Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UDADAVUZI: UNFPA ni nini na kwa nini ni muhimu?

Mwanamke mjamzito anafanyiwa uchunguzi wa ultrasound kutoka kwa mkunga katika kituo cha afya nchini DR Congo, akitazama picha hiyo kwenye simu janja.
© UNFPA DRC/Junior Mayindu Mwanamke anapimwa uchunguzi wa afya ya uzazi katika kituo cha afya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

UDADAVUZI: UNFPA ni nini na kwa nini ni muhimu?

Afya

UNFPA, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi na haki za kijinsia, linafanya kazi katika zaidi ya nchi 150 kusaidia haki za wanawake na wasichana.

Shirika hili hushirikiana na serikali, mashirika, na jamii kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya, upangaji uzazi, na ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia. Kwa kifupi lengo lake kubwa ni kuhakikisha afya ya uzazi na haki kwa wote.

Dhamira ya UNFPA

UNFPA inalenga kuwa na dunia ambayo kila ujauzito ni wa kupangwa, kila kujifungua ni salama, na kila kijana anapata fursa ya kufanikisha ndoto zake. Shirika hili linahakikisha huduma bora za afya ya uzazi, hasa kwa wanawake na vijana, ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao na miili yao.

Wafanyakazi wa UNFPA wakiweka hema la kutoa misaada kwenye kilima huko Jajarkot, Nepal.
© UNFPA Nepal/Bikash Karki Kliniki tembezi ya UNFPA imeanzishwa baada ya tetemeko la ardhi huko Karnali, Nepal.

Kwa nini haki za uzazi ni muhimu

Kwa mujibu wa UNFPA haki za uzazi sio masuala ya kibinafsi pekee, zinaathiri jamii nzima.

Ukiukwaji wa haki hizi za uzazi kama vile ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia, na ukosefu wa upangaji uzazi husababisha watoto  kuacha shule, vifo vya wajawazito, na matatizo ya kiuchumi, yanayoathiri maendeleo ya dunia nzima.

Athari za kiuchumi za afya ya uzazi

Shirika hilo la UNPA linasema wanawake wakikosa huduma za afya, uchumi huathirika.

Mama anayefariki dunia wakati wa kujifungua hawezi kushiriki katika soko la ajira au kuwekeza katika jamii yake.

Uwekezaji katika afya ya uzazi huimarisha jamii, kustawisha uchumi, na kuongeza mnepo kwa kijamii.

Muuguzi aliyevaa koti jeupe akimpa mama mchanga aliyembeba mtoto wake kirutubisho cha chuma katika kliniki ya afya inayohamishika inayoungwa mkono na UNFPA.
© UNFPA Msumbiji/Mbuto Machili Ancha (kushoto) akipokea dawa za kuongeza dawa za kuongeza damu mwilini kutoka kwa Juliana Germano ndani ya kliniki tembezi ya UNFPA.

Malengo matatu muhimu ya UNFPA

UNFPA inalenga kumaliza vifo vya wajawazito vinavyoweza kuzuilika, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango, na kukomesha ukatili wa kijinsia.

Kupitia mafunzo ya wakunga, huduma za uzazi wa mpango, na mipango ya kuzuia ukatili wa kijinsia, UNFPA inatekeleza malengo haya.

Athari za kazi za UNFPA

Mwaka 2023 pekee, UNFPA ilisaidia kuzuia zaidi ya mimba zisizotarajiwa milioni 18, kutoa huduma za afya ya uzazi kwa watu milioni 27, na kuzuia zaidi ya vifo 34,000 vya wajawazito.

Pia, shirika hilo lilisaidia kuimarisha huduma za ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Muuguzi Tatiana Putria amesimama karibu na gari la wagonjwa UNFPA na ambulansi yenye hewa hafifu katika njia nyembamba huko Kherson, Ukraine.
© UNFPA Ukraine/Alina Stara Ambulensi inayoungwa mkono na UNFPA nchini Ukraine inawasaidia wauguzi kufikia wanawake na wasichana wanaohitaji.

Kusaidia walio katika mazingira magumu

Katika majanga na migogoro, UNFPA hutoa huduma muhimu za afya ya uzazi na ulinzi kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia na kingono.

Kuanzia maeneo ya vita hadi sehemu zilizoathirika na majanga ya asili, kliniki zake tembezi hutoa msaada wa dharura unaookoa maisha.

Kwa nini kazi ya UNFPA ni muhimu

Kwa mujibu wa UNFPA afya ya uzazi ni haki, na si anasa. Kila mwanamke, bila kujali mahali alipo au hali yake, anastahili uhuru wa mwili wake, usalama, na huduma za afya. Kazi ya UNFPA ni muhimu katika kujenga dunia yenye usawa na haki zaidi.