DRC: Utulivu kiasi waripotiwa kurejea baada ya mapigano makali Goma; UNICEF yasaka dola milioni 22
DRC: Utulivu kiasi waripotiwa kurejea baada ya mapigano makali Goma; UNICEF yasaka dola milioni 22
- Utulivu kiasi Goma, M23 inadhibiti eneo kubwa
- Shule zimefungwa Goma na Nyiragongo
- UNICEF yasaka dola milioni 22 kukidhi mahitaji ya watoto 282,000
Baada ya siku mbili za mapigano makali kati ya jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) na waasi wa M23, huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, hali ya utulivu imeshuhudiwa kwa kiasi fulani tangu mchana wa tarehe 28 Januari 2025.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, (OCHA) imeripoti hii leo kwamba waasi wa M23 wanaonekana kudhibiti sehemu kubwa ya mji wa Goma, huku mapigano yakiacha uharibifu mkubwa wa miundombinu bila kusahau vifo na majeruhi miongoni mwa raia.
Wakimbizi wauawa Nyiragongo
Ofisi hiyo inasema katika makazi ya wakimbizi ya Rusayo namba 1 na Rusayo namba 2, kwenye kitongoji cha Nyiragongo, takribani watu 12 waliuawa na wengine 10 walijeruhiwa kufuatia mlipuko wa makombora siku ya Jumapili.
Katika kambi ya wakimbizi ya Kanyaruchinya, wakimbizi wamekimbia na kwenda kusaka hifadhi kwenye jamii za wenyeji, shule na majengo ya umma.
Maduka, ofisi na maghala yanayomilikiwa na mashirika ya misaada ya kibinadamu yamelengwa na kuporwa.
Hakuna huduma ya intaneti
Huduma muhimu mjini Goma zimevurugika kwa kiasi kikbwa, “huduma za maji na umeme zilisitishwa tangu tarehe 26 Januari, huku mtandao wa intaneti ukikatwa tangu mchana wa tarehe 27 Januari. Hali hii imeathiri juhudi za misaada ya kibinadamu, ingawa mawasiliano ya simu za mkononi bado yanafanya kazi,” imesema taarifa ya OCHA.
Shule Goma na Nyiragongo zimefungwa
Kwa sasa, huduma za afya na zile za maji, usafi wa mazingira ndizo zinazotolewa kwa kiwango cha chini.
Tangu tarehe 22 Januari, shule zote zilizoko mjini Goma na Nyiragongo zimefungwa kutokana na machafuko.
Hospitali zimefurika na wahudumu wa misaada wanajitahidi kutoa huduma kwa waliojeruhiwa, licha ya changamoto za kukatika kwa umeme na maji.
Uokoaji wa wagonjwa pia umekuwa mgumu baada ya magari ya wagonjwa kushambuliwa, ambapo dereva mmoja wa gari la wagonjwa alipigwa risasi tarehe 28 Januari.
UNICEF yasaka dola milioni 22 kusambaza huduma za kibinadamu Goma
Kufuatia kuvurugwa kwa shughuli za kibinadamu na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, (UNICEF) limezindua ombi la dola milioni 22 kushughulikia mahitaij ya dharura ikiwemo huduma za majisafi ya kunywa, huduma za kujisafi, dawa, vifaa vya matibabu, huduma za ulinzi kwa watoto na kutibu utapiamlo.
Kaimu Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Jean Francois Basse kupitia taarifa iliyotolewa leo Kinshasa, mji mkuu wa DRC, amesema wana hofu kubwa kutokana na kuendeleza kuzorota kwa hali ya kibinadamu ambapo fedha hizo zinalenga watoto 282,00 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
“Hali Goma ni mbaya sana, na imefanya hali ya kibinadamu iliyokuwa mbaya sasa kuwa taabani. Raia wamechoshwa na matukio ya kutisha, wana njaa, kiu na uchovu wa kupindukia. Familia hazina huduma za maji, umeme, na intaneti na sasa wanasaka hifadhi kokote pale,” amesema Basse.
Amesema hofu iliyoko sasa ni watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kuambukizwa magonjwa kama vile kipindupindu, surua na mpox. “Kutokana na hofu ya mapigano, wazazi wanahofia kupeleka watoto wao hospitali.”
Amesema ni vema pande husika kusitisha ghasia kwani zinaongeza machungu kwa watoto.