Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muhtasari wa habari: DRC, Gaza na AI

Mwanamume akibeba maji katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
UN News
Mwanamume akibeba maji katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Muhtasari wa habari: DRC, Gaza na AI

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa na wadau wanasalia na wasiwasi mkubwa kufuatia amri iliyotolewa Jumatatu na waasi wa M23 huko jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ya kupatia wakimbizi wa ndani saa 72 wameondoka kwenye kambi mjini Goma na viunga vyake, na kurejea vijijini mwao.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA Jens Laerke amesema kitendo chochote cha kurejea vijijini kinapaswa kuwa cha hiari na kifanyike kwa usalama na mazingira ya kiutu kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu

Gaza

Na sasa Ukanda wa Gaza ambako Rolando Gomez, Mkuu wa Mawasiliano kwenye Ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva Uswisi, amezungumza na waandishi wa habari akimnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akisema lazima kuepusha gharama zozote zinazoweza kuibuka iwapo uhasama utaanza upya Gaza kwani italeta janga kubwa. Amesema “natoa wito kwa Hamas kuendelea na mpango wa kuachilia huru mateka Jumamosi ijayo na pande zote lazima zizingatie ahadi zao kwenye makubaliano ya sitisho la mapigano na zirejee kwenye awamu ya pili ya mashauriano ya Doha.”

Paris

Na akihutubia viongozi huko Paris Ufaransa kwenye mkutano wa Kuchukua Hatua kwa Akili Mnemba ili inufaishe wote, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza udharura kwa dunia kuwa tayari kukabiliana na changamoto zitokanazo na teknolojia hiyo iliyo mikononi mwa wachache licha ya kuleta mapinduzi kwenye sekta lukuki kama vile elimu, afya, na kilimo. Amehoji nani anaaamua changamoto zipi AI itatue na zipi isitatue; nani ananufaika na miundo hiyo; nani anabeba gharama za makosa ya AI? Ni maswali yanayoathiri kila mtu, hivyo na majawabu lazima yahusishe kila mtu.