Miaka miwili ya vita Sudan, wananchi wanastahili hatua bora zaidi - OCHA
Miaka miwili ya vita Sudan, wananchi wanastahili hatua bora zaidi - OCHA
Mapigano ya takribani miaka miwili nchini Sudan kati ya jeshi la serikali, SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF, yamesababisha machungu na kugeuza baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kuwa kama jehanamu, amesema Edem Wosornu, Afisa kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya kibinadamu, OCHA, wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Baraza hilo limekutana leo jijini New York, Marekani kujadili hali ya kibinadamu Sudan,kwa mujibu wa azimio namba 2715 linalotaka Katibu Mkuu kuwasilisha ripoti kila baada ya siku 120 ambapo Bi. Wosornu alihutubia kwa niaba ya Mkuu wa OCHA, Tom Fletcher.
“Baadhi ya takwimu za kibinadamu zitokanazo na janga hili zinafaa kurudiwa kuelezwa. Zaidi ya watu milioni 12 wamefurushwa makwao, wakiwemo milioni 3.4 waliokimbilia nchi jirani,” amesema Bi. Wosornu.
Zaidi ya watu milioni 24.6 sawa na zaidi ya nusu ya idadi ya wananchi wa Sudan, wanakabiliwa na njaa.
Kama hiyo haitoshi, huduma za afya zimesambaratika, mamilioni ya watoto wanakumbwa na kiwewe na hawako shuleni. Ukatili wa kingono umefurutu ada.
Ghasia Zamzam zimefurusha wahudumu wa kibinadamu
Bi. Wosornu akageukia kambi ya Zamzam ambako huko amesema kuna hali ya kutisha. “Darfur Kaskazini, ambako miezi 8 iliyopita Baraza hili lilipitisha azimio namba 2736, raia wanaendelea kushambuliwa.”
Amesema picha kutoka angani zinathibitisha matumizi ya hivi karibuni silaha nzito kwenye eneo la Zamzam na viunga vyake na uharibifu wa soko kuu ndani ya kambi hiyo. Raia wakiwa wamejaa hofu, wakiwemo wahudumu wa kibinadamu, walishindwa kuondoka eneo hilo pindi mapigano yaliposhika kasi. Wengi wao waliuawa, wakiwemo wahudumu wawili wa kiutu.
Tayari Jumatatu wiki hii Madaktari Wasio na Mipaka, MSF, ambao ndio watoa huduma tegemewa wa chakula na afya kambini Zamzam walitangaza kusitisha huduma zao kambini kutokana na hali ya usalama kudorora.
“Na leo hii, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP limethibitisha kusitisha msaada wake wa vocha za fedha kwa wakimbizi wa ndani kambini Zamzam, kutokana na ukosefu wa usalama na kushambuliwa kwa soko.”
Hivyo ametaja mambo makuu matatu ambayo OCHA inapenda kuona yanachukuliwa hatua.
Mosi: Ulinzi wa raia
Baraza la usalama na nchi zote wanachama zenye ushawishi na pande kinzani Sudan zichukue hatua ya haraka kuhakikisha pande zote zinazingatia sheria za kimataifa za kiutu, zinalinda rai ana miundombinu wanayotegemea.
Pili: Ufikishaji misaada
“Tunahitaji utekelezaji wa uhakika na wa kweli wa ahadi zote zilizotolewa ili kuwezesha misaada ya kiutu kufikia wahitaji kwa haraka na bila vikwazo,” amesema Bi. Wosornu.
Tatu: Ufadhili wa fedha
Kwa mujibu wa OCHA, kiwango cha mahitaji Sudan ni kikubwa kuliko ilivyotarajiwa na hivyo mahitaji ya fedha nayo ni makubwa. “Tunahitaji uhamasishaji wa kimataifa wa usaidizi wa fedha na pia upatikanaji wa fedha kuendana na wakati.
Ametamatisha kwa kusema, “raia wa Sudan wanastahili jambo bora zaidi kutoka kwa viongozi wa jumuiya ya kimataifa. Lazima tuchukue hatua zaidi ambazo zitafungua milango kwa mamilioni ya watu waliolazimika kukimbia makwao. Sasa kuliko wakati wowote ule, miaka miwili sasa, wananchi wa Sudan wanahitaji hatua zenu.”
Mfungo wa Ramadhani uwe na utulivu
Kwa kiasi kikubwa wajumbe waliopata fursa ya kuzungumza kwenye kikao wametaka mamlaka huru, mipaka na uhuru wa Sudan uheshimiwe na kwamba kuelekea mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhani, unaoanza mwishoni mwa wiki hii, pande zote kinzani zinyamazishe silaha kwa ajili ya amani.
Mathalani Mwakilishi wa China amekumbusha kuwa mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kutaka sitisho la mapigano wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tunaomba na mwaka huu pande kinzani zizingatie wito huo.
Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ekitela Lokaale ameeleza wajumbe jinsi serikali ya Kenya ilivyoweka mazingira kwa pande kinzani nchini Sudan kuweza kufanyia vikao vyao jijini Nairobi, kama njia ya kufanikisha amani.
Mara baada ya kikao cha wazi, wajumbe waliingia kwenye mashauriano ya faragha yaliyomjumuisha pia Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Ramtane Lamamra.
Lamamra asisitiza utashi wa wasudani uzingatiwe
Mapema akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa, Bwana Lamamra amesema suluhisho lolote la amani Sudan lazima lizingatie uhuru na umoja wa nchi hiyo.
“Jawabu hilo lazima liwe la kisiasa, na litegemee busara na uwezo wa kupatia suluhu chanzo cha SAF na RSF kutumbukia kwenye mapigano. Wananchi wa Sudan ni huru na wawe na kauli ya mwisho kwenye mustakabali wao,” amesema Bwana Lamamra.
Amesema kwa upande wake yeye anafanya kila juhudi kushawishi pande kinzani na wapitisha maamuzi kuwa jawabu lolote lazima liwe na mzizi kutoka utashi wao wa pamoja wa kisiasa.
Amesisitiza umuhimu wa kupatia kipaumbele ulinzi wa raia, akisisitiza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa sitisho la uhasama wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kutamatisha mahojiano yake ya kusisitiza udugu wakati wa mwezi huo mtukufu.
“Ujumbe wangu ni ujumbe wa udugu. Ujumbe uliobeba maadili ya kiislamu yanayothaminiwa na waislamu na wasio waislamu. Wahusika lazika wafuate mafundisho halisi ya kiislamu na kukubali uhai wa binadamu. Matumaini yetu ni kwamba ndugu zetu watatumia fursa hii kufikiria kuhusu Ramadhani isiyo na vurugu, Ramadhani iliyojaa udugu na matarajio ya mustakabali bora.”