Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo DRC: OCHA yasihi kufunguliwa kwa viwanja vya ndege Goma na Kavumu

Mafundi wawili waliovaa fulana zinazoonekana sana wakiandaa ndege nyeupe isiyo na rubani yenye chapa ya UN kwenye lami kwenye uwanja wa ndege huko Goma, ikiwa na hangar kubwa nyuma.
UN Photo/Sylvain Liechti Ndege isiyokuwa na rubani au drone ikijiandaa kupaa huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo -DRC. (Maktaba)

Mzozo DRC: OCHA yasihi kufunguliwa kwa viwanja vya ndege Goma na Kavumu

Msaada wa Kibinadamu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likifanya kikao cha dharura jijini New York, Marekani kujadili hali ya usalama inayozidi kuzorota kila uchao huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya kibinadamu nchini humo, Bruno Lemarquis amesema kupanuka kwa mzozo huo kumezidi kugharimu maisha na mustakabali wa raia.

Kauli ya Bwana Lemarquis imo kwenye taarifa iliyotolewa Kinshasa, mji mkuu wa DRC na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya dharura OCHA, wakati huu ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameendeleza mashambulizi yao hadi jimboni Kivu Kusini na tayari wametwaa mji wa Bukavu.

Raia wanakimbia kusaka usalama wakikumbwa na mazingira magumu

Bwana Lemarquis amesema kasi kubwa ya kusambaa kwa mzozo huo hasa jimboni Kivu Kusini, inaendelea kuwa na madhara kwa raia kama ilivyoshuhudiwa na mwelekeo mpya wa raia waliolazimika kukimbia maeneo yenye mapigano katika mazingira magumu.

Amesema raia hawawezi kuendelea kulipa gharama kubwa ya mzozo huo unaoendelea kutishia utulivu wa ukanda mzima wa Maziwa Makuu.

Wafanyakazi wa WFP wakipakua chakula katika ghala huko Goma, DR Congo.
© WFP/Michael Castofas Msaada wa dharura wa kibinadamu unawasilishwa Goma mashariki mwa DR Congo.

Uporaji wa bidhaa za misaada ya kiutu

OCHA inasema kwa mara nyingine tena, tarehe 15 mwezi huu, uporaji uliripotiwa huko Bukavu, kwenye vituo vya kibinadamu pamoja na mabohari ya kuhifadhi misaada ya kibinadamu, kitendo kinachokwamisha uwezo wa mashirika ya kiutu kutoa huduma zao ambazo tayari zilishakumwba na mkwamo.

Ametaka pande zote kwenye mzozo, kufanikisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwa kuchukua hatua haraka kama vile kufungua uwanja wa ndege wa Goma jimboni Kivu Kaskazini, na ule wa Kavumu jimboni Kivu Kusini.

Wakimbizi wasilazimishwe kurejea makwao bila hiari

Halikadhalika kuheshimu haki za wakimbizi wa ndani, na kwamba hatua yoyote ya kuwataka raia warejee makwao lazima izingatie usalama wao, na ifanyike kwa hiari, na kwa mujibu wa kanuni za kimataifa.

Mama Masika Mukize na watoto wake wameketi mbele ya makazi ya muda huko Goma, DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire Familia iliyohamishwa na vita imeketi mbele ya makazi yao ya muda huko Goma, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.

Operesheni za kiutu haziegemei upande wowote

Mratibu huyo wa misaada ya kibinadamu amesisitiza kwamba  lengo pekee la timu za misaada ni kutoa msaada muhimu na ulinzi kwa wale walio katika hatari zaidi, “popote walipo na hatua hii inaongozwa na kanuni za kibinadamu za kutokupendelea upande wowote, kutoegemea upande, ubinadamu, na uhuru, bila kuchukua upande wowote au kushiriki katika masuala ya kisiasa.”

Dharura ya DRC ni moja ya mizozo mikubwa na migumu zaidi ya kibinadamu duniani; ikifuatiwa na miongo ya mapigano kati ya jeshi la serikali, FARDC na makundi yaliyojihami likiwemo la M23, makundi ambayo yanasababisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na unyanyasaji wa kijinsia.

Mahitaji ya kibinadamu ni mengi

Kwa sasa mahitaji ya kibinadamu ni makubwa sana na si tu mashariki mwa DRC, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, amablo limebainisha kuwa watu milioni 7 ndani ya taifa hilo la Ukanda wa Maziwa Makuu ya Afrika wamelazimika kuhama makazi yao na zaidi ya milioni 1 wamesaka hifadhi nje ya mipaka ya nchi.

Idadi kubwa wamepokelewa Angola, Burundi, Jamhuri ya Congo, Malawi, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Tanzania na Zambia.

Wakati huo huo, DRC - nchi yenye ukubwa mara saba ya Ujerumani - pia inapokea zaidi ya wakimbizi na waombaji hifadhi nusu milioni.

Mapigano ya hivi karibuni yaliyoshamiri kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu huko  mashariki mwa DRC tayari yamefanya mamia ya maelfu ya watu wasiojiweza kuhama katika kipindi cha wiki chache tu.

Kati ya watu 10,000 na 15,000 wamevuka mpaka na kuingia Burundi kwa muda wa siku chache ambapo UNHCR inatoa wito wa msaada wa haraka ili kuwasaidia wakimbizi na kuzuia mateso zaidi.