Watoto wa Haiti wanalipa gharama kubwa ya mgogoro unaoendelea: UNICEF
Watoto wa Haiti wanalipa gharama kubwa ya mgogoro unaoendelea: UNICEF
Sheria na Kuzuia Uhalifu
Mgogoro unaoendelea nchini Haiti unawaathiri sana watoto wa nchi hiyo, ambapo maelfu ya watoto wanashinikizwa kujiunga na vikundi vya wahalifu vyenye silaha nzito kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi UNICEF imeonya kwamba kadri hali ya magenge ya uhalifu inavyoshika kasi, nafasi za watoto kupata elimu na maisha bora zinapotea haraka.
Geetanjali Narayan, mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti, ameonya leo kwamba vurugu zinazozidi kuongezeka na kuajiriwa kwa watoto katika makundi ya wahalifu zinawasukuma watoto wengi wa Haiti kutumbukia katika hali mbaya.
Uharibifu wa shule unawaacha watoto mila mahali pa kujifunza
Katika wiki chache zilizopita, UNICEF inasema vurugu zimeathiri sana mfumo wa elimu nchini Haiti.
Mwezi jana tu, vikundi vyenye silaha viliharibu shule 47 katika mji mkuu, Port-au-Prince, na kuongeza idadi ya shule zilizoharibiwa mwaka 2024 kufikia 284. Narayan wa UNICEF amesisitiza athari mbaya kwa uwezo wa watoto kujifunza, akionyesha kuwa mashambulizi haya yanaongezeka na kuacha maelfu ya watoto bila fursa ya kupata elimu.
Amesema “Mashambulizi yasiyokoma dhidi ya mfumo wa elimu yanazidi kuongezeka, yakiwaacha maelfu ya watoto bila mahali pa kujifunza,” akisisitiza ukubwa wa mgogoro.
Watoto wanaingizwa kwenye magenge ya uhalifu
Amesema vurugu dhidi ya watoto zinazidi kuongezeka wakati magenge ya wahalifu yakiwajumuisha watoto.
Matokeo ya vurugu hizi yanazidi kuathiri zaidi watoto kuliko uharibifu wa miundombinu.
Kwa mujibu wa UNICEF, kuajiriwa kwa watoto katika makundi yenye silaha kumeongezeka kwa asilimia 70 mwaka 2024.
Ripoti zinaonyesha kuwa nusu ya wanachama wa vikundi hivi ni watoto, baadhi wakiwa na umri wa miaka minane tu.
Narayan ameelezea kwa uchungu jukumu la watoto hawa katika vikundi vyenye silaha, ambapo watoto wadogo hutumika kama wajumbe au wasemaji, wakati watoto wakubwa wanashiriki katika vitendo vya vurugu.
UNICEF imesema kuajiriwa huku kunaashiria hasara kubwa ya kupoteza utoto wao, kwani watoto hawa wengi wanashurutishwa kutekeleza vitendo vya vurugu chini ya vitisho, jambo linalosababisha madhara makubwa ya kisaikolojia.
Madhara ya kisaikolojia kwa watoto kuingizwa katika mage ya wahalifu
Madhara ya kisaikolojia kwa watoto hawa kutokana na ushiriki wao katika makundi yenye silaha ni makubwa.
Narayan ameelezea madhara hayo kama “yasiyoweza kuelezeka,” akisisitiza kuwa ubongo wa watoto bado unakua kwa umri mdogo, hivyo kuwafanya kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata athari za kudumu za uathiriwa na vurugu.
“Kuwa sehemu ya magenye yenye silaha ambapo unazungukwa na vurugu kila wakati na ambapo wewe mwenyewe unaweza kulazimika kutekeleza vitendo vya vurugu kuna athari kubwa kwa mtoto,” amesema.
Matokeo ya muda mrefu kwa watoto hawa yanatarajiwa kudumu kwa miaka mingi, kama si katika maisha yao yote.
UNICEF inafanya kazi ya kuwaachilia na kuwarudisha watoto waliojumuishwa kwenye magenge ya wahalifu
Licha ya changamoto, UNICEF inafanya kazi kwa bidii kusaidia kuachiliwa na kurudisha watoto wa kivita kwenye jamii.
Itifaki ya makabidhiano iliyosainiwa mwaka 2024 kati ya Umoja wa Mataifa, UNICEF, na serikali ya Haiti imefanikiwa kurejesha watoto zaidi ya 100 mwaka jana.
Narayan amesisitiza kuwa juhudi zaidi zinahitajika, akieleza kuwa mchakato wa kurudisha watoto unawapa watoto nafasi ya kurejea kwao na, katika hali nyingi, kuendelea na elimu yao. Hata hivyo, juhudi hizi zinahitaji msaada zaidi na fedha ili ziweze kuwa na ufanisi.
Ukosefu wa fedha unatishia juhudi za UNICEF
Juhudi za UNICEF kusaidia watoto wa Haiti zinakutana na upungufu mkubwa wa fedha.
Shirika hilo limeomba dola milioni 38 kutekeleza hatua muhimu, kama vile kuunda maeneo ya muda ya kujifunza kwa watoto waliofurushwa na kurekebisha shule zilizoharibiwa.
Hata hivyo, fedha kwa ajili ya juhudi hizi kwa sasa ni asilimia 5 tu ya kiasi kinachohitajika.
Narayan amesisitiza dharura ya hali hiyo, akieleza kuwa zaidi ya watoto nusu milioni hawawezi kupata elimu kutokana na athari za vurugu na ukosefu wa fedha. Zaidi ya hayo, kupunguzwa kwa misaada ya kibinadamu kutoka Marekani kumeongeza hali mbaya ya mgogoro wa Haiti, na kuacha huduma muhimu za UNICEF zikididimia.
Changamoto kubwa ya ufadhili
Juhudi za jumuiya ya kibinadamu kukabiliana kushughulikia mgogoro nchini Haiti zimekuwa katika changamoto ya ufadhili.
Mwaka 2024, mpango wa dola milioni 600 ulizinduliwa, lakini ni asilimia 40 tu ya fedha zilizoidhinishwa ndio zimepatikana, na zaidi ya nusu yake zilitoka Marekani. Licha ya ujasiri mkubwa wa watoto wa Haiti, hali inaendelea kuwa mbaya, na wengi wako katika hatari ya utapiamlo, magonjwa yanayoweza kuzuiwa, na maumivu ya muda mrefu.
Kama alivyosema msemaji wa UNICEF, James Elder, hatua za haraka na fedha zinahitajika ili kuzuia mateso zaidi na kuhakikisha kuwa watoto wa Haiti wanapata fursa ya kujenga maisha bora.