Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza lazima isalie kuwa sehemu muhimu ya taifa la baadaye la Palestina - Sigrid Kaag

Mwanamke amesimama nje ya makazi yake ya hema huko Gaza.
© UNRWA
Mwanamke amesimama nje ya makazi yake ya hema huko Gaza.

Gaza lazima isalie kuwa sehemu muhimu ya taifa la baadaye la Palestina - Sigrid Kaag

Msaada wa Kibinadamu

Eneo la Mashariki ya Kati kwa sasa linapitia mabadiliko makubwa kwa kasi, na hii inaweza kuwa fursa ya mwisho ya kutekeleza suluhisho la mataifa mawili, yaani Palestina na Israeli, amesema Mratibu Maalum wa Mchakato wa Amani wa Mashariki ya Kati na Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Ukarabati wa Gaza, Sigrid Kaag, wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama leo Jumanne katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Baraza la Usalama limekutana katika mkutano wake wa kila mwezi kuhusu Hali Mashariki ya Kati ikiwemo hoja ya Palestina, MEPQ.

Kaag amekaribisha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya usitishaji mapigano, ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa mateka 34 wa Israeli, lakini akalaani vitendo vya Hamas vya kuwaonesha hadharani mateka walioachiliwa, kuwashinikiza kutoa matamko kwa nguvu, na kuonesha miili ya waliofariki dunia.

Kama sehemu ya makubaliano ya usitishaji mapigano, wafungwa na mahabusu 1,135 wa Kipalestina wameachiliwa hadi sasa, amesema Kaag, akiongeza kuwa ripoti za mateso na fedheha walizopitia wakati wakiwa kizuizini ni za kushtusha.

Juhudi za kibinadamu na ukarabati wa Gaza

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu Januari 19, ambapo awamu ya kwanza ya mpango wa usitishaji mapigano ilianza kutekelezwa, Umoja wa Mataifa na wadau wake wameongeza kiwango cha misaada ya kibinadamu Gaza. Uokoaji wa wagonjwa kupitia mpaka wa Rafah ulianza pia Februari 1. 

“Lazima kuepuka kurejea katika mapigano kwa gharama yoyote. Natoa wito kwa pande zote mbili kutekeleza kikamilifu ahadi zao chini ya makubaliano ya usitishaji mapigano na kukamilisha awamu ya pili ya mazungumzo.” amesema Kaag.

Amekumbusha kuwa, kwa mujibu wa makadirio ya awali, urejeshaji wa Gaza katika hali nzuri utahitaji dola bilioni 53.

Hali katika Ukingo wa Magharibi

“Wakati jumuiya ya kimataifa inaendelea kuangazia Gaza, nina wasiwasi kuhusu operesheni za kijeshi, mashambulizi, na ongezeko la vurugu katika Ukingo wa Magharibi,” amesema Kaag.

Ameeleza kuwa vikosi vya Israel vinafanya mashambulizi ya anga na kutumia silaha nzito, huku wapiganaji wa Kipalestina wakifanya mashambulizi kwa kutumia vilipuzi vya kutengenezwa kienyeji na bunduki.

Shughuli haramu za ujenzi wa makazi ya walowezi zinaendelea pia, kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa, ambapo takriban nyumba 2,000 mpya zimejengwa katika wiki za hivi karibuni, hasa katika Eneo C. Ubomoaji wa nyumba za Wapalestina na kufukuzwa kwao vimeongezeka, huku vikwazo vikali vya usafiri vikiendelea kulemaza maisha ya kila siku ya Wapalestina wengi.

“Matukio haya, pamoja na wito unaoendelea wa kutwaliwa kwa ardhi, ni tishio la moja kwa moja kwa uwezekano wa kuundwa kwa taifa la Palestina lenye uhuru na uwezo wa kujitegemea, na hivyo basi, suluhisho la mataifa mawili,” alisema Kaag.

Mustakabali wa maeneo ya Palestina

Mratibu Maalum ametoa wito wa kuhakikisha kuwa Gaza inasalia kuwa sehemu muhimu ya taifa la baadaye la Palestina. Kwa mujibu wake, Gaza na Ukingo wa Magharibi, ukiwemo Jerusalem Mashariki, vinapaswa kuwa na umoja wa kisiasa, kiuchumi, na kiutawala. Uwepo wa muda mrefu wa jeshi la Israel Gaza unapaswa kuepukwa, huku wasiwasi wa Israel kuhusu usalama wake ukizingatiwa.

“Tunapaswa kujitolea kumaliza ukaliaji wa kimabavu na hatimaye kutatua mgogoro huu kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa, na makubaliano ya awali,” amesema Kaag.

Ili kufanikisha malengo haya, ni muhimu kuendelea kuunga mkono utekelezaji kamili wa makubaliano ya usitishaji mapigano, ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa mateka wote, amesisitiza. Aidha, ni muhimu kutoacha kufuatilia "hali hatari" katika Ukingo wa Magharibi na kufanya kazi kuelekea "upunguzaji wa mivutano kwa haraka."

Zaidi ya hayo, Kaag ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono Mamlaka ya Palestina katika kufanya mageuzi na kurejesha mamlaka yake katika Ukanda wa Gaza. Vikosi vya usalama vya Palestina vinapaswa pia kupewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao katika maeneo waliyopewa mamlaka. Msaada wa kisiasa na kifedha kwa juhudi za kurejesha na kujenga upya Gaza unahitajika, ameongeza Kaag.

Msaada wa afya na chakula

Wakati huo huo, akizungumza katika kikao cha waandishi wa habari mjini Geneva leo, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani (WHO) katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu (OPT), Rick Pieperkorn, amesema takribani watoto 548,000 wamepewa chanjo ndani ya siku tatu za kampeni mpya ya chanjo ya polio Gaza, ikiwa ni zaidi ya asilimia 92 ya kiwango kilichopangwa.

Pia shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani (WFP) limesema kuwa usitishaji mapigano Gaza umesababisha ongezeko maradufu la kiwango cha chakula kinachoingizwa Gaza kila mwezi. Watu milioni moja wamepokea msaada wa WFP, ikiwa ni pamoja na vifurushi vya chakula, milo ya moto, mkate mpya, na msaada wa kifedha.