DRC inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha magonjwa ambayo hayajatambuliwa na vifo katika jimbo la Equateur
DRC inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha magonjwa ambayo hayajatambuliwa na vifo katika jimbo la Equateur
Mamlaka ya afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na wataalamu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kundi jingine wa magonjwa na vifo vya watu katika jimbo la Equateur.
Katika miezi ya hivi karibuni, ufuatiliaji wa magonjwa umeonesha ongezeko la magonjwa na vifo katika maeneo matatu tofauti ya nchi, na kusababisha uchunguzi zaidi ili kuthibitisha chanzo cha magonjwa na kutoa msaada unaohitajika.
Tangu mwanzo mwa mwaka 2025, mkoa wa Equateur umekumbwa na mfululizo wa magonjwa na vifo vya watu. Mlipuko wa magonjwa wa hivi karibuni umetokea katika eneo la afya la Basankusu, ambapo wiki iliyopita watu 141 walikumbwa na magonjwa, bila ya vifo kuripotiwa. Katika eneo hilo hilo la afya, magonjwa 158 na vifo 58 viliripotiwa mapema mwezi Februari. Mnamo Januari, eneo la afya la Bolamba liliripoti watu 12 waliokumbwa na magonjwa, vikiwemo vifo 8.
Dalili ya magonjwa haya kulingana na utafiti
Ufuatiliaji wa magonjwa umebaini kuwa watu 1096 walikumbwa na magonjwa na vifo 60 vilitokea katika Basankusu na Bolomba, wakionesha dalili za homa, maumivu ya kichwa, baridi, jasho, maumivu ya shingo, maumivu ya misuli, maumivu ya viungo vingi, kutokwa na damu puani, kukohoa, kutapika na kipindupindu. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakutana na mizozo na milipuko mingi kwa wakati mmoja, na kuleta mzigo mzito kwa sekta ya afya na wananchi.
Wanachokifanya ili kuyakabili magonjwa haya
Katika kukabiliana na mrundikano huu wa magonjwa, timu ya msaada wa haraka kutoka Kinshasa na Equateur, pamoja na wataalamu wa dharura wa WHO, walitumwa katika maeneo ya Basankusu na Bolomba ili kuchunguza hali hiyo na kubaini kama kuna mwelekeo usio wa kawaida. Wataalamu hawa wanaboresha ufuatiliaji wa magonjwa, kufanya mahojiano na wanajamii ili kuelewa hali halisi, na kutoa matibabu kwa magonjwa kama vile malaria, homa ya matumbo (typhoid), na homa ya uti wa mgongo (meningitis). WHO imepeleka vifaa vya dharura vya matibabu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kupima, na kuandaa itifaki kwa kina ili kuboresha uchunguzi wa magonjwa.
Uchunguzi wa maabara wa awali umeonesha kuwa sampuli zote hazikubaini virusi vya Ebola wala Marburg, lakini karibu nusu ya sampuli zilithibitishwa kuwa na malaria, ambayo ni kawaida katika eneo hilo. Uchunguzi zaidi utafanywa kwa uti wa mgongo, na sampuli za chakula, maji na mazingira pia zitachunguzwa ili kubaini kama kuna uchafuzi. Sampuli mbalimbali zitapelekwa kwa uchunguzi zaidi katika maabara ya kitaifa huko Kinshasa.
Changamoto katika upatikanaji wa huduma za afya
Basankusu na Bolomba yana umbali wa kilomita 180, na zaidi ya kilomita 300 kutoka mji mkuu wa Mbandaka. Umbali huu unaleta changamoto kubwa kwa upatikanaji wa huduma za afya, ikiwa ni pamoja na vipimo na matibabu. Miundombinu duni ya barabara na mawasiliano pia ni changamoto kuu. WHO inaunga mkono mamlaka za afya za ndani kuimarisha uchunguzi na hatua za majibu, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya wahudumu wa afya ya jamii zaidi ya 80 ili kugundua na kuripoti mlipuko wa magonjwa haya na vifo.
Juhudi zaidi zinahitajika ili kuimarisha vipimo, ugunduzi wa mapema wa magonjwa hayo, na ufuatiliaji wa ripoti, sio tu kwa tukio hili bali pia kwa milipuko ya baadaye. WHO inasalia nchini DRC kutoa msaada kwa wahudumu wa afya, ikishirikiana kwa karibu na mamlaka ya afya ya kanda mkoa na kitaifa, ili kutoa vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha na kuratibu majibu ili kupunguza kuenea kwa magonjwa na milipuko mengine katika eneo hilo.