Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Majaji, mawakili mafichoni baada ya wafungwa kutoroka jela Goma, raia nao mashakani

Patrice Vahard, Mkuu wa Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu UN nchini DRC, anaonekana kwenye picha wakati wa ziara ya gereza huko Beni, Kivu Kaskazini, akizungumza na wafanyakazi UN na wanajeshi.
BCNUDH RDC Patrice Vahard, Mkurugenzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Pamoja ya Haki za Binadamu, UNJHRO, nchini DRC, akiwa ziarani Beni, Kivu Kaskazini.

DRC: Majaji, mawakili mafichoni baada ya wafungwa kutoroka jela Goma, raia nao mashakani

Haki za binadamu

Wakati waasi wa M23 ikiendelea kusonga mbele kuelekea ‘maeneo mengine ya kimkakati’ mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, baada ya kuteka miji ya Goma jimboni Kivu Kaskazini na Bukavu na Kamanyola jimboni Kivu Kusini Umoja Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu athari mbaya za kutoroka kwa wafungwa kulikoshuhudiwa Goma, pamoja na magereza makuu ya Kabare na Bukavu.

Baadhi ya wafungwa walikuwa ni wababe wa ukatili na watu hatari sana DRC kutokana na ukatili waliokuwa wametenda kwenye jamii ikiwemo ukatili wa kijinsia.

Katika mahojiano na Idhaa ya Kifaransa ya Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Pamoja ya Haki za Binadamu, UNJHRO, nchini DRC, Patrice Vahard, nchini DRC amebainisha kuwa kutokana na magereza kushambuliwa na kuharibiwa, waathiriwa sasa wanajikuta si tu wakiishi pamoja na watesi wao, bali pia wafungwa wa zamani wako huru, wakiweka hatari maisha ya majaji waliowahukumu hapo awali au mawakili waliowatetea wanawake manusura wa ukatili wa kingono.

Baadhi ya majaji na mawakili wanaishi mafichoni

"Hivyo, madhara yatakuwa makubwa, kwanza kwa utawala wa sheria, lakini hasa kwa wanawake hawa waliokuwa na imani katika haki kwa sababu walirejeshewa hadhi, lakini kwa bahati mbaya leo wanakabiliwa na hatari ya kukutana na watesi wao", amesema Vahard.

Kwa sasa, huku M23 ikiendelea kusonga mbele mashariki mwa DRC na kutoroka kwa wafungwa kukiendelea kuripotiwa, baadhi ya majaji na mawakili wanaishi mafichoni. "Wakati mawakili wanapofuatiliwa kwa sababu ya kuwatetea wateja wao, wakati majaji wanapolazimika kujificha kwa sababu waliamua haki, au wakati wanachama wa familia zao wanatishwa, ni lazima kila mtu aungane ili kulinda utawala wa sheria nchini DRC".

Tahadhari hii inakuja siku moja baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kilichofanyika Jumatano huko New York ambapo Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO, alikumbusha kuhusu maombi ya msaada wanaopokea kila siku kutoka kwa Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Miongoni mwao ni "maombi ya ulinzi binafsi kutoka kwa wadau mbalimbali wa kijamii, wakiwemo watetezi wa haki za binadamu ambao mara kwa mara wanakabiliwa na vitisho na hatari za kulipizwa kisasi na M23 katika maeneo wanayodhibiti", alisema Bintou Keïta.