Goma: Kipaumbele cha MONUSCO ni kulinda raia, watumishi na mali - Dujarric
Goma: Kipaumbele cha MONUSCO ni kulinda raia, watumishi na mali - Dujarric
Amani na Usalama
- Walinda amani kuendesha doria ya tathmini
- Majina ya walinda amani waliouawa yatajwa
- Uwanja wa ndege Goma bado umefungwa
- Mpaka wa DRC na Rwanda uko wazi kwa misingi ya kiutu
Kipaumbele cha sasa kwa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni ulinzi wa watumishi wake, vifaa na raia ambao wamesaka hifadhi kwenye eneo la ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO jimboni Kivu Kaskazini.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani wakati akiwapatia taarifa mpya kutoka watendaji wa UN walioko kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu ambako siku mbili zilizopita ziligubikwa na mapigano makali kati ya jeshi la serikali, FARDC na waasi wa M23.
“Mapigano yameendelea kuripotiwa maeneo ya Sake na Kaskazini-Magharibi mwa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini,” amesema Dujarric, mji ambao mapema ilielezwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, kuwa kwa kiasi kikubwa unashikiliwa na waasi wa M23.
Amesema MONUSCO inapanga kutuma walinda amani wake kwenda kuendesha doria Goma ili kutathmini hali halisi ya usalama na barabara na pia kusambaza vifaa.
“Kwenye mji mkuu Kinshasa, hali pia imeripotiwa kuwa tulivu licha ya wito wa kutaka kufanyika kwa maandamano,” amesema Dujarric akiongeza kuwa barabara kuu zimefungwa, halikadhalika maduka makubwa kwa hofu ya kuporwa.
Majina ya walinda amani waliouawa yatajwa
Bwana Dujarric ametumia mkutano wake huo pia kutaja majina ya walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa waliouawa wakati wa mapigano huko Goma hivi karibuni.
Walinda amani hao ni Askari Rodolpho Cipriano Alverez Suarez kutoka Uruguay, aliyekuwa na umri wa miaka 39; na wawili kutoka Afrika Kusini, Askari Mokote Joseph Mobe, aliyekuwa na umri wa miaka 33, na Askari Andries Tshidiso Mabele, aliyekuwa na umri wa miaka 30.
Umoja wa Mataifa umetuma salamu za rambirambi kwa serikali za Uruguay na Afrika Kusini pamoja na wananchi na familia zao.
Kwa mujibu wa Dujarric, idadi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliojeruhiwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wa M23 ni 22.
“Natumia tena fursa hii kusisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, sio tu hayakubaliki, bali pia yanaweza kuwa uhalifu wa kivita,” amesema Dujarric.
Uwanja wa ndege wa Goma bado umefungwa
Akinukuu mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kutoa misaada nchini DRC, Dujarric amesema hadi sasa uwanja wa ndege wa Goma umefungwa na hivyo kufanya kuwa vigumu kuingiza misaada ya kibinadamu.
Halikadhalika, barabara nyingi zinazounganisha Goma na nchi jirani ya Rwanda nazo zimefungwa.
Ingawa hivyo mpaka wa Rwanda na DRC umesalia wazi kwa misingi ya kibinadamu ambapo baadhi ya wahudumu wa kibinadamu waliweza kuingia leo.
Ametoa wito kwa pande husika kwenye mzozo kuheshimu sheria za kiutu za kimataifa na kuachana na ghasia dhidi ya raia zilizoshuhudiwa hivi karibuni.