Afrika ikigeuza changamoto kuwa fursa inaweza kuvuna dola trilioni 3.4- UNCTAD
Afrika ikigeuza changamoto kuwa fursa inaweza kuvuna dola trilioni 3.4- UNCTAD
- Afrika inaweza kutumia biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda ili kugeuza changamoto za kiuchumi kuwa fursa .
- Afrika inaweza kuimarisha uchumi na kupunguza utegemezi wa masoko ya kimataifa yanayoyumba kwa kutumia Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), mageuzi ya kiuchumi, na mbinu bunifu za kifedha.
- Uwekezaji katika miundombinu, utofauti wa biashara, na biashara ndogo na za kati (SMEs) ndio msingi wa kufungua ukuaji na kusongesha maendeleo endelevu.
Ripoti ya mpya kuhusu Maendeleo ya Kiuchumi barani Afrika kwa mwaka 2024 iliyozinduliwa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD, imeeleza jinsi Afrika inaweza kuwa mhimili mkubwa wa biashara ya kimataifa na ukuaji wa uchumi duniani.
Ripoti imezinduliwa leo huko Geneva, USwisi na Katibu Mkuu wa UNCTAD, Rebeca Grynspan, pamoja na Waziri wa Biashara, Viwanda na Uendelezaji wa Biashara ndogo za n aza kati, SMEs wa Côte d'Ivoire, Souleymane Diarrassouba.
Mathalani ripoti inataja jinsi mageuzi madhubuti ya sera na uwekezaji wa kimkakati vinaweza kuimarisha ustahimilivu wa Afrika dhidi ya misukosuko ya kiuchumi duniani na kuanzisha fursa mpya za maendeleo.
“Afrika imekumbana na changamoto kubwa – kutoka masoko ya kimataifa yenye kuyumba na gharama kubwa za madeni hadi ukosefu wa miundombinu,” amesema Bi. Grynspan.
“Hata hivyo changamoto hizi zimeweza pia kuwa fursa ya kuunda upya mustakabali wa uchumi wa bara hili. Kupitia mageuzi madhubuti, uwekezaji, na utekelezaji kamili wa AfCFTA, Afrika imeweza kuwa na nguvu zaidi, ustahimilivu mkubwa, na ushindani wa hali ya juu.”
Jinsi ya kupunguza utegemezi kwa masoko yenye kuyumba, kupunguza gharama, kuimarisha SMEs
Ripoti inasema takribani nusu ya nchi za Afrika zimetegemea mafuta, gesi, au madini kwa angalau asilimia 60 ya mapato ya mauzo ya nje, hali ambayo imeziweka katika hatari ya kuyumba kwa bei. Kutofautisha bidhaa za kuuza nje na kukuza biashara ndani ya Afrika kunaweza kuleta mapato thabiti zaidi.
Upungufu wa miundombinu katika sekta ya usafiri, nishati, na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, TEHAMA umefanya biashara kuwa ghali kwa asilimia 50 zaidi ya wastani wa kimataifa, jambo ambalo limepunguza ushindani, hasa kwa mataifa yasiyo na bahari. Uwekezaji katika usafirishaji na teknolojia ya kidigitali unaonekana kuwa muhimu kwa ukuaji wa uchumi.
Biashara ndogo na za kati, SMEs, zimeweza kutoa asilimia 80 ya ajira barani Afrika lakini zimeendelea kukabiliwa na changamoto za miundombinu hafifu, kuyumba kwa sarafu, na upatikanaji mdogo wa fedha. Kupanua mikopo, zana za kudhibiti hatari, na minyororo ya usambazaji ya kikanda vitaweza kuongeza uthabiti wao.
Kufungua fursa za biashara ya kikanda
Ripoti inatanabaisha kuwa biashara ndani ya Afrika imeendelea kuwa moja ya fursa kubwa zaidi za bara hili, lakini imechangia tu asilimia 16 ya mauzo ya nje, huku biashara nyingi bado zikiwa nje ya bara.
Utekelezaji kamili wa AfCFTA umeweza kuunda soko la dola trilioni 3.4, lakini kufungua uwezo huu kunahitaji uwekezaji katika miundombinu kwa kupanua mitandao ya usafiri, nishati, na TEHAMA, kurahisisha sera na taratibu za biashara kama forodha, na kusaidia viwanda kupitia, kwa mfano, punguzo la kodi na mikopo ya riba nafuu ili kukuza uzalishaji wa viwanda na bidhaa za kikanda.
Hatua za kisera kwa mustakabali imara
Ripoti hii ya "Maendeleo ya Kiuchumi barani Afrika 2024" ya UNCTAD imeonesha mikakati muhimu ambayo imeweza kubadilisha changamoto kuwa fursa:
- Motisha kwa viwanda: Punguzo la kodi, kupunguza gharama za mtaji, na mikopo ya riba nafuu kwa kampuni zinayowekeza katika uzalishaji wa viwanda na masoko ya kikanda.
- Mifumo ya kudhibiti hatari: Kuanzisha mifumo ya kifedha ya kikanda na mifumo ya tahadhari ya mapema dhidi ya biashara, pamoja na kuunganisha rasilimali za umma na binafsi kwa mipango ya dharura na malipo ya bima.
- Mifumo ya kukabiliana na migogoro: Kuunda mifumo ya kifedha ya biashara kusaidia biashara zilizoathirika na misukosuko ya kimataifa, kuzisaidia kuhamia kwenye masoko ya kikanda na kulinda ajira.