Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: M23 wakiwa wanasogelea Bukavu, Lemarquis atahadharisha kuhusu hali ya kibinadamu

Eneo la kuhama kwa Don Bosco Ngangi, karibu na Goma, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo, tarehe 4 Februari 2025. Eneo hilo limejaa vifusi na uchafu baada ya kuondolewa na kuharibiwa na mapigano ya hivi karibuni.
© UNICEF/Jospin Benekire Kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma imesalia tupu kufuatia mapigano makali ya hivi majuzi katika jiji hilo.

DRC: M23 wakiwa wanasogelea Bukavu, Lemarquis atahadharisha kuhusu hali ya kibinadamu

Amani na Usalama

Kadri waasi wa M23 wanavyoendelea kupata mafanikio katika jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia misaada ya kibinadamu ameonya kuhusu kuongezeka kwa changamoto na mahitaji katika eneo hilo, ambapo zaidi ya watu milioni moja walikuwa tayari wamepoteza makazi yao hata kabla ya mgogoro wa sasa.

“Mstari wa mbele unazidi kusogea karibu na Uwanja wa Ndege wa Kavumu,” Bruno Lemarquis ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa (UN News) jana Jumatano kupitia mahojiano ya video.

Baada ya kuanguka kwa Goma, mji mkuu wa Kivu Kusini, mwishoni mwa Januari mwaka huu 2025, kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda sasa linapiga hatua dhidi ya jeshi la Congo kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini.

“Kalehe, ambao ni mji mkubwa katika jimbo hili, umeanguka leo mchana,” Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu aliripoti.

Mji huo uliotekwa uko umbali wa maili 20 tu kutoka Kavumu, ambao unahifadhi uwanja mkuu wa ndege wa jimbo hilo.

Kutokana na hali hiyo, uwanja wa ndege wa kibiashara, ulioko umbali wa maili 20 kutoka Bukavu, sasa unatumiwa zaidi kwa operesheni za kijeshi za serikali ya Kinshasa, ambayo inakabiliana na mashambulizi ya waasi.

“Hadi hivi karibuni, huu ulikuwa hii ndio ilikuwa njia yetu kuu kupeleka wafanyakazi Kivu Kusini,” alisema. 

Lakini kama ilivyo kwa uwanja wa ndege wa Goma, ambao bado haujarejea kwenye shughuli zake, sasa njia hiyo imefungwa.

Bruno le Marquis, Mwakilishi UN , akizungumza na waandishi wa habari katika kambi ya Bulengo huko Goma, DRC.
UN News/Byobe Malenga Bruno le Marquis, mwakilishi wa katibu mkuu na mratibu wa UNOCHA nchini DRC akizungumza mbele ya waandishi kambini bulengo.

Hali Mbaya ya Kibinadamu 

Kabla ya mashambulizi ya hivi karibuni ya M23 mwanzoni mwa mwaka huu, Lemarquis alikumbusha kuwa hali ya kibinadamu Kivu Kusini ilikuwa tayari mbaya.

Takribani watu milioni 1.65, sawa na zaidi ya asilimia 20 ya wakazi wa jimbo hilo, walikuwa wamepoteza makazi kwa sababu mbalimbali.

“Kuna migogoro mingine jimboni, mvutano wa kijamii, na migogoro ya ardhi,” alieleza.

Kivu Kusini pia inaathiriwa na majanga ya asili, yakiwemo maporomoko ya ardhi kando ya Ziwa Kivu, ambayo yamesababisha watu wengi kuhama makazi yao.

“Hivyo, tulikuwa tayari na operesheni kubwa ya kibinadamu inayoendelea Kivu Kusini,” anasema Lemarquis.

Mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wa M23, ambao wameingia Kivu Kusini kwa mara ya kwanza tangu Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) ulipoondoka jimboni humo mwezi Juni 2024, yanazidisha hali kuwa mbaya zaidi.

“Hili litazidisha changamoto na mahitaji,” alisema Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu.

Mwanamke anayebeba mtoto mgongoni mwake na kifurushi kikubwa anatembea barabarani karibu na Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati pikipiki inapopita.
© WFP/Moses Sawasawa Tarehe 26 Januari 2025, mama mkimbizi akiwa amembeba mwanae pamoja na virago vyake akikimbia kutoka kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako waasi wa M23 wametwaa maeneo ya mji huo huku wakipambana na jeshi la serikali, FARDC.

Takribani watu 170,000 wameyahama makazi yao

Lemarquis anakadiria kuwa mapigano ya hivi karibuni yamesababisha watu wapya takribani 170,000 kuhama makazi yao, idadi ambayo haijumuishi makadirio ya wiki mbili zilizopita.

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu pia alibainisha kuwa watu wengi wanakimbilia mji mkuu wa jimbo hilo, ambapo tayari kuna wakazi takribani milioni 1.3.

“Kulingana na jinsi hali itakavyoendelea, katika siku zijazo, tunaweza kuona idadi kubwa ya watu wanaokimbilia Bukavu, kisha kutoka nje ya mji, kuelekea Kusini,” alieleza.

Kiongozi huyo anaeleza kwamba hali hiyo, inaweza kuzuia watu walio hatarini kupata huduma za afya na kijamii.

Hatari ya milipuko ya magonjwa

Katika muktadha huu, Lemarquis analeza wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kutokana na mapigano yanayoendelea Kivu Kusini, jimbo ambalo lina maambukizi mengi ya kipindupindu.

“Huduma muhimu zinapoathirika, hii inaweza kusababisha milipuko ya magonjwa,” anaonya.

Hili ni jambo la kutia hofu zaidi, aliongeza, kwa sababu jimbo hilo kwa sasa ndilo kitovu cha mlipuko mpya wa ugonjwa wa mpox, unaojulikana kama clade Ib, ambao umekuwa ukienea sana katika mji wa Kalehe, ambao sasa uko chini ya udhibiti wa M23.

Wafanyakazi wa WFP na watu wa kujitolea wasambaza msaada wa chakula kwa watu waliokimbia makazi yao nchini DRC.
WFP Wanawake mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini wakibeba chakula kilichowasilishwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake.

Hakuna njia za kibinadamu kuelekea kusini

Kwa upande mzuri, Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu anasema barabara kutoka Goma hadi Minova, mji wa kwanza wa Kivu Kusini uliotekwa na M23 katikati ya Januari, sasa imefunguliwa tena.

“Kulikuwa na siku chache ngumu kwa wenzetu wa kibinadamu kwa sababu ya mapigano,” anakiri na kuongeza “lakini sasa ufikiaji umeimarika.” 

Hata hivyo, kusini mwa jimbo hilo, njia za misaada ya kibinadamu bado zimekatwa.

“Kwa muda mrefu, barabara kati ya Goma na Bukavu hajaweza kupitika bado,” alisema.

Njia mbadala, ikiwemo kupitia Ziwa Kivu, ambalo linapakana na jimbo hilo na linaunganisha Goma Kaskazini na Bukavu Kusini, pia zimekatwa. 

“Njia mbadala si nyingi, na uwanja wa ndege ndio njia kuu ya upatikanaji,” alikiri.

Hata hivyo, Mratibu huy wa Misaada ya Kibinadamu ataja uwezekano wa kupeleka misaada kupitia nchi jirani ya Rwanda, ingawa alisema kuwa hiyo si suluhisho rahisi.

“Hii ni hali tete,” anasisitiza Lemarquis.