Kwa nini walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwa DRC kwa miaka 65?
Kwa nini walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwa DRC kwa miaka 65?
Historia ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeangaziwa na vita vikali vinavyohusishwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa wa kitaifa, mwingiliano wa migogoro ya kikanda, na unyonyaji wa maliasili nyingi za taifa hilo la Afrika ya Kati. Tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1960, Umoja wa Mataifa umeleta manufaa sana nchini DRC, ikiwa ni pamoja na kutumwa kwa operesheni tatu za amani ambazo kwa upande wake zimechagiza shughuli za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 65 iliyopita.
Tupate maelezo machache kuhusu historia ya uwepo wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
1.Uwepo wa UN baada ya DRC kupata uhuru
Umoja wa Mataifa uliingilia kati kwa mara ya kwanza nchini DRC wiki chache tu baada ya uhuru wa nchi hiyo, tarehe 30 Juni 1960, kufuatia miaka 75 ya utawala wa Ubelgiji. Mali ya kibinafsi ya Mfalme Leopold II kutoka 1885 hadi 1908, koloni rasmi ya serikali ya Ubelgiji, DRCongo ilinyonywa kwa maliasili yake na nguvu kazi yake, bila maandalizi yoyote ya kweli ya uhuru wa kisiasa.
Mnamo Julai 1960, uhuru ulitishiwa na majimbo mawili, Katanga na Kasai Kusini yenye utajiri wa madini. Baadaye walifaidika kutokana na kuungwa mkono na Ubelgiji na maslahi ya kiuchumi ya nje ambayo yanataka kudumisha udhibiti wa rasilimali za nchi.
Nchi hiyo ilizama katika mgogoro mkubwa wa kisiasa, uliochagizwa na mauaji ya Waziri Mkuu wake, Patrice Lumumba, mwaka wa 1961. Baada ya kukabiliana na hali hii, UN ilipeleka Operesheni ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DR Congo - ONUC mnamo Julai 1960.
Ujumbe wa kwanza wa kulinda amani UNOC unalenga kusaidia serikali huko Leopoldville, jina la zamani lililopewa mji mkuu, Kinshasa , kurejesha utulivu na umoja nchini na kuhakikisha kuwa wanajeshi wa Ubelgiji wanaondoka. Ujumbe huo, ambao ulikuwa na walinda amani 20,000 katika kilele chake ulichukua jukumu muhimu katika kumaliza kujitenga kwa Katangan mnamo 1963, kabla ya kujiondoa mnamo 1964.
2. MONUC: Jibu kwa vita vya DR Congo
Baada ya zaidi ya miaka 30 ya udikteta chini ya utawala wa Mobutu Sese Seko, nchi hiyo, ambayo wakati huo ilipewa jina la Zaire, ilitumbukia katika migogoro miwili iliyofuatana - vita vya "kwanza" (1996-1997) na "pili" (1998-2003) vya DR Congo.
Mnamo mwaka wa 1996, Rwanda, ikiungwa mkono hasa na Uganda na Burundi, iliingilia kati Mashariki mwa Zaire, kuwafukuza rasmi wanamgambo wa Kihutu, waliohusika na mauaji ya kimbari ya 1994, ambao walikuwa wamekimbilia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini.
Mnamo Mei 1997, kwa msaada wa kijeshi kutoka Kigali na Kampala, Laurent-Désiré Kabila alichukua mamlaka, na kumlazimisha Mobutu uhamishoni, na kuibadilisha nchi hiyo kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mnamo 1998, Kabila aliwageuka washirika wake wa zamani wa Rwanda na Uganda, ambao walikuwa wakiunga mkono uasi huko mashariki mwa nchi.
Kabila anaungwa mkono na Angola, Zimbabwe na Namibia.
Baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Kusimamisha Mapigano wa Lusaka mwaka 1999, UN ulituma Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUC) kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Hata baada ya kumalizika rasmi kwa vita mwaka 2003, DRC inasalia kuwa suala la kimkakati kwa mamlaka za kikanda, kutokana na maliasili yake ya kipekee (cobalt, coltan, dhahabu, almasi, shaba, nk.) na jukumu lake muhimu katika utulivu wa eneo la GREAT LAKES
3. MONUSCO: Ujumbe ulioendelea kuwepo
Mnamo mwaka wa 2010, MONUC ikawa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO na mamlaka iliyopanuliwa ambayo ilijumuisha ulinzi wa raia na msaada kwa serikali ya Congo katika kuimarisha amani na utulivu.Ikiwa bado imetumwa hivi karibuni katika majimbo matatu ya mashariki ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, MONUSCO iliondoa wanajeshi wake kutoka Kivu Kusini mnamo Juni 2024 kwa ombi la DRC.Walinda amani wa ujumbe huo wamesalia Kivu Kaskazini na Ituri.
Licha ya juhudi za Umoja wa Mataifa, makundi kadhaa yenye silaha yanaendelea kufanya kazi katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na Allied Democratic Forces (ADF) na M23 (March 23 Movement), ambayo inatetea maslahi ya Watutsi wa Kongo na kufurahia kuungwa mkono na majeshi ya Rwanda.
Tangu mwanzoni mwa 2025, M23, wakiungwa mkono na jeshi la Rwanda, wamehusika na mlipuko wa hivi punde wa ghasia mashariki mwa nchi hiyo, ambapo wanamiliki miji kadhaa ya kimkakati huko Kivu Kaskazini na Kusini.
4. Maliasili: sababu kubwa katika migogoro
DRC inafaidika kutokana na maliasili nyingi, hasa katika majimbo matatu ya mashariki. Wana akiba kubwa ya dhahabu, almasi na bati, ambayo hutumiwa katika vifaa vya elektroniki.
Kivu Kaskazini na Kusini pia ni tajiri wa coltani, chuma ambacho kinatamaniwa sana na sekta ya teknolojia kwa sababu ya matumizi yake katika utengenezaji wa 'capacitor' zinazopatikana katika simu za mkononi na kompyuta.
DRC pia ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa kobalti duniani, madini ya kimkakati yanayotumika katika utengenezaji wa takriban betri zote zinazoweza kuchajiwa tena, duniani hivi sasa. Amana za cobalt zinatumiwa katika Kivu Kaskazini na Kusini.
Rasilimali hizi za asili zinavutia uchoyo wa nchi jirani na ndio kiini cha migogoro ya eneo hilo, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo.
Makundi yenye silaha, kama vile M23, yanashutumiwa kwa kutumia rasilimali hizo kinyume cha sheria ili kufadhili shughuli zao, kwa ushirikiano wa makampuni ya ndani na nje ya nchi, pamoja na nchi jirani.
Umoja wa Mataifa umeweka mikakati kadhaa ya kukabiliana na biashara haramu ya madini, zikiwemo mbinu za kuziwekea vikwazo kampuni zinazohusika na biashara hiyo na vikwazo vya silaha ili kukabiliana na kuenea kwao nchini DRC. Hata hivyo, vita dhidi ya unyonyaji haramu wa rasilimali bado ni changamoto kubwa.