"Hii ni ardhi yetu" Kujenga mustakbali wa Gaza kutoka kwenye magofu ya vita
"Hii ni ardhi yetu" Kujenga mustakbali wa Gaza kutoka kwenye magofu ya vita
Msaada wa Kibinadamu
Usiku, analala chini ya turubai juu ya magofu ya nyumba ya familia yake. Kama wengine waliorejea kaskazini mwa Gaza baada ya miezi ya kuhama kutokana na vita, Sufian Al-Majdalawi anashikilia chochote anachoweza kupata.
Akitumia zana ndogo na mikono yake, anapekua katika lundo la vifusi na mchanga akijaribu kuchimbua mali na nyaraka muhimu kama hati za umiliki kuthibitisha kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo.
Anatamani siku moja aweze kuijenga upya, kwa muda mfupi, anatumaini kwamba hata magofu yanaweza kuwa na thamani fulani.
Uharibifu usio na kifani
Vita vya Gaza vimeacha kiwango kisicho na kifani cha uharibifu, huku tani milioni 51 za vifusi zikifunika mandhari ambapo vitongoji vilivyokuwa na shughuli nyingi vilikuwa vikiendelea.
Kulingana na ripoti mpya ya tathmini ya uharibifu na mahitaji ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 60 ya nyumba ambazo ni takriban nyumba 292,000 na asilimia 65 ya barabara zimeharibiwa katika eneo la takriban kilomita za mraba 360.
Wakati jumuiya ya kimataifa inatafakari mustakabali wa Gaza na jinsi ya kuijenga upya, Al-Majdalawi ana jambo moja la uhakika "Hatutaondoka. Hilo halitatokea. Hii ni ardhi yetu."
Waathirika ni wengi
Akiendelea kwa tahadhari kupitia na kufufua vifusi, Yasser Ahmed anasema “Natafuta makaratasi yangu.”
Utafutaji wake wa kukata tamaa unakuwa mgumu zaidi kwa sababu majengo ya jirani yameanguka juu ya kila moja.
“Labda wakati ninapoondoa vifusi, nitapata mwili wa binadamu, au kifaa cha mlipuko,” anaongeza, akionyesha hatari kubwa ya kihisia na kimwili ya kuondoa magofu yaliyosalia katika eneo la vita.
“Labda wakati ninapoondoa vifusi, nitapata mwili wa binadamu, au kifaa cha mlipuko,” anaongeza, akionyesha hatari kubwa ya kihisia na kimwili ya kuondoa magofu yaliyosalia katika eneo la vita.
Kwa kushirikiana na wizara ya kazi za umma na makazi ya Palestina, Shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo UNDP linatoa msaada kwa watu wa Palestina na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP, wanaongoza kikundi cha usimamizi wa vifusi kinachojumuisha zaidi ya mashirika 20 kusaidia kukabiliana na suala hili muhimu kote Ukanda wa Gaza.
Uzoefu wa mashirika ya UN
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatumia uzoefu wa kina kutoka Mosul, Iraq, na miji ya Syria ya Aleppo na Latakia maeneo yote yaliyoharibiwa na vita.
UNOPS, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa huduma za miundombinu, ununuzi, na usimamizi wa miradi kote duniani, ni sehemu ya kikosi kazi cha usimamizi wa vifusi Gaza.
Shirika hilo, ambalo limefanya tathmini za tishio na hatari kote katika eneo hilo, limeunda mbinu za kisasa za GeoAI na teknolojia za kuhisi kwa mbali, ikiwemo uchunguzi wa muundo wa 3D, ili kuboresha tathmini ya hatari za vilipuzi na mikakati ya kuondoa vifusi.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNOPS, Jorge Moreira da Silva, baada ya ziara yake ya hivi karibuni Gaza, alisema kuwa elimu kuhusu hatari za vilipuzi imetolewa kwa Wapalestina 250,000 na wahudumu wa misaada wapatao 1,000, ikitoa "ujuzi muhimu wa kukaa salama na kukabiliana na hatari za vilipuzi kwa ufanisi."
UNDP, shirika linalosaidia nchi kupunguza umaskini, kujenga uthabiti, na kufanikisha maendeleo endelevu, lilianza kuondoa vifusi kutoka Gaza mwezi Desemba 2024, wiki chache kabla ya kusitishwa kwa mapigano kuanza kutekelezwa.
Tani 28,500 za vifuzi ziliondolewa
UNDP kupitia mwakilishi wake, Sarah Poole, inasema kuwa takriban tani 28,500 za vifusi ziliondolewa awali, huku tani 290 zikitumika katika kazi za barabara ili kuboresha shughuli za misaada ya kibinadamu, kurejesha upatikanaji wa maeneo muhimu kama hospitali, maduka ya mkate, na kituo muhimu cha usambazaji wa maji.
Poole ameelezea suala la umiliki wa ardhi na mali huko Gaza kuwa “gumu sana hasa wakati hati za umiliki, kumbukumbu za urithi, na nyaraka nyingine za kisheria zinapopotea au kuharibiwa.”
Amjad Al-Shawa, Mkurugenzi wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs katika Ukanda wa Gaza, anasema suala la vifusi linawakilisha “changamoto kubwa. Tunahitaji utaratibu wa kuondoa vifusi ambao utachukua muda mrefu, na unahitaji rasilimali ambazo hazipatikani Gaza,” anasema akiongeza kuwa “Leo, vifusi hivi pia vinawakilisha mali za wakazi. Mizozo mingi inaweza kutokea kati ya familia.”
Dola milioni 7 zimetolewa kusaidia kusafisha vifusi
Hadi sasa, kiasi cha dola milioni 7 kimetolewa na wafadhili mbalimbali kusaidia kuondoa vifusi lakini Poole anasema kuwa kiasi cha ziada cha dola milioni 40 kinahitajika “katika hatua hii ya awali ili kuongeza kazi kwa kiwango kikubwa. Suala la upatikanaji wa vifaa vizito na uwezo wa kuviingiza ni muhimu sana,” ameongeza.
Changamoto iliyo mbele ni kubwa
Changamoto inayokuja inaonekana kuwa kubwa. Vitongoji ambavyo vilikuwa vikichanua sasa vimesambaratishwa hakuna kilichosalia katika eneo hili ambapo watu wanaotimiza umri miaka 18 tayari wamepitia migogoro mikubwa ya silaha mara tano, uharibifu wa wakati huu ni mbaya zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Gharama ya uharibifu wa miundombinu ya kimwili inakadiriwa kuwa takriban dola bilioni 30, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Sekta ya makazi imeathirika zaidi, kwa hasara zinazofikia dola bilioni 15.8, huku gharama za kujikwamua na ujenzi upya zikikadiriwa kuzidi dola bilioni 53.
“Hakuna maisha ya makazi hapa. Natazama pande zote na naona uharibifu tu,” anasema Yasser Ahmed, akisimama mbele ya mabaki ya nyumba yake.
“Kazi ngumu ya miaka 59, miaka ya maisha yangu imepotea, na kila kitu kimeangamia. Kila kitu kipo chini ya vifusi,” anasema akiongeza kuwa “Ninaikumbuka nyumba yangu mtu hupata faraja tu katika nyumba yake na mahali pake mwenyewe.”
“Kazi ngumu ya miaka 59, miaka ya maisha yangu imepotea, na kila kitu kimeangamia. Kila kitu kipo chini ya vifusi,” anasema akiongeza kuwa “Ninaikumbuka nyumba yangu mtu hupata faraja tu katika nyumba yake na mahali pake mwenyewe.”
Ramadan ni muathirika mwingine
Karibu naye, Ramadan Katkat ameketi juu ya mabaki ya nyumba yake. Akiishi kwenye mahema yaliyosimamishwa kwa shida juu ya lundo la kifusi, anashiriki huzuni inayohisiwa na wengi.
Chini yake kunaweza kuwa na mchanganyiko hatari wa mabomu yasiyolipuka na miili ya binadamu.
Tamaa yake ni moja tu “Tunataka kuishi.” Hata hivyo, Al-Majdalawi anasisitiza kwa uthabiti kwamba “Tuna uwezo wa kuijenga upya ardhi hii.”
Wiki ijayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatarajiwa kuelekea Cairo Misri kwenye mkutano wa jumuiya ya nchi za Kiarabu utakaojadili ujenzi mpya wa Gaza.