Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Nchini DRC, makumi wafa, mamia waambukizwa ugonjwa usiojulikana

Mfanyakazi wa matibabu akiwa amevaa vifaa kamili vya kujikinga anasimama ukutani, akifanya ishara ya msalaba kwa mikono yake.
UN Photo/Martine Perret Mhudumu wa afya wa nchini DRC (Maktaba)

WHO: Nchini DRC, makumi wafa, mamia waambukizwa ugonjwa usiojulikana

Afya
  • Mpaka sasa WHO inaendelea na uchunguzi
  • Sampuli 13 zimeonesha si Ebola wala Marburg
  • Eneo liko ndani na halina maabara wala ufuatiliaji wa magonjwa

Kufuatia ripoti za kuweko kwa ugonjwa usiojulikana huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambao tayari umeambukiza mamia ya watu na kusababisha makumi ya vifo, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, limesema bado linaendelea na uchunguzi wa ugonjwa huo uliotangazwa kwa chapisho la kikanda la WHO.

Msemaji wa WHO, Tarik Jašarević amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa hadi sasa sampuli 13 zilizofanyiwa uchunguzi zimeonesha kuwa ugonjwa huo si Ebola wala homa ya Marburg, na kwamba WHO inaendelea kuchunguza kubaini ni kitu gani.

Hatufahamu kama ni simu au ni kijiumbe maradhi

WHO inaendelea kuchunguza kufahamu iwapo ni aina nyingine ya mdudu mwenye maambukizi ya magonjwa au ni sumu,” amesema Jašarević na kuongeza kuwa sumu ni kitu ambacho wananchi wanaweza kuwa wamekula na kusababisha madhara, na kiumbe ambukizi kuwa ni kitu ambacho kinasambaa miongoni mwa watu.

“Maeneo ambako ugonjwa huo usiojulikana umeripotiwa kuweko, ni maeneo ya ndani yenye ufuatiliaji hafifu wa maradhi na pia miundombinu isiyotosheleza ya afya,” amesema afisa huyo wa WHO akiongeza kuwa eneo hilo bila kulitaja jina, halina maabara.

Amesema hivi sasa ni muhimu kwa WHO kusaidia mamlaka za afya nchini DRC ili kuweza kubaini ugonjwa huo.

Msemaji huo amesisitiza kuwa "hadi sasa WHO haifahamu ugonjwa huo uko katika kiwango gani na hivyo inahitaji kufanya uchunguzi zaidi."

Kwa sasa WHO inawasiliana na mamlaka za afya za DRC ili kubaini aina ya msaada unaohitajika.