Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukweli kuhusu dhana nne potofu kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni

Watoto wakijifunza kwa kutumia kompyuta ndogo au tablet katika Shule ya Umma ya Melen ya Yaoundé, Kamerun.
© UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakijifunza kwa kutumia kompyuta ndogo au tablet katika Shule ya Umma ya Melen ya Yaoundé, Kamerun.

Ukweli kuhusu dhana nne potofu kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Maisha ya watoto na vijana kwa muda mrefu yameunganishwa na intaneti na mitandao ya kijamii na kadri teknolojia inavyoendelea kubadilika kwa kasi jambo hili linaongezeka na kuenea zaidi na kuruhusu watoto kufikia ulimwengu wa habari, kujifunza, kushirikiana, burudani na zaidi inaweza kuwa chanya lakini wakati mwingine kuna hatari, linaeleza shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF katika makala hii iliyochapishwa kwenye wavuti wa shirika hilo leo Siku ya Kimataifa ya intaneti salama.

UNICEF inaeleza kuwa miaka ya hivi karibuni, kuna dhana potofu nyingi ambazo zimeenea kuhusu athari za teknolojia za kidijitali kwenye maisha ya watoto, na kuwapotosha wazazi, walezi, waelimishaji na watunga sera. "Hivyo basi, mwaka huu tunapoadhimisha Siku ya Mtandao Salama, hebu tuangalie – na tupinge – baadhi ya dana hizi nne potofu."
 

Dhana potofu #1: Kuwapa watoto wengi upatikanaji mkubwa wa intaneti kunaweza tu kuwawezesha na kunufaisha wao na jamii zao.

UNICEF imesema  wakati watoto wananufaika kwa kutumia muda wao mtandaoni, na wakati usawa katika ufikiaji ni lengo la msingi, sio kwamba ufikiaji mkubwa huja tu na faida kubwa zaidi. Kwa kweli, nchi ambazo ufikiaji wa mtandao ni wa juu mara nyingi hushuhudia watoto watoto wakiwa hatarini kukumbana na ujumbe wa chuki na picha za vurugu mtandaoni.

Ingawa hivyo, intaneti inaweza kuchochea muunganisho wa kijamii, ushiriki na ubunifu kwa watoto, lakini kwa kuwa mazingira yao ya kidijitali bado hayadhibitiwi, na mara chache hayabuniwi kwa kuzingatia maslahi yao bora, pia hurahisisha kuenea kwa maudhui hatari kama vile ujumbe wa chuki na picha za kutatanisha. Serikali zinapaswa kutunga será thabiti ili wahusika walazimike kujumuisha uzingatiaji wa haki za watoto, ikijumuisha tathmini thabiti za athari, katika mchakato wa kudhibiti chuki na vurugu mtandaoni. Hatua zaidi za serikali kuchukua zimeainishwa katika muhtasari huu wa sera wa UNICEF .

Dhana potofu #2: Kucheza michezo ya video ni mbaya kwa maendeleo na ustawi wa watoto.

Michezo ya video imekuwa maarufu tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980, na kwa hivyo kuna mjadala mkali kuhusu uwezo wa michezo hiyo wa kuwadhuru watoto wanaoicheza. Lakini, kwa kweli, michezo ya video inaweza kuchangia na kusaidia ustawi wa watoto - lakini lazima iundwe kwa kuzingatia mahitaji ya watoto na umri wao. Michezo ya kidijitali huongeza uwezo wao wa kuelewa na kudhibiti hisia, na kuunda na kudhibiti mahusiano. Kwa hivyo, wabunifu wanahitaji kuelewa jinsi uzoefu mzuri wa uchezaji unavyoweza kuonekana kwa watoto tofauti, na ni chaguo gani za muundo au njia ambazo zinaweza kuwaunga mkono.

Dhana potofu #3: Vurugu za mtandaoni ni tofauti kabisa na aina nyingine za vurugu.

UNICEF inasema utafiti umeonesha kwamba matukio ya watoto ya unyanyasaji katika anga za dijitali mara nyingi yanahusishwa na vurugu katika miktadha mingine. Kwa mfano, kwa watoto wengi, unyanyasaji mtandaoni ni mwendelezo wa unyanyasaji ambao tayari wanapata nyumbani, shuleni au katika mitaa yao.

Imeongeza kwamba, baadhi ya watoto huulizwa au kulazimishwa wakati fulani na mkosaji mmoja kueneza  picha za ngono zinazozalishwa kibinafsi mtandaoni, ana kwa ana au katika nafasi zote mbili. Wahalifu pia hutumia mitandao ya kijamii au ujumbe wa papo hapo kuwasukuma watoto kukutana nao ana kwa ana, kuwezesha vurugu au unyanyasaji wa kingono, jambo ambalo lazima likomeshwe na kuwa na será za kulazimisha wamiliki wa mitandao za kijamii kuzuia athari hizo kwa watoto.

Dhana potofu #4: Hatari kutoka kwa wageni: Unyanyasaji wa kingono wa watoto mtandaoni hufanywa zaidi na watu wageni kwa mtoto

Aina nyingi za unyanyasaji wa kingono kwa watoto mtandaoni mara nyingi hufanywa na mtu ambaye mtoto tayari anamjua, anaweza kuwa rafiki, mtu anayefahamiana naye, mwanafamilia au mshirika wa kimapenzi. Wageni ndio wahalifu wa kawaida, na kupendekeza kuwa uzuiaji wa ujumbe na njia za elimu, pamoja na majibu, zitakuwa na ufanisi zaidi ikiwa zitadhibitiwa na serikali.

UNICEF imesisitiza kuwa ni lazima tuwape walezi, viongozi wa jamii, waelimishaji na wataalamu wengine taarifa za kisasa na usaidizi wa kuzuia unyanyasaji wa kingono kwa watoto katika intaneti. Hili litasaidia kuondoa dhana potofu za kawaida kuhusu unyanyasaji wa kingono, ikiwa ni pamoja na wahusika wa unyanyasaji, na kuunda mifumo ya usaidizi ambayo watoto wanaweza kutegemea na kuamini .

Shirika hilo limetamatisha likisema kwamba teknolojia ya kidijitalii ni sehemu kubwa inayounda maisha ya watoto, yenye uwezo wa kutoa fursa nyingi za kujifunza, mwingiliano wa kijamii, na ujumuishwaji, lakini, watoto wanapopitia ulimwengu huu wa kidijitali, pia wanakabiliwa na hatari kubwa kwa ustawi wao, uhuru na usalama wao.

Pata maelezo zaidi kuhusu utafiti wa UNICEF uitwayo Innocenti kuhusu watoto na teknolojia ya kidijitali hapa