Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malori 10,000 ya misaada yameingia Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano: UN

Kikosi cha malori yaliyobeba misaada ya kibinadamu yanaingia katika Mkoa wa Gaza kupitia bandari ya Kerem Shalom, ikipita majengo yaliyoharibiwa na magofu. Watu wanatembea karibu na malori.
© UNICEF/Eyad El Baba Malori yaliyobeba misaada ya kibinadamu yakiingia Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha Kerem Shalom.

Malori 10,000 ya misaada yameingia Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano: UN

Amani na Usalama

Mpango wa jumuiya ya misaada ya kibinadamu wa kuijaza Gaza kwa msaada wa kuokoa maisha umefikia hatua muhimu leo huku habari zikithibitisha kuwa zaidi ya malori 10,000 ya misaada ya kibinadamu yameingia katika eneo hilo tangu kusitishwa kwa mapigano tarehe 19 Januari.

Mpango wa jumuiya ya misaada ya kibinadamu wa kuijaza Gaza kwa msaada wa kuokoa maisha umefikia hatua muhimu leo huku habari zikithibitisha kuwa zaidi ya malori 10,000 ya misaada ya kibinadamu yameingia katika eneo hilo tangu kusitishwa kwa mapigano tarehe 19 Januari.

Akitangaza hatua hiyo, mkuu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, amesema kuwa malori hayo yamesheheni misaada mbalimbali ikiwemo chakula cha kuokoa maisha, dawa, na mahema bidhaa ambazo zinahitajika sana na wakazi wa Gaza baada ya zaidi ya miezi 15 ya mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa Israel.

Kauli ya mkuu huyo wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA imetolewa wakati alipokuwa akijiandaa kujiunga na msafara wa misaada unaovuka kuingia kaskazini mwa Gaza.

Katika siku za hivi karibuni, Fletcher amekuwa na "mazungumzo ya kivitendo na mamlaka za Israeli huko Tel Aviv na Jerusalem ili kuhakikisha misaada ya Umoja wa Mataifa inaendelea kuingia Gaza kwa kiwango kikubwa.”

Mazungumzo haya yanajumuisha COGAT ambayo  ni chombo cha Israel kinachohusika na kuidhinisha maombi ya misaada kwa Gaza na Ukingo wa Magharibi na wizara ya mambo ya nje ya Israel.

Wapalestina waliokimbia makazi yao, wakiwemo wanawake na watoto, wanatembea kwenye vifusi huko Rafah, Ukanda wa Gaza, wakiwa wamebeba mali na mtungi wa gesi. Nyuma, majengo yaliyoharibiwa yanaonekana.
© WFP Wapalestina waliokimbia makazi yao wakipitia kwenye vifusi vya mijengo huko Rafah kusini mwa Gaza

Kusafisha kifusi ili kuishi

Kwa mujibu wa ofisi ya OCHA, zaidi ya watu nusu milioni wamerejea kaskazini mwa Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano.

Mahitaji ya chakula, maji, huduma za usafi, huduma za afya na mahema ni makubwa sana, huku baadhi ya wakazi wakirudi kwenye makazi yao ya zamani wakiwa na majembe kwa ajili ya kusafisha kifusi kwenye magofuya nyumba zao, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.

Katika taarifa mpya, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO lilisema limepokea malori 63 ya vifaa vya matibabu kutoka kwa washirika wa misaada ili kujaza upya maghala yake matatu yaliyoko Gaza.

Aidha, zaidi ya wagonjwa 100 waliokuwa wagonjwa mahututi na majeruhi wamehamishiwa Misri kwa matibabu ya dharura tangu kusitishwa kwa mapigano kuanza.

Wakati huo huo, OCHA imebainisha kuwa huduma za afya za msingi na za kawaida zinaendelea kutolewa kote katika Ukanda wa Gaza.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa magari matano ya wagonjwa yaliingia Gaza Jumanne ili kuimarisha uwezo wa huduma za dharura.

Uzalishaji wa chakula umepigwa jeki

Shirika la OCHA pia limeripoti kuwa katika Ukanda wa Gaza, maduka 22 ya kuoka mikate  yanayosaidiwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP sasa sasa yanafanya kazi kikamilifu.

Tangu kusitishwa kwa mapigano kuanza kutekelezwa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Chakula Duniani WFP, limewapatia zaidi ya watoto 80,000 na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha msaada wa chakula wa virutubisho vya lishe, huku UNICEF ikiendelea kusambaza msaada wa lishe kwa watoto wachanga.

“Washirika wa misaada ya kibinadamu wamewachunguza zaidi ya watoto 30,000 wa chini ya umri wa miaka mitano kwa utapiamlo tangu kusitishwa kwa mapigano. Kati ya hawa, kesi 1,150 za utapiamlo mkali zimegunduliwa, zikiwemo kesi 230 za unyafuzi,” limesema shirika la OCHA.

Aidha, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, limesambaza takriban tani 100 za chakula cha mifugo kusaidia wafugaji katika maeneo ya Deir al Balah na Khan Younis, likinufaisha mamia ya watu wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo.

Ili kuendeleza shughuli za elimu katika Ukanda wa Gaza, washirika wa elimu wameanzisha maeneo matatu mapya ya muda ya kujifunzia katika majimbo ya Gaza, Rafah na Khan Younis, kwa ajili ya watoto 200 wa shule.

Mwanamke na mtoto wa Kipalestina wakisherehekea usiku huko Gaza kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano.
© UNRWA Wapalestina Gaza wanasherehekea tangazo la makubaliano ya kusitisha mapigano.

Msukumo wa kusitisha mapigano

Misaada hii imeongezeka wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jumatano aliposisitiza wito wake wa kusitisha mapigano wa kudumu Gaza na kuachiliwa kwa mateka wote waliobaki, huku akipinga vikali pendekezo la kuwahamisha Wapalestina nje ya ardhi yao ya asili.

“Katika kutafuta suluhisho, hatupaswi kuzidisha tatizo. Ni muhimu kushikamana na misingi ya sheria za kimataifa. Ni lazima tuepuke aina yoyote ya ukandamizaji wa kikabila,” Antonio Guterres aliiambbia Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki Zisizotenguliwa za Wapalestina, ambayo ilikutana kupanga shughuli zake kwa mwaka huu.

Aliongeza kuwa “Lazima tuthibitishe suluhisho la mataifa mawili.”

Akisisitiza matamshi ya Katibu Mkuu, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema kuwa “kuhamishwa kwa lazima au kuhamishwa kwa watu bila msingi wa kisheria ni marufuku kabisa.”