Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Mashariki mwa DRC wakabiliwa na unyanyasaji wa kingono, utekaji na kuajiriwa vitani: UNICEF

Jean-Marie Hakizimana akimshika mkono mwanawe wa miaka 6, Pascal, nje ya jengo la muda katika Hospitali ya Kanyaruchinya huko Goma, DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire Baba akimpeleka mwanawe aliyejeruhiwa kwa matibabu katika hospitali karibu na Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Watoto Mashariki mwa DRC wakabiliwa na unyanyasaji wa kingono, utekaji na kuajiriwa vitani: UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa vurugu katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambako watoto wanazidi kukabiliwa na unyanyasaji wa kingono, utekaji nyara, na kuajiriwa na makundi yenye silaha.

Katika taarifa iliyotolewa mjini Kinshasa Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesisitiza kuhusu hali mbaya katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, akibainisha kuwa kiwango cha ukatili dhidi ya watoto kimefurutu ada.

Kulingana na UNICEF, wiki ya Januari 27 hadi Februari 2 mwaka huu, ilishuhudia ongezeko la mara tano la visa vya ubakaji vilivyotibiwa katika vituo 42 vya afya katika eneo hilo, ambapo asilimia 30 ya waathiriwa walikuwa watoto.

Shirika hilo  limesema linahofia kuwa idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na kutoripotiwa kwa visa vingi.

Limesisitiza kuwa kuongezeka kwa visa hivi kumeacha vituo vya afya vikihaha kutoa huduma muhimu baada ya unyanyasaji, ikiwemo dawa za kuzuia maambukizi ya VVU.

Darasa tupu lenye madawati ya mbao na ubao mweusi katika Shule ya Msingi ya Bulengo katika eneo la wakimbizi karibu na Goma, DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire Darasa katika shule ya msingi inayoungwa mkono na UNICEF katika kambi ya watu waliokimbia makazi karibu na Goma mashariki mwa DR Congo imesalia tupu.

Simulizi za kutisha za waathirika

Kwa mujibu wa UNICEF hadithi za kusikitisha kutoka waathirika zinaonyesha ukubwa wa ukatili huu.

Bi. Russel amesema “Mama mmoja amewasimulia wafanyakazi wa UNICEF jinsi binti zake sita, mdogo akiwa na umri wa miaka 12 tu, walivyobakwa na wanaume wenye silaha walipokuwa wakitafuta chakula.”

Amesema hadithi kama hizi zinaonyesha vitisho visivyokwisha vinavyowakabili watoto na familia zao katikati ya mashambulizi na kufurushwa mara kwa mara katika eneo hilo.

Shirika hilo la watoto limeonya kwamba “Migogoro hiyo imesababisha maelfu ya watoto kuhama makazi yao, wengi wao wakitenganishwa na familia zao, na kuwaweka katika hatari kubwa ya unyanyaswaji  na ukatili”

Shirika hilo limeongeza kuwa “Katika wiki mbili zilizopita pekee, zaidi ya watoto 1,100 wasio na walezi wamebainika katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, na idadi ikiendelea kuongezeka.”

UNICEF inafanya kila liwezekanalo kusaidia

UNICEF imesema inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma za haraka za matibabu na ushauri nasaha wa kisaikolojia, huku pia wakiwekwa katika familia za malezi ya muda.

Taarifa ya UNICEF pia imeonyesha kuongezeka kwa ajira ya watoto na makundi yenye silaha, huku watoto wadogo wenye umri wa miaka 12 wakilazimishwa kujiunga na kupigana.

Shirika hilo limezitaka pande zote zinazohusika katika migogoro kukomesha ukiukaji wa haki dhidi ya watoto, kuhakikisha ulinzi wa raia, na kuruhusu mashirika ya misaada kufikia bila vikwazo watoto na familia zilizoathirika.

UNICEF pia imetoa wito wa juhudi za kidiplomasia kuimarishwa ili kukomesha vurugu na kuhakikisha mustakabali wa amani kwa watoto wa DRC.