Baraza la Usalama la UN lakutana, Rwanda na DRC zarushiana lawama juu ya hali inayoendelea
Baraza la Usalama la UN lakutana, Rwanda na DRC zarushiana lawama juu ya hali inayoendelea
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mchana huu kwa saa za New York, jijini Marekani, wakati huu ambapo hali ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC inazidi kuzorota, uwanja wa ndege wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini ukiwa tayari umetwaliwa na waasi wa M23 ambao Umoja wa Mataifa unasema wanaungwa mkono na Rwanda.
Kauli ya MONUSCO kutoka kwa Vivian van de Perre
Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, anayehusika na Ulinzi na Operesheni, Vivian van de Perre amehutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video akisema kuwa changamoto za kiusalama na kibinadamu zimeongezeka.
M23 walifanya shambulio kubwa wakitumia silaha nzito mjini Goma, punde tu baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama Jumapili ya tarehe 26 mwezi huu.
MONUSCO imepokea idadi kubwa ya watu wanaosaka msaada wakiwemo wafanyakazi, raia na wanamgambo waliojisalimisha.
“Kuhamisha majeruhi imekuwa changamoto kubwa, mfano kule Sake, siku nne zilizopita. Mashambulizi ya wiki iliyopita yameharibu miundombinu kama barabara na hata kukwamisha usafirishaji wa bidhaa muhimu kama vile dawa, vyakula,” amesema Bi. Van de Perre.
Ameongeza kuwa bohari la MONUSCO katika uwanja wa ndege Goma limeporwa vifaa vyake. Huku wafungwa wakiripotiwa kutoroka gereza la Goma ,hali inayotia mashakani usalama kwa wanawake na watoto.
“Tunatoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano ili kurejesha usalama,” amesema Naibu Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu nchini DRC.
Mapema leo mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliripoti kwamba vurugu zimeshamiri kwenye mitaa ya mji wa Goma, idadi ya vifo ikiongezeka, na watu wakikimbia eneo hilo, huku kambi za wakimbizi mjini humo zikisalia tupu.
Kurejesha mchakato wa amani wa Luanda ndio jawabu pekee la amani ya kudumu, amesema Bi. Van de Perre akiongeza kuwa vita si suluhu ya amani.
Tunatumaini matokeo kutoka vikao vya AU na EAC - Ufaransa
Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa Nicolas de Rivière amesema tunavyozungumza hivi sasa M23 inadhibiti Goma ikisaidiwa na Rwanda, “kutwaliwa kwa Goma inatia wasiwasi mkubwa kwa raia. M23 lazima iondoke haraka kwenye maeneo inayoshikilia.”
Amesema ni matumaini yake kuwa vikao vya Muungano wa Afrika, (AU) na Jumuiya ya Afrika MAshariki, (EAC) vitaleta suluhu ya kikanda kwenye mgogogoro huo.
Balozi Rivière amelaani pia mashambulizi ya M23 dhidi ya MONUSCO, wahudumu wa kibinadamu na raia, akisema vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu.
Sierra Leone, Algeria na Msumbiji
Fursa pia ilipatiwa nchi tatu za Afrika zenye ujumbe Baraza la Usalama ambazo ni Sierra Leone, Algeria na Msumbiji au (A3).
Mwakilishi wa Sierra Leone kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Michael Imran Kanu akizungumza kwa niaba ya A3 amesema, chini ya saa 72 Baraza limekutana kujadili mara mbili kuhusu hali ya DRC na uwezekano wa mzozo kuvuka mpaka.
“Tumesikiliza kwa makini kauli ya Van de Perre na machungu wanayopitia wananchi. Silaha lazima zinyamazishwe. Kwa hivyo basi tunataka mambo matatu ikiwemo sitisho la mapigano, haraka na utulivu, Goma. M23 iache kusonga mbele, na pande zote zilinde raia. Ni muhimu jitihada zote iwe kutoka MONUSCO au yeyote yule zijikite katika kulinda raia.”
Jambo lingine amesema ni muhimu kwa viongozi wa Rwanda na DRC kutekeleza kwa nia njema makubaliano ya mchakato wa Luanda, akirejelea sitisho la mapigano lililopitishwa lakini likakiukwa.
Janga gani la kibinadamu DRC litakidhi hatua thabiti za Baraza?
Fursa ikafika ya Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC Thérèse Kayikwamba Wagner ambaye ameanza kwa kutuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa walinda amani waliouawa katika mapigano kati ya waazi wa M23 na jeshi la serikali FARDC.
Amesema “tunatuma salamu za rambirambi kwa Rwanda pia kutokana na askari wao waliouawa ndani ya ardhi ya DRC ingawa yenyewe inakataa kuweko kwa askari wake ndani ya ardhi yetu,” amesema Bi. Wagner.
Tunahakikisha ulinzi wa wafanyakazi wa UN
Akizungumzia machafuko kwenye mji mkuu Kinshasa, Waziri Wagner amehakikishia jamii ya kimataifa kuwa serikali inachukua kila mbinu kuhakikisha ulinzi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa DRC amezungumzia michakato ya amani ikiwemo wa Luanda na Nairobi akieleza wajumbe kwamba “Rwanda imethibitisha kuwa kauli zenu hazimaanishi chochote kwake,” akisihi wajumbe wa Baraza la Usalama lichukue hatua thabiti likitambua vitendo vya Rwanda.
Amesema wanaoathirika si tu raia wa DRC bali wa mataifa mengine akigusia walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha akiwemo wa Uruguay.
“Ni kiwango gani cha uharibifu na ukiukaji wa haki za binadamu kwenye ardhi yetu kinapaswa kufikiwa ili kiweze kuchukuliwa hatua?” amehoji Bi. Wagner.
Hakuna askari wa Rwanda aliyefia DRC – Balozi Rwamucyo
Kisha Rais wa Baraza akampatia nafasi ya kuzungumza Mwakilishi wa kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ernest Rwamucyo ambaye amekanusha kuweko kwa wanajeshi wa Rwanda waliofia DRC, akisema kama kuna ushahidi uwasilishwe. "Nina hakika hakuna ushahidi huo."
Amelaani uchokozi unaofanywa na serikali ya DRC ya kushambulia eneo lake la mpakani.
“Rwanda kila wakati itachagua amani katika mzozo huu ambao sisi tuna mengi ya kupoteza kwa kuwa tunafahamu faida ya amani. Sisi tumejizatiti kwenye kusimamia amani,” amesema Balozi Rwamucyo.
Rwanda inapokea wakimbizi Rubavu
Amesema hivi sasa Rwanda kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa wanasaidia wakimbizi wanaokimbilia Rwanda.
“Tayari tumeandaa kambi ya wakimbizi Rubavu na tayari tunafanikisha uhamishaji wa wafanyakazi wa kimataifa wakiwemo wa Umoja wa Mataifa kupitia Kigali,” amesema Balozi Rwamucyo akielezea pia jinsi ambavyo Muungano wa Ulaya umeomba kusaidiwa kuhamisha watendaji wake.
Kuhusu mashambulizi kwenye jengo lake la ubalozi Kinshasa, amesema “Rwanda inaomba serikali ya DRC iwajibike na mikataba ya kimataifa ya kulinda ofisi za kibalozi.”
Balozi Rwamucyo amesema iwapo Rais wa DRC Felix Tshisekedi angalikubali wito wa mazungumzo, mzozo huu ungalishaisha akisema alienda kinyuma na Mchakato wa Nairobi, ikiwa ni pamoja na kutoa kauli za chuki dhidi ya Rwanda ambapo “Ondoeni utawala huu wa kihovyo huko Kigali,” akimnukuu Rais Tshisekedi akizungumza na vijana wa kinyarwanda.
Hatuwezi kunyamazia kauli za kichochezi
Mwakilishi huyo wa Rwanda amesema katika kutekeleza hatua hiyo, “Rais wa DRC amehamasisha vikundi vya waasi kikiwemo FDRL na Wazalendo ili kutekeleza azma hiyo jambo ambalo Rwanda haiwezi kunyamazia.”
Amesema Rwanda inasalia kushikamana na mchakato wa amani ikiwemo wa Luanda kwa lengo la kupata amani ya kudumu ukanda huo wa Maziwa Makuu na inasisitiza kila pande kuzingatia mkataba huo.
Ametamatisha kwa kujulisha wajumbe kuwa Rais Paul Kagame amezungumza na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini jana Jumatatu na wamekubaliana kuanza tena kwa mazungumzo ya kisiasa ikiwa ni pamoja na AFC na M23.
Kutoka OCHA
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misada ya dharura, OCHA, imesema “hali imefikia pabaya huku mapigano makali kati ya kundi la waasi la M23 linailoungwa mkono na Rwanda na majeshi ya Congo yakitishia maisha ya raia. Huku chakula na maji vikikosekana na ufikiaji wa misaada kuzuiliwa, saa 24 zijazo zitakuwa muhimu kwa watu waliokwama katikati ya mapigano,”
Kutoka WHO
Dkt. Adelheid Marschang, Mratibu wa hatua za dharura kutoka WHO, amesema kwamba “wagonjwa wengi wanatibiwa majeraha ya risasi na vipande vya chuma, huku hatari ya maambukizi ikiongezeka. Wanawake na wasichana wanakutana na ukatili mkubwa, ikiwa ni pamoja na ubakaji, huku ripoti zikionyesha visa vingi vya ubakaji wakati wakienda kuchanja kuni.”
Kutoka OHCHR
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, leo jijini Geneva, Uswisi ameonya kuwa janga la haki za binadamu katika mji wa Goma, imewaacha raia wakikabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na amezikumbusha pande zote kuhusu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa kulinda raia.