwa na Marekani
  • Hii si mara ya kwanza Marekani inachukua hatua hii
  • Madai ni kwamba UNFPA inashinikiza utoaji mimba, hoja inayopingwa na UNFPA

Sasa ni rasmi kuwa Marekani imeondoa mchango wake wa dola milioni 377 kwa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA, hatua ambayo itakuwa na madhara makubwa kwa wanawake na wasichana.

Thibitisho hilo lilipatikana Alhamisi kufuatia ripoti za siku iliyotangulia Jumatano ya kwamba “takribani usaidizi wa fedha kwa miradi 48 ya UNFPA kutoka shirika la Marekani la Misaada ya kimaendeleo, USAID na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesitishwa,” UNFPA imesema kupitia taarifa yake.

“Uamuzi huu utakuwa na madhara makubwa kwa sekta ya afya, wanawake na wasichana, na pia kwa wahudumu wa kibinadamu ambayo wanawahudumia kwenye maeneo yenye majanga zaidi duniani.”

Misaada ya USAID ililenga kusaidia kwenye huduma muhimu za afya ya wajawazito, ulinzi dhidi ya ghasia, tiba kwa wale waliokumbwa na vitendo vya ubakaji na huduma zingine za kuokoa maisha kwenye maeneo yenye majanga.

Hii inajumuisha kazi za UNFPA za kutokomeza vifo vya wajawazito, wajawazito kujifungua salama na kutatua tatizo la ukatili wa kijinsia unaokumba wanawake na wasichana kwenye maeneo ya mizozo kama vile Gaza, Sudan na Ukraine.

Msichana mdogo wa Kiafghani aliyevaa kitambaa cha kijani kichwani ameketi kwenye kiti karibu na jozi ya magongo, mbele ya chombo kilichoandikwa nembo UNFPA .
© UNFPA Afghanistan Mtoto nchini Afghanistan ambaye amenufaika na usaidizi kutoka UNFPA

Kuanzia Afghanistan hadi Ukraine

UNFPA inashirikiana na wadau katika nchi 150 kutoa huduma mbalimbali za afya ya uzazi na kuhakikisha kujamiiana kuliko salama.

Lengo lake ni kukidhi mahitaij ya uzazi wa mpango ambayo bado hayajakidhiwa, kuzuia vifo vya wajawazito, ukatili wa kijinsia na mila potofu, ikiwemo ndoa katika umri mdogo na ukeketaji wanawake na wasichana ifikapo mwaka 2030.

“Matangazo haya ya kusitisha ufadhili inahusisha misaada ambayo awali iwali ilirejeshwa kwa misingi ya kiutu, kwa kuwa ilionekana kuwa ni ya kuokoa maisha kwa wanawake na wasichana walio hatarini,” imesema UNFPA.

Misaada hiyo ya fedha hufadhili miradi katika nchi kama vile Afghanistan, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC), Haiti, Mali, Sudan, Syria na Ukraine.

Waliowahi kukata ukeketaji katika Kituo cha Masanga kinachoungwa mkono na UNFPA katika mkoa wa Mara wana mabango kuhusu afya na usawa wa kijinsia.
Warren Bright/UNFPA Tanzania Wanawake hawa zamani walikuwa mangariba, sasa wamedondosha nyembe na wanashiriki katika ukeketaji mbadala kufuatia mafunzo kwenye kituo cha Masanga mkoani Mara. Kituo hiki kinapata msaada kutoka shirika la idadi ya watu duniani, UNFPA. Maghariba pia wakidondosha nyembe wanakuwa na mradi mbadala wa kupata kipato.

Usitishaji wa awali wa ufadhili

Hatua ya sasa ya kuondoa ufadhili inafuatia hatua za awali za taifa hilo tajiri zaidi duniani za kuondoa ufadhili kwenye UNFPA na UNAIDS mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu  na kuacha huduma zikiwa zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa mara kadhaa serikali zilizotangulia za Marekani zimekuwa zikiondoa ufadhili wao kwa UNFPA kwa madai kuwa shirika hilo linasaidia miradi ya kulazimisha utoaji mimba au kuzuia watu kupata watoto, madai ambayo yamekuwa yakikanushwa na serikali nyingine za Marekani zilizoko madarakani, uchunguzi huru, na viongozi wa UNFPA na Umoja wa Mataifa kwa ujumla.

“Jukumu la UNFPA ni kinyume na madai hayo – ni kuhakikisha haki ya mtu kuchagua anachotaka inalindwa,” imesema UNFPA.

UNFPA inategemea ufadhili na michango kutoka serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, mifuko na sekta binafsi na watu binafsi.