MONUSCO yaimarisha doria Ituri kufuatia mauaji ya raia 80
MONUSCO yaimarisha doria Ituri kufuatia mauaji ya raia 80
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, umeimarisha doria huko jimboni Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia shambulio lillilofanywa na waasi wa CODECO mapema wiki hii.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amewaambia waandishi wa habari hii leo kwamba doria hizo zinalenga kulinda raia.
“Mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita, tayari amelaani shambuli hilo la kikatili lililosababisha vifo vya raia 80,” amesema Dujarric.
Jumanne ya wiki hii, MONUSCO ilijenga kituo cha muda cha operesheni kwenye vijiji vya Lodha na Aar, ambavyo ni vitovu vya mji wa Djugu ili kuzuia ghasia miongoni mwa wanajamii na vile vile kulinda raia.
Ujumbe huo pia umeimarisha doria zake huko Djaiba, ikiwemo kwenye eneo linalohifadhi wakimbizi wa ndani kwa lengo la kuzuia mashambulizi zaidi na kujaribu kuwapatia hakikisho la usalama kwani raia wamekumbwa na kiwewe.
Bi. Keita pia ametoa wito kwa kila mtu mwenye kuwajibika na anayejali ubinadamu akomeshe wimbi hili la sasa la ghasia.