Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulisses de Mesquita Gomes wa Brazil, Kamanda mpya wa MONUSCO

Ulisses de Mesquita Gomes, Kamanda mpya wa Jeshi la MONUSCO, amesimama akiwa amevaa sare za kijeshi mbele ya nembo UN na bendera.
Ulisses de Mesquita Gomes Ulisses de Mesquita Gomes, Kamanda mpya wa Kikosi cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO

Ulisses de Mesquita Gomes wa Brazil, Kamanda mpya wa MONUSCO

Amani na Usalama

Jumanne ya Januari 28, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitangaza uteuzi wa Luteni Jenerali Ulisses de Mesquita Gomes wa Brazil, kuwa Kamanda mpya wa kikosi cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Luteni Jenerali Gomes anachukua nafasi ya Kaimu Kamanda wa kikosi cha MONUSCO, Meja Jenerali Khar Diouf wa Senegal, ambaye Katibu Mkuu ameshukuru kwa utumishi wake wa kujitolea.

Akizungumza na Idhaa ya Kireno ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya simu Luteni Jenerali Gomes amesema, « ni furaha kubwa kupokea taarifa za kuteuliwa na Katibu Mkuu wa UN António Guterres kuwa Kamanda wa Kikosi cha MONUSCO. Pia ni heshima kubwa kuwakilisha jeshi la Brazil, na bendera ya Brazil kwenye misheni hii muhimu wa ulinzi wa amani duniani. »

Amesema anapenda kuungana na raia, polisi na wanajeshi ndani  ya MONUSCO, “ Kwa pamoja tutafanya kazi kutekeleza majukumu ya MONUSCO hasa ulinzi wa raia na kuwezesha wananchi wa DRC kuwa na mustakabali bora. Asante sana, na  punde nitaelekea DRC. »

Kamanda huyo mpya wa kikosi cha MONUSCO ana uzoefu wa miaka 35 ya kuchukua hatua kwenye majanga, menejimenti ya mizozo na ulinzi wa amani.

Kwa mara ya mwisho ndani ya Umoja wa Mataifa alikuwa Mkuu wa kitengo cha Operesheni za kijeshi kwenye Idara ya Umoja wa Mataifa ya Operesheni za Ulinzi wa Amani.