Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nini kifanyike Akili Mnemba inufaishe kila mtu?

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika Mkutano wa Utekelezaji wa Akili Mnemba au AI huko Paris, Ufaransa.
United Nations/Marie Etchegoyen
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika Mkutano wa Utekelezaji wa Akili Mnemba au AI huko Paris, Ufaransa.

Nini kifanyike Akili Mnemba inufaishe kila mtu?

Masuala ya UM

Mabibi na mabwana, hebu twende moja kwa moja kwenye suala hili. Mkutano huu una swali la msingi kuhusu uhusiano wetu na Akili Mnemba: Tuko tayari kwa zama zijazo? Jibu ni rahisi. Hapana!

Ndivyo alivyoanza hotuba yake ya kurasa nne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres mbele ya viongozi wa nchi na wa taasisi za kiserikali na kimataifa mjini Paris, Ufaransa kuhusu Hatua kwa Akili Mnemba au AI.

Guterres amesema inawezekana hatuko tayari hata kwa sasa, kwani kwa kile kinachoonekana katika fumba fumbua  AI imehama kutoka jambo la kutunga la kisayansi hadi kuwa nguvu thabiti inayobadilisha dunia yetu.

Katibu Mkuu amesema AI sasa inaumba upya jinsi watu wanavyoishi, wanavyofanya kazi na wanavyotangamana.

“Inachochea mambo makubwa kwenye elimu, sayansi, kilimo… lakini vile vile inaleta mtihani mkubwa katika maadili yetu ya pamoja,”  amesema Guterres katika mkutano huo ulioandaliwa kwa pamoja na serikali ya Ufaransa na India.

Roboti aitwaye Ameca alishiriki Mkutano wa viongozi kuhusu Akili Mnemba kwa Matumizi Bora  uliofanyika Geneva, USwisi Julai 2023.
UN Photo/Elma Okic
Roboti aitwaye Ameca alishiriki Mkutano wa viongozi kuhusu Akili Mnemba kwa Matumizi Bora uliofanyika Geneva, USwisi Julai 2023.

AI inashikiliwa na wachache

Amezungumzia vile ambavyo AI iko mikononi mwa wachache akisema wakati baadhi ya kampuni na nchi chache zinasonga mbele kwa kasi kubwa kwenye uwekezaji, nchi nyingi zinazoendelea zinajikuja zimeachwa nyuma.

“Hii ni hatari inaweza kuhatarisha mgawanyiko mkubwa zaidi wa kijiografia,” ameonya Guterres akisema lazima tuepusha dunia ya walio na AI na wasio na AI.

AI izibe pengo badala ya kulizidisha

Hivyo amesema ni vema AI itumike kama daraja la kuziba pengo kati ya nchi tajiri na masikini badala ya kuendelea kuongeza pengo hilo.Ni lazima ichochee maendeleo endelevu, badala ya kuchochea ukosefu wa usawa.

Amesema Umoja wa Mataifa tayari umeweka wazi jukwaa jumuishi, wazi na fanisi kwa ajili ya mshikamano kwenye AI na jukwaa hilo si kitu kingine bali ni Mkataba wa Kimataifa wa Kidijitali uliopitishwa mwaka 2024 wakati wa Mkutano wa Zama Zijazo.

Mkataba huo ni makubaliano ya kwanza ya kimataifa ya usimamizi wa AI ambapo dira ni moja teknolojia inayohudumia binadamu na si kinyume chake.

Katibu Mkuu amesema kuundwa kwa Jopo Huru la Wataalamu wa Kisayansi kuhusu AI kutakuwa msingi wa kutafsiri dira hiyo kuwa vitendo.

Amesihi kila mtu kuunga mkono kuanzishwa kwa jopo hilo bila kuchelewa.

Amekumbusha kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walikubaliana kuanzisha Mazungumzo ya Kimataifa kuhusu Usimamizi wa AI, ndani ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha kila nchi ina fursa ya kupaza sauti kuhusu mustakabali wa AI.

Guterres amesema ni matumaini yake kuwa mkutano huu utaimarisha mazungumzo hayo.

Nchi zinazoendelea zisisalie kuwa watumiaji pekee wa AI

Amezungumzia pia jinsi Mkataba wa Kimataifa kuhudu Dijitali unavyotaka kujengea uwezo nchi zinazoendelea zisiishie tu kwenye kutumia AI bali ziwe sehemu ya mapinduzi ya teknolojia hiyo.

“Kuanzisha mtandao wa kimataifa wa kujengea uwezo, kama ilivyopendekezwa na Jopo la Ngazi ya Juu la Ushauri Kuhusu AI, ni hitaji la kiuchumi na suala bora kimaadili,” amesema KAtibu Mkuu.

Hivyo amesema kitendo cha kuzinduliwa hii leo kwa Mfuko wa AI kwa Maslahi ya Umma, ni mchango muhimu.

“Punde nitawasilisha ripotiyangu kuhusu mifumo bunifu ya uchangiaji hiari na mipango ya kujengeana uwezo ili kusaidia nchi zote kunufaia na AI.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akutana na Alain Beurset, Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya katika Mkutano wa Utekelezaji wa AI huko Paris, Ufaransa.
United Nations/Marie Etchegoyen
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akutana na Alain Beurset, Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya katika Mkutano wa Utekelezaji wa AI huko Paris, Ufaransa.

AI na tabianchi

Hakusahau AI na hatua kwa tabianchi akisema, sote tunafahamu kuwa AI inaweza kuwa na mchango mkubwa katika mazingira na nishati fanisi. Lakini tunafahamu pia kuwa mifumo ya AI inayotumia kiwango kikubwa cha nishati tayari inaelemea sayari yetu ambayo tayari imezidiwa uwezo.

Hivyo amesema ni muhimu kuweka mifumo na miundombinu ambayo inatumia nishati kidogo na kwa ufanisi.

Ametamatisha kwa kusema kuwa kila nchi ishiriki kwenye mchakato wa matumizi ya AI kwani nani anaaamua changamoto zipi AI itatue na zipi isitatue; nani ananufaika na miundo hiyo; nani anabeba gharama za makosa ya AI? Ni maswali yanayoathiri kila mtu.

“Hivyo ni wajibu wa kila kiongozi wa serikali, teknolojia kuahidi kuweka miongozo, kubadilishana mifano bora na kuweka sera zenye uwiano,” amesema Guterres.