Awamu ya tatu ya chanjo dhidi ya polio inaendelea Gaza
Awamu ya tatu ya chanjo dhidi ya polio inaendelea Gaza
Uchanjaji huu wa sasa kwa njia ya matone dhidi ya polio ni wa dharura kutokana na kugunduliwa kwa virusi vya polio katika sampuli za maji taka huko Gaza hivi karibuni, ikionesha kuwa virusi hivyo vinaendelea kuzunguka katika mazingira na hivyo kuwaweka watoto katika hatari.
Hakuna maambukizi mapya ya polio yaliyoripotiwa tangu mtoto wa miezi kumi alipopooza mwezi Agosti mwaka jana2024, lakini sampuli za maji kutoka Deir al-Balah na Khan Younis, zilizokusanywa mwezi Desemba 2024 na Januari 2025, zinathibitisha ueneaji wa virusi vya polio, huku aina ya virusi vilivyogunduliwa vikihusiana kijenetiki na virusi vya polio vilivyogunduliwa katika Ukanda wa Gaza mnamo Julai mwaka jana 2024.
Dkt. Richard Peeperkorn, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, (WHO) katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa, anafafanua akisema,
" Tuko hapa kaskazini mwa Gaza hapa Hospitali ya Kamal Adwan. Kampeni hii imeandaliwa na Wizara ya Afya, WHO, UNICEF, UNRWA na wadau wengine wenye malengo mawili makuu. Kwanza, kuzuia ueneaji wa virusi vya polio ndani ya Gaza na pili, kuzuia kusambaa kwa virusi vya polio nje ya Gaza. Lengo ni kuwachanja zaidi ya watoto 590,000 kote Gaza katika kampeni itakayodumu kwa siku tatu, pamoja na siku mbili za nyongeza kwa wale waliokosa chanjo. Hili ni zoezi kubwa la vifaa na rasilimali, likihusisha zaidi ya timu 1,650, kati ya hizo, timu 1,250 ni za kuhamahama na vituo 420 vya kudumu."
Katika hospital hii ya Kamal Adwan, Gaza Kaskazini, Hana Khalil Majeed ambaye ni mchanjaji anaonekana akimwekea mdomoni matone ya chanjo mtoto mmoja anaeleza kwamba "hii ni kampeni ya tatu dhidi ya polio na wamekuta idadi kubwa ya familia, hasa katika eneo la kaskazini, wakija kuwachanja watoto wao. Kundi lengwa kwa chanjo ni watoto kuanzia umri wa siku moja hadi miaka 10. Anasema,wameshuhudia mwitikio mkubwa kutoka kwa watu waliokuja kuwachanja watoto wao na mwanzoni, walidhani eneo hili litakuwa tupu, lakini wanamshukuru Mungu, idadi kubwa ya watu kutoka eneo la kaskazini wamekuja."
Miongoni mwa waliokuja ili watoto wao wachanjwe ni mama huyu aliyembeba mtoto wake wa kike ambaye punde amepatiwa chanjo.
"Leo nimefika Kamal Adwan huku kaskazini, ili binti yangu apate dozi ya tatu ya chanjo. Amepokea chanjo ya kwanza huko Khan Younis katika Al-Qarara na ya pili huko Deir al-Balah. Leo, baada ya kurejea kaskazini, nimempa dozi yake ya tatu ya chanjo ya polio. Bila shaka, hii ni kwa ajili ya kuwalinda watoto wetu dhidi ya polio."