Ni kwa vipi ufinyu wa bajeti unaathiri vibaya operesheni za UN za ulinzi wa amani?
Ni kwa vipi ufinyu wa bajeti unaathiri vibaya operesheni za UN za ulinzi wa amani?
Historia ya ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa inaonesha ulianza miaka mitatu tu baada ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa wenyewe. Na kutokana na umuhimu wa ulinzi wa amani kote duniani, shughuli hiyo imedumu kwa miaka yote hiyo 77 hadi sasa na bado ni muhimu lakini inaendelea kukumbwa na changamoto.
Brigedia Jenerali George Mwita Itang’are, Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania (TPTC) chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ au TPDF anatoa wito kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono ulinzi wa amani duniani kwa kuzikabili changamoto wanazokutana nazo walinda amani.
“Changamoto ziko nyingi lakini changamoto kubwa kabisa ambayo ninaweza nikaisema vikundi vyetu vinakabiliana nayo ni paple ambapo wanajikuta kwamba wana majukumu makubwa lakini hakuna rasilimali za kutosha,” anasema Brigedia Jenerali Itang’are akiangazia ufinyu wa bajeti unaozikabili operesheni nyingi za ulinzi wa amani kote duniani.
Brigedia Jenerali Intang’are anatoa mfano wa moja ya vikundi vya Tanzania ambavyo vilivyokuwa katika shughuli za ulinzi wa amani vililazimika kujigawa katika makundi madogo madogo ili kutoa huduma katika eneo pana.
Anasema kikundi kililazimika, “kujigawanya katika vikundi zaidi ya tisa kwa wakati mmoja. Yaani kikundi kinagawanyika katika vikundi vidogovidogo vingi lakini katika eneo kubwa ambapo hata ikitokea tatizo ni vigumu kusaidiana au kutoa msaada wa kijeshi unaohitajika.”
Wito
Tanzania ni moja ya nchi 10 zinazochangia kwa wingi zaidi vikosi vya ulinzi wa amani duniani. Brigedia Jenerali Itang’are anatoa wito kwa nchi wanacahama wa Umoja wa Mataifa akisema,
“Wito wangu mimi ni kwamba Nchi Wanachama (wa Umoja wa Mataifa) zitekekeze maamuzi mbalimbali yaliyopo ili kuhakikisha operesheni za ulinzi wa amani zinapatiwa rasilimali za kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao kama ilivyokusudiwa lakini pia mamlaka nguvu ‘mandate’ zitolewe kulingana na hali halisi lakini zilenge kumaliza tatizo.”
Brigedia Jenerali Itang’are anasisitiza kuwa jukumu la ulinzi wa amani duniani sio la ncho moja, ni jukumu la wanachama wote wa Umoja wa Mataifa.
“Tanzania kama moja ya nchi ambayo ni mchangiaji mkubwa katika operesheni za ulinzi wa amani wito wetu sisi ni kuona nchi zote tunakuwa pamoja katika kuhakikisha mamlaka nguvu za hizo.
Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC)
Kituo hiki kilianzishwa mwaka 2003 kufuatia wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Boutros Boutros Ghali (1992 hadi 1996) kwenye taarifa yake ya ajenda ya ulinzi wa amani.
Tanzania iliitikia wito huo wa Umoja wa Mataifa wa kuona umuhimu wa kuwepo kwa vyuo vya ulinzi wa amani amani vya kikanda ili kupunguza changamoto ya kukosekana kwa amani katika nchi zenye migogoro duniani.