Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Mashambulizi yakishamiri, sinfohamu yakumba wakimbizi

Kambi ya ugani UNHCR huko Lushagala, Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hutoa makazi ya muda kwa watu waliokimbia makazi yao ya ndani.
© UNHCR/Guerchom Ndebo Makazi ya wakimbizi wa ndani ya Lushagala Kivu Kaskazini nchini DRC. (Maktaba)

DRC: Mashambulizi yakishamiri, sinfohamu yakumba wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, lina wasiwasi mkubwa kuhusu janga la kibinadamu linalozidi kuwa baya tena kwa kasi kubwa huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kwani kushindwa kufikia wahitaji kumekwamisha ufikishaji misaada ya haraka inahoyitajika.

Mashambulizi ya mabomu mazito yameharibu makazi ya muda 70, 000 ya wakazi karibu na mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini na Minova, jimboni Kivu Kusini na kuwaacha takribani watu 350,000 waliokimbia makazi yao bila mahali pa kujihifadhi, amesema  Eujin Byun, msemaji wa UNHCR akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo.

Ametoa kauli hiyo wakati tayari saa 72 zilizotolewa na waasi wa M23 kwa wakimbizi Goma wawe wameondoka na kurejea kwenye makazi yao halisi zikiwa zimeshapita.

Hivi sasa mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao sasa  wanaishi katika maeneo kama vile makanisa, shule, na hospitali, huku vitendo vya uhalifu na uporaji vikigubika waliokimbia Goma.

Watoto wanacheza mchezo unaohusisha ngome ya chuma katika eneo lenye miamba huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
United Nations Watoto wakusanyika Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Ingawa takriban wakimbizi 100,000 wamejaribu kurejea katika maeneo yao ya nyumbani, ambako nyumba zao zimeharibiwa na hakuna huduma muhimu au ni chache, wengi wao wameendelea kusalia katika vituo vya pamoja.

Uharibifu wa miundombinu umeripotiwa Kivu Kaskazini ikiwa ni pamoja na chumba cha kuhifadhi maiti,  huku msongamano mkubwa hospitalini ukiongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, yakiwemo kipindupindu, malaria, na surua.

Bi.  Byun amesema UNHCR imeendelea kutoa misaada kwa wakimbizi Kivu Kaskazini na Kivu Kusini kwa kadri iwezavyo wakati huu ambapo, watendaji wa UNHCR, wameona familia zikiwa kwenye sintofahamu ya kurejea makwao wasiko na uhakika au kusalia waliko.

Amesema, “miongoni mwao ni mama mjane wa miaka 55 mwenye watoto watano, ambaye amepoteza kila kitu alipokimbia kijiji chake kutafuta usalama huko Goma. Sasa, amelazimika kuondoka kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo kandokando ya jiji, bila kufahamu aende wapi. Wakazi wa Bukavu, jiji lenye watu milioni 1.3, Kivu Kusini, wamekuwa katika hali ya tahadhari kubwa huku usalama ukizidi kuzorota, jambo ambalo limewalazimu wengi wao kukimbilia kusini au maeneo ya mbali zaidi.”

UNHCR imesema inatarajia watu wengi zaidi kukimbilia mijini siku zijazo kutokana na waasi wa M23 kusonga Bukavu, hali inayoweza kufuatiwa na wimbi kubwa la uhamaji zaidi.

UNHCR inatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja ili kuhakikisha usalama wa raia, wakiwemo waliokimbia makazi yao, na kuheshimu kanuni za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya kusafiri kwa uhuru kutafuta usalama.

Muonekano wa nje wa kambi ya wakimbizi ya Kanyaruchinya huko Goma, DRC, unaonyesha watu wakitembea katikati ya mahema UNHCR .
UN News Mwonekano wa nje wa kambi ya wakimbizi ya Kanyaruchinya iliyoko Goma nchini DRC.

Hofu ya usalama yalazimu wagonjwa wa mpox kutoroka vituo vya matibabu

Wakati huo huo, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, Christian Lindmeier, amezungumzia jinsi machafuko yanavyokwamisha juhudi za kukabili ugonjwa wa homa ya nyani au mpox mjini Goma na viunga vyake kwani mapigano yanaelekea kusini mwa mji huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Geneva, Uswisi, amesema ni lazima ikumbukwe kuwa DRC ndio nchi iliyoathiriwa vibaya zaidi na mpox, huku majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yakiwa ndio kinara wa maambukizi ya virusi vya mpox aina ya clade 1b.

Amesema kutokana na kasi kubwa ya kusambaa kwa aina hiyo ya virusi, mwezi Agosti mwaka jana, WHO ilirejelea tena kutangaza mpox kuwa tishio la afya ya umma duniani, ikiwa ni mara pili kutangazwa baada yam waka 2022.

Mapema mwezi juu, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus alitangaza kutulia kwa maambukizi ya mpox nchini DRC lakini mapigano ya sasa na kuhamahama kumelazimu wagonjwa kukimbia vituo vya matibabu, na hivyo kuongeza hatari ya maambukizi.

Mtaalamu wa matibabu aliyevaa scrubs za bluu na glavu akiwa ameshika bomba la majaribio huku mgonjwa wa kiume, Bashibara, akimtazama wakati wa matibabu ya mpox katika Hospitali ya Kavumu huko Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WHO/Guerchom Ndebo Mwanamume mmoja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo apeana damu yake kama sehemu ya matibabu yake ya ugonjwa wa mpox.

Wagonjwa wa mpox wamekimbia vituo vya tiba kwa hofu ya usalama

Kati ya wagonjwa 143 waliothibitishwa kuugua mpox walioko kwenye eneo tengwa mjini Goma na viunga vyake, 128 wamekimbia kwa hofu ya usalama wao,” amesema Bwana Lindmeier, akisisitiza kuwa “ni wagonjwa 15 tu wamesalia kwenye vituo vya matibabu. Hii bila shaka ni hatari kwa kila mtu.”

Ameongeza kuwa baadhi ya vituo vya afya vimeporwa, wahudumu wa afya wamekimbia, na watu hawawezi kupata huduma za afya kwa sababu ya hali tete ya usalama.