Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Goma DRC: Türk atoa wito wa hatua za haraka kukabiliana na janga kubwa la haki za binadamu

Watu waliokimbia makazi yao wanakimbia kutoka kambi ya wakimbizi wa ndani karibu na Goma, DRC, huku baadhi yao wakiendesha pikipiki zilizojaa kupita kiasi kando ya barabara iliyojaa watu.
© WFP/Moses Sawasawa Watu waliotawanywa na ukosefu wa usalama huko Goma wanakimbia mji.

Goma DRC: Türk atoa wito wa hatua za haraka kukabiliana na janga kubwa la haki za binadamu

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, leo jijini Geneva, Uswisi ameonya kuwa janga la haki za binadamu katika mji wa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), umewaacha raia wakikabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na amezikumbusha pande zote kuhusu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa kulinda raia.

Kundi la waasi la M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda wanapambana na majeshi ya DRC, yakisaidiwa na kundi la wanamgambo la Wazalendo, katika mji wa Goma. Makombora yameanguka katika takribani maeneo mawili yanayohifadhi watu waliopoteza makazi yao. 

“Kadri ghasia na mapigano ya mijini yanavyoongezeka ndani ya Goma, raia wanakabiliwa na hatari kubwa – ikiwa ni pamoja na matumizi ya silaha za mlipuko kama vile mizinga na makombora katika maeneo yenye watu wengi,” almenya Kamishna Türk.

“Kuenea kwa ghasia katika vijiji na miji mingine kutazidisha mgogoro wa haki za binadamu uliopo,” ameongeza, akieleza hofu kwamba mapigano yanaweza kusambaa hadi miji mingine muhimu katika Kivu Kaskazini na hadi Mkoa wa Kivu Kusini.

Ripoti zinaonesha maelfu ya raia wamepoteza makazi yao tangu mapigano yaanze, na upatikanaji wa chakula, maji na umeme unazidi kuwa mbaya. Upatikanaji wa intaneti na huduma nyingine za mawasiliano pia umepunguzwa.

“Maelfu ya watu ambao tayari wamepitia ghasia, kupoteza makazi na hali ngumu za maisha wamelazimika kukimbia tena,” alisema Kamishna Mkuu.

Wasiwasi utawala wa sheria

Türk pia ameonesha wasiwasi juu ya kuzorota kwa hali ya usalama na utawala wa sheria katika Goma baada ya wafungwa wapatao 4,763 kutoroka kutoka gereza la Muzenze, gereza kubwa zaidi Goma, tarehe 27 Januari.

Türk ameeleza wasiwasi kuhusu hali ya watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari, na wanaharakati wa mashirika ya kiraia huko Goma na ametoa wito wa kuhakikisha usalama wao. Pia ameonya kuhusu hatari kubwa ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono. 

Pia Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kukomesha hotuba za chuki na mashambulizi yanayoendeshwa kwa misingi ya kikabila, ikiwa ni pamoja na yale yanayolenga watu wanaoonekana kuwa wa jamii ya Kitutsi au wanaochukuliwa kuwa wasaliti. Amewahimiza wahusika wote, wakiwemo viongozi wa jadi, kidini, kisiasa na wenye ushawishi, kukuza umoja wa kijamii.

Amewakumbusha wahusika wote wa mzozo kwamba vitendo vyao vinafuatiliwa na kwamba watawajibishwa kwa ukiukwaji mkubwa na uhalifu wote watakaofanya.