DRC: Janga la haki za binadamu linazidi kuongezeka kadri M23 wanavyosogea
Janga la haki za binadamu katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) linaendelea kuzidi kuwa baya, wakati mapigano kati ya jeshi la serikali na kundi lenye silaha la M23 linaloungwa mkono na Rwanda yakienea kuelekea jimbo la Kivu Kusini kufuatia kundi hilo kuteka mji wa Goma. Ripoti zinaonyesha kuwa M23 imeendelea kusonga kusini kuelekea Bukavu, imeeleza Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) kupitia taarifa iliyotolewa leo Januari 31 mjini Geneva, Uswisi.
Tangu kuanza kwa mgogoro huu, mabomu yamepiga angalau maeneo mawili ya wakimbizi wa ndani (IDP), na kusababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia. “Tumethibitisha pia mauaji ya watu wasiopungua 12 yaliyofanywa na M23 kati ya tarehe 26 na 28 Januari.” Imesema OHCHR.
Aidha OHCHR imeeleza kuwa imerekodi matukio ya ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, vinavyodaiwa kufanywa na jeshi la serikali ya DRC na wapiganaji wa Wazalendo katika eneo la Kalehe. Na wamesema wanachunguza ripoti zinazoeleza kuwa wanawake 52 walibakwa na wanajeshi wa Congo katika Kivu Kusini, zikiwemo taarifa za kubakwa kwa makundi.
Katika maeneo mengine yanayodhibitiwa na M23 huko Kivu Kusini, kama vile Minova, kundi hilo limechukua shule na hospitali, limewafukuza wakimbizi wa ndani kutoka kambini na kuwalazimisha raia kujiunga na kundi lao kwa lazima au kufanya kazi za kulazimishwa.
Aidha, maafisa wa DRC wanaripoti kuwa takribani wanawake 165 walibakwa na wafungwa wa kiume wakati wa uvamizi wa gereza la Muzenze huko Goma mnamo tarehe 27 Januari, ambapo zaidi ya wafungwa 4,000 walitoroka wakati M23 lilipoanza mashambulizi yake dhidi ya mji huo.
Ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro umekuwa jambo la kutisha katika mzozo huo unaotumia silaha mashariki mwa DRC kwa miongo kadhaa. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Volker Türk, ana wasiwasi mkubwa kwamba kuzuka upya kwa ghasia hizi kunaweza kuongeza zaidi hatari ya ukatili wa kingono. Kuenea kwa silaha kwa kiwango kikubwa katika mji wa Goma kunazidisha hatari ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
OHCHR imesema inaendelea kupokea maombi ya dharura kutoka kwa raia wanaotafuta ulinzi na tunafanya kazi pamoja na wenzao wa Umoja wa Mataifa na washirika wengine ili kuhakikisha usalama wao.
Kadiri M23 inavyoripotiwa kusonga kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini, Kamishna Mkuu anatoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia na kwa pande zote kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu. Ni muhimu kufanya uchunguzi wa ukiukwaji wa haki, kwa lengo la kuwafikisha wahusika mbele ya sheria na kuhakikisha uwajibikaji wa kina.