Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Haiti wako chini ya mashambulizi huku ukatili ukiongezeka kwa asilimia 1000: UNICEF

Mwanamke aliyekimbia makazi yake Tamaila Augustin kutoka Haiti akimbeba mtoto wake uani.
© UNICEF/Ralph Tedy Erol Mwanamke na mtoto waliokimbia makazi yao sasa wanaishi katika shule katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince pamoja na wakibizi wengine wa ndani.

Watoto Haiti wako chini ya mashambulizi huku ukatili ukiongezeka kwa asilimia 1000: UNICEF

Amani na Usalama

Mgogoro wa kibinadamu unazidi kuongezeka nchini Haiti huku makundi yenye silaha yakiendelea kutekeleza ukatili wa kutisha dhidi ya watoto limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Kulingana na msemaji wa UNICEF, James Elder, ukatili wa kingono dhidi ya watoto umeongezeka kwa asilimia 1,000 katika mwaka uliopita, na kugeuza miili yao kuwa uwanja wa vita.

Takwimu hizi za kutisha, amesema ambazo haijapewa uzito unaostahili na vyombo vya habari vya kimataifa, zinaonyesha hali ngumu inayowakumba vijana wa Haiti.

Akitoa mfano amesema “Mmoja wa waathiriwa, Roseline mwenye umri wa miaka 16, alitekwa nyara, akapigwa kikatili, na kubakwa mara kwa mara kwa kipindi cha mwezi mzima kabla ya kuachiliwa na watekaji wake. Sasa anaishi katika nyumba salama inayosaidiwa na UNICEF, moja kati ya nyingi zinazowahifadhi wasichana waliopitia madhila kama yake.”

Makundi yenye silaha yanadhibiti asilimia 85 ya mji wa Port-au-Prince

Kwa mujibu wa UNICEF mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, kwa sasa uko chini ya udhibiti wa makundi yenye silaha, huku yakiripotiwa kudhibiti takriban asilimia 85 ya jiji hilo.

Ukosefu wa usalama umesababisha ongezeko kubwa la uandikishaji wa watoto katika makundi haya, ambapo ripoti zinaonyesha ongezeko la asilimia 70 katika mwaka uliopita limesema shirika hilo.

Inakadiriwa kuwa hadi nusu ya wanachama wa makundi haya ni watoto, baadhi yao wakiwa na umri wa miaka minane tu.

Wengine wanalazimishwa kujiunga, huku wengine wakishurutishwa au kutokana na hali ngumu inayosababishwa na umasikini uliokithiri. Mzunguko huu hatari unaendeleza mateso kwa watoto wa Haiti, ambao ndio wahanga wakuu wa mgogoro huu.

Huduma muhimu ziko kwenye hatihati ya kuporomoka

Ghasia zinazoendelea zimesababisha huduma muhimu za Haiti karibu ya kuporomoka kabisa. Hospitali zimezidiwa uwezo, huku zaidi ya nusu ya vituo vya afya nchini vikikosa vifaa vya msingi vya matibabu.

Zaidi ya watoto milioni 1.2 wanaishi chini ya tishio la mara kwa mara la mashambulizi ya silaha, huku 500,000 wakiwa wameyakimbia makazi yao. Limesema shirika la UNICEF

Limeongeza kuwa mfumo wa elimu pia umedorora, ambapo zaidi ya watoto 300,000 wanakabiliwa na changamoto kutokana na kufungwa kwa shule na kufurushwa kwenye makazi yao.

UNICEF imesisitiza kuwa athari mbaya kwa watoto wa Haiti hazihusiani tu na ghasia za sasa, bali pia zinahatarisha afya yao ya muda mrefu, elimu, na maendeleo yao kwa ujumla.

Juhudi za jamii na mnepo

Hata hiyo Elder amesema licha ya hali hii mbaya, raia wa Haiti wanaendelea kupambana kwa ajili ya mustakabali bora.

Mpango wa UNICEF wa U-Report, ambao ni jukwaa la kidijitali linalohusisha vijana katika masuala ya kijamii, umehamasisha vijana 135,000 nchini Haiti kutoa msaada muhimu. Katika mwezi mmoja pekee wa mwaka 2024, waandishi wa U-Report walisaidia kutambua na kuripoti visa vya utapiamlo, ukosefu wa chanjo, na msaada muhimu kwa wanawake wajawazito katika jamii zilizofurushwa. Ameongeza kuwa juhudi hizi za kijamii zinaonyesha mnepo wa jamii za Haiti hata katikati ya changamoto kali.

Wito wa dharura wa msaada wa kimataifa

UNICEF na washirika wake wamepiga hatua kubwa katika kutoa misaada, kwa kuanzisha vituo tembezi salama 32, kupeleka wataalamu wa afya 380, na kutoa msaada wa kifedha kwa takriban familia 30,000.

Hata hivyo, shirika hilo linasema upungufu wa fedha bado ni changamoto kubwa. Ombi la dharura la UNICEF Haiti la mwaka 2024 la dola milioni 221.4 limefadhiliwa kwa asilimia 28 pekee, hali inayotishia mipango muhimu inayolenga kuwalinda watoto na kuwazuia kuingia katika vurugu.

UNICEF imesisitiza kuwa “Bila msaada wa haraka wa kimataifa, watoto wa Haiti wataendelea kuteseka, na mzunguko wa ghasia utaendelea kwa vizazi vijavyo. Dunia lazima ichukue hatua sasa ili kulinda maisha na mustakabali wa watoto wa Haiti.