Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

NTDs: Magonjwa yenye kinga na tiba lakini bado yanaua na kusababisha umaskini

Wakazi wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa usubi, matende na mabusha huko Muheza, mkoani Tanga nchini anzania.
© CDC Global Health
Wakazi wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa usubi, matende na mabusha huko Muheza, mkoani Tanga nchini anzania.

NTDs: Magonjwa yenye kinga na tiba lakini bado yanaua na kusababisha umaskini

Afya
  • Ni pamoja na usubi, ukoma, kichocho, donda ndugu, kuumwa na nyoka
  • Mabadiliko ya tabianchi, mizozo ni mojawapo ya vichocheo vya NTDs
  • Magonjwa yana tiba na kinga na kuna nchi zilizotokomeza baadhi yao.

Leo ni siku ya kimataifa ya magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele au NTDs. Haya ni magonjwa yanayosababishwa na aina tofauti za vijiumbe maradhi kama vile virusi, bakteria, vimelea, minyoo, kuvu na sumu. Vijiumbe maradhi hivi vinapompata binadamu husababisha madhara kwenye sio tu afya yake kupitia magonjwa, bali pia kiuchumi na kijamii.

Maeneo rafiki kwa NTDs

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, linasema NTDs huathiri zaidi jamii maskini kwenye maeneo ya kitropiki, au vijijini, kwenye mizozo na kusikofikika kirahisi ambako huduma za maji safi, kujisafi, na huduma za afya hupatikana kwa shida, hazitoshelezi au haziko kabisa.

Yanashamiri pia kwenye maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi, ambako upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na huduma za kujisafi ni shida. Ingawa hiyo baadhi ya NTDs hupatikana katika maeneo mengine yasiyo ya kitropiki.

Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs
WHO
Watoto wakiwa na vidonge vyao tayari kumeza ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs

Kwa nini huitwa magonjwa yasiyopatiwa kipaumbele?

Yanaitwa yasiyopatiwa kipaumbele kwa sababu kihistoria kwenye ajenda ya magonjwa duniani, yamekuwa yakipatiwa nafasi ya chini, na hata kama yakiwekwa juu, ufadhili bado ni changamoto.

Magonjwa hayo ni pamoja na matende, mabusha, vikope au trakoma, kung’atwa na nyoka, ukoma, malale, chaga, chikungunya, kichocho, minyoo ya tumbo, usubi na donda ndugu.

Mathalani, malale, husababishwa na kung’atwa na mbung’o; kichocho :usubi ambao huhusisha pia mgonjwa kupata upofu husababishwa na minyoo na kuenezwa na nzi wanaozaliana kwenye vijito.

Licha ya kuwa na kinga, magonjwa haya husababisha vifo vya maelfu ya watu kila mwaka. Hadi mwishoni mwa mwaka 2023, watu waliokuwa wanahitaji tiba angalau kwa aina moja ya ugonjwa wa NTDs walikadiriwa kuwa bilioni 1.5.

Gharama za NTDs kwa jamii

  • Nchi zinazoendelea, kila mwaka hugharimika mabilioni ya dola kutibu magonjwa haya yenye kinga.
  • Uzalishaji kazini na tija vinapungua
  • Familia kutumia kipato kwenye tiba badala ya kujiendeleza
  • Kijamii kuna ubaguzi na unyanyapaa kwa wagonjwa na hivyo kushindwa kufikia ustawi wao ikiwemo kielimu.
  • Magonjwa haya pia husababisha vifo na ulemavu

Je kuna kinga na tiba dhidi ya NTDs

WHO inasema magonjwa hayo yote yana kinga, yanaweza kudhibitiwa na kutokomezwa.

  • Mwaka 2024 nchi 7 zilitokomeza kabisa aina moja ya NTD ikiwemo Togo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
  • Hadi Desemba mwaka 2024 ,nchi 54 zilifanikiwa kutokomeza angalau aina moja ya NTDs, ikiwa ni zaidi ya nusu ya lengo la WHO la kutaka nchi 100 ziwe angalau zimetokomeza ugonjwa mmoja wa NTDS ifikapo 2030.
  • Nchi kadhaa zimetokomeza aina 2, 3, au 4 za NTDs.
Mfanyabiashara aliyeathiriwa na ukoma akisubiri wateja mjini Addis Ababa, Ethiopia.
ILO/Fiorente A.
Mfanyabiashara aliyeathiriwa na ukoma akisubiri wateja mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mara nyingi wenye uhitaji hawafikiwi

  • Mwaka 2023, zaidi ya watu milioni 860 walipatiwa tiba dhidi ya NTDs kupitia kampeni za utoaji dawa au usimamizi wa tiba kwa mgonjwa mmoja mmoja.
  • WHO inasema bado kuna pengo, na licha ya kuwepo kwa tiba, mara nyingi wanaohitaji dawa husika hawafikiwi.
  • Dawa dhidi ya NTDs zinatolewa na kampuni 12 za kutengeneza dawa kupitia mgao wa kimataifa wa dawa.
  • Kati ya mwaka 2011 na 2024, takribani vidonge na chupa za dawa bilioni 30 vilisambazwa kwa matibabu.

    COVID-19 ilivuruga kampeni dhidi ya NTDs

  • Ujio wa COVID-19 ulivuruga tiba na huduma dhidi ya NTDs. Hata hivoy hivi sasa mipango inaendelea kurejesha utekelezaji wake.
  • Mwaka 2020 WHO ilichapishwa Mkakati wa NTDs wa 2021-2030 ili kuhakikisha magonjwa hayo yanadhibitiwa na yanatokomezwa ifikapo mwaka 2030.
  • Hata hivyo kutokana na uwekezaji hafifu, malengo yaliyowekwa yakilandana na Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, yako hatarini kutofikiwa.
  • Changamoto ni pamoja na kubadilika kwa mfumo wa ufadhili, nchi husika kutomiliki kikamilifu mipango ya utokomezaji NTDs, ukosefu wa utaalamu, dawa, mbinu za uchunguzi, vifaa na ugumu wa kukusanya takwimu.
Sumu itokanayo na kung'atwa na nyoka inaweza kuleta madhara ya kimwili na kiakili na kusababisha mtu kupoteza mwelekeo wa maisha  yake.
Thea Litschka-Koen
Sumu itokanayo na kung'atwa na nyoka inaweza kuleta madhara ya kimwili na kiakili na kusababisha mtu kupoteza mwelekeo wa maisha yake.

Nini kifanyike kutokomeza NTDs?

WHO inapendekeza mikakati 5 ya kuchagiza kinga, udhibiti na kutokomeza ambayo ni:

  • Kubuni na kuimarisha mbinu za usimamizi wa magonjwa
  • Tibakinga kupitia mionzi
  • Kudhibiti mazalia ya vimelea vya wadudu
  • Kuimarisha afya ya umma ya wanyama
  • Kuhakikisha kuna huduma ya maji safi na huduma za kujisafi na usafi

Hivyo katika siku ya NTDs Januari 2025, WHO inataka kila mtu, wakiwemo viongozi na jamii kuungana, kuchukua hatua na kutokomeza magonjwa yasiyopatiwa kipaumbele, NTDs.