Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia DRC: M23 yataka MONUSCO ikabidhi raia inaowalinda Goma

Familia iliyohamishwa na vita wakiwa mbele ya makazi yao ya muda huko Goma, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire Familia iliyohamishwa na vita wakiwa mbele ya makazi yao ya muda huko Goma, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.

Ghasia DRC: M23 yataka MONUSCO ikabidhi raia inaowalinda Goma

Amani na Usalama

Waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wametaka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO uwakabidhi raia waliosaka hifadhi kwenye maeneo ya ujumbe huo mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hayo leo jijini New York, Marekani wakati akizungumza na waandishi wa habari akinukuu wafanyakazi wa Umoja huo nchini DRC wakisema hali ya usalama imesalia tete kwenye majmbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Madai ya M23 dhidi ya MONUSCO

“Jimboni Kivu Kaskazini, MONUSCO inaendelea kuhifadhi na kulinda takribani watu 1,400 kwenye maeneo yake Goma. M23 wanataka wakabidhiwe raia hao na wanalaani waziwazi kuwa MONUSCO imekuwa inaachiia wanajeshi wa serikali, FARDC kushambulia raia,” amesema Bwana Dujarric.

Ameongeza kuwa jana jumatatu umati mkubwa wa watu ulikusanyika nje ya kituo cha MONUSCO cha Lava lakini baadaye waandamanaji hao walitawanyika kwa amani.

“Wahudumu wetu wa kibinadamu nao wanaripoti kuwa katika siku za karibuni maeneo kadhaa ya kuhifadhi wakimbizi yamekumbwa na uporaji. Takribani wakimbizi 56,000 wamehamia kwenye vituo vipya 34 vilivyoanzishwa kwenye maeneo tofauti tofauti mjini Goma,” amesema Dujarric.

Wakati huo huo, wanawake, wanaume na watoto 390,000 bado wako kwenye kambi za wakimbizi mjini Goma na viunga vyake.

Miundombinu imeharibiwa

Amezungumzia pia uharibifu wa miundombinu kama vile shule ambapo amesema takribani 80 zimeharibiwa, vituo 27 vya afya vimeporwa au kuharibiwa, huduma ya elimu na afya imevurugwa.

Takribani wanafunzi 400,000 wameathiriwa vibaya na mapigano ya hivi karibuni mjini Goma na viunga vyake.

Huduma za kibinadamu zasitishwa Djugu, Ituri

Huko mjini Djugu, jimboni Ituri, Mashariki mwa DRC, ghasia zimelazimu wahudumu wa kibinadamu kusitisha huduma zao, na hivyo kuvuruga usaidizi kwa watu 30,000.

Huko Kivu Kusini, wadau wa kibinadamu wanaripoti kuweko kwa uporaji katika maeneo ya Bukavu, mwishoni mwa wiki ikiwemo katika bohari ya shirika la Mpango wa Chakula duniani, WFP.

Watu wamesaka hifadhi kwenye makanisa na vituo vya kuhifadhi watu, huku mamlaka zikiwa na hofu ya kusambaa kwa ugonjwa wa mpox jimboni Kivu Kusini, kwa kuwa wagonjwa wengi wamekimbia vituo vya tiba kuhofia usalama wao.