DRC: Doria za pamoja za MONUSCO na FARDC huko Ituri zaimarisha usalama
DRC: Doria za pamoja za MONUSCO na FARDC huko Ituri zaimarisha usalama
Katika kitongoji cha Komanda jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, doria za pamoja zinazoendeshwa na walinda amani wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO na jeshi la serikali FARDC zimeimarisha usalama kwenye maeneo ya raia.
Video ya MONUSCO iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa X, zamani Twitter inamwonesha Noe Temwembi, Chifu wa eneo la Walese-Vokuntu akisema;
“Kwa wananchi, doria hizo za pamoja zina faida sana kwa kuwa zinasambaratisha vikundi vya adui. Mfano katika msitu wa Monhoyo, MONUSCO kwa pamoja na FARDC walifurumusha waasi wa kikundi cha ADF-Nalu. Na hilo lilikuwa jambo kubwa kwa wanajamii..”
Kando ya mashambulio kutoka makundi ya waasi, MONUSCO pia inasaidia kuleta maelewano baina ya jamii, kama anavyoendelea Chifu Temwembi.
“Kunapokuwa hakuna maelewano baina ya jamii, MONUSCO inaingilia kati haraka sana ili kujaribu kuzileta pande kinzani kwenye meza moja. Mathalani kulikuweko na mvutano kati ya watu kabila la walese walipokuwa wanazozana na watu wa kabila la wanande, tuliwasilisha ombi kwa ofisi ya MONUSCO ya masuala ya raia, ambao waliaandaa mazungumzo baina ya wanajamii. Na kutokana na mazungumzo hayo walitamatisha kwa makubaliano. Na tunavyozungumza sasa walese na wanande wanaishi pamoja kwa amani, hakuna tena mvutano kama awali.”
Kwa sasa MONUSCO imesalia katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini kwani katika maeneo mengine ilifungasha virago kwa ombi la serikali ya DRC, ombi ambalo liliridhiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
MONUSCO inatarajiwa kuondoka kabisa DRC ifikapo tarehe 31 mwezi Desemba mwaka huu, kwa mujibu wa Azimio la Baraza la Usalama.