Tom Fletcher: Wapalestina wahitaji ufadhili na mshikamano wa kimataifa
Tom Fletcher: Wapalestina wahitaji ufadhili na mshikamano wa kimataifa
Huko Mashariki ya Kati Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA Tom Fletcher alifanya ziara ya siku tatu huko Ukingo wa Magharibi na Gaza ili kujionea hali halisi ya raia.
Taswira ya kutoka mbali ya mji wa Yerusalemu Mashariki ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ni kwenye eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli.
Kwa mbali utaona majengo yaliyosimama, lakini kamera inatusogeza karibu kabisa na kushuhudia uharibifu wa majengo. Makombora ya jeshi la Israeli yamesambaratisha makazi ya watu, ikiwemo nyumba Fakhri Abu Thiyab. Akisimulia akiwa kwenye eneo la nyumba yake iliyobomolewa anasema..
“Hii ni nyumba yangu. Hii ni nyumba ambamo nilizaliwa. Kabla ya mwaka 1967 ilikuwa ndogo. Nimeishi, nimeoa na nikapata watoto. Kumbukumbu za mama yangu zimo humu. Lakini Manispaa imebomoa nyumba yangu tarehe 14 mwezi Februari mwaka 2024. Baada ya kuikarabati, kwa kuwa sikuweza kuishi mtaani, au kununua nyingine au kujenga nyumba nje ya eneo hili, ilibomolewa tena tarehe 5 mwezi Novemba mwaka 2024.”
Kilichosalia sasa ni vifusi na nondo. Ukichunguza zaidi kwenye video hii ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, unaona vifaa kama vile baiskeli ya mtoto, mabaki ya feni na masponji ya viti vya kukalia. Bwana Thiyab anaendelea.
“Tulikuwa watu 10 tunaishi ndani ya nyumba hii: mimi mwenyewe, watoto wangu na wajukuu zangu. Baada ya kubomolewa, watoto wangu walihama. Mimi na mke wangu tulibakia kwenye nyumba inayovutwa na gari. Hata yenyewe tunaishi na vitisho. Nadhani manispaa ina nia ya kuvunja kabisa kitongoji hiki. Ina mpango wa kukibadilisha, kujenga makazi ya walowezi na kutufukuza.”
Video inamuonesha Thiyab akitoka ndani ya nyumba hiyo inayovutwa kwa gari na anarejea kwenye eneo nyumba yao ilikobomolewa.
“Nilizaliwa hapa na nikaishi hapa wakati wa utoto wangu. Kwa hiyo sasa tumekuwa hatuna tena historia yetu, hatuna kumbukumbu na hata hatuna mustakabali na hii ni kwa sabbau ya sera ya Israeli isiyokuwa halali.”
Thiyab akaungana na ujumbe wa Umoja wa Mataifa ukiongozwa na Mkuu wa OCHA Tom Fletcher uliofika hapa kujionea hali halisi ya uharibifu wa makazi ya watu, na pia kutathmini mahitaji ya raia.
Baada ya kuzungumza na wakazi wa hapa, Bwana Fletcher akafunguka.
“Kwa hiyo hii ndio hali halisi ya familia nyingi za wakazi wa Yerusalemu Mashariki. Nimekuwa nikisikia simulizi kutoka kwa wamiliki wa hii nyumba, nyumba ambamo ndimo amekulia. Nyumba ambamo alikuzia watoto na wajukuu zake. Nyumba imetoweka ndani ya nusu saa. Kumbukumbu zote zimefukiwa kwenye kifusi hiki. Hata hivyo wamenijulisha kuwa hawataondoka, watabakia hapa hapa. Wanaweza kuwa wamepoteza mali zao, lakini hawatokata tamaa juu ya utu wao na matumaini yao.”
Kutoka hapa Yerusalemu Mashariki, Bwana Fletcher alikwenda Gaza, ambako nako aliona kiwango cha juu cha uharibinu na machungu yasiyoelezeka.
Ingawa hivyo kutokana na sitisho la mapigano wahudumu wa kibinadamu wameweza kufikishia wahitaji misaada ya kuokoa maisha kama vile chakula, maji, mahema, dawa. Amesisitiza umuhimu wa OCHA kuendelea kuwezeshwa ili iweze kusaidia wahitaji Gaza.