Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 4 waua na 3 wajeruhiwa katika shambulizi kwenye hospitali ya Saudi El Fasher Sudan: UNICEF

Hapa ni katika hospitali moja mjini Port Sudan, nchini Sudan ambako akina mama wanahudumia watoto wao wanaougua unyafuzi. Vita imesababisha uhaba wa chakula nchini Sudan.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfatih
Hapa ni katika hospitali moja mjini Port Sudan, nchini Sudan ambako akina mama wanahudumia watoto wao wanaougua unyafuzi. Vita imesababisha uhaba wa chakula nchini Sudan.

Watoto 4 waua na 3 wajeruhiwa katika shambulizi kwenye hospitali ya Saudi El Fasher Sudan: UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limealaani vikali shambulio dhidi ya hospitali ya Saudi El Fasher Kaskazini Darfur lilikokatili Maisha ya watu wakiwemo watoto na kujeruhi wengine llikisema shambulizi hilo linadhihirisha hatari zinazoongezeka kwa watoto katika maeneo ya vita.

Shambulio hilo lililotkea mwishoni mwa wiki kwa mujibu wa UNICEF limekatili Maisha ya watoto wanne, akiwemo msichana mmoja na wavulana watatu, na kujeruhi wavulana wengine watatu.

UNICEF inasema “Watoto hawa walikuwa miongoni mwa wagonjwa waliokuwa wakiendelea kupata matibabu katika wodi ya dharura ya hospitali hiyo, wakitibiwa majeraha yaliyosababishwa na mabomu yaliyotangulia kutokea katika eneo hilo. Tukio hili la kusikitisha linaonyesha hatari zinazoendelea zinazokumba watoto waliokwama katikati ya mapigano.”

Huu ni ukiukwaji wa haki za watoto 

Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, amekemea shambulizi hilo, akilielezea kama "ukiukaji wazi wa haki za watoto."

Amesema, "Watoto wanauwawa na kujeruhiwa katika sehemu ambazo wanapaswa kuwa salama zaidi dhidi ya madhara," akirejelea hospitali, ambazo zinapaswa kuwa maeneo ya huduma na usalama.

Ameongeza kuwa mashambulizi kama haya yanaongeza mzigo kwa hali mbaya inayowakumba watoto na familia waliozingirwa na vita, kutokuwa na usalama, na kukosa ulinzi.

Changamoto ya huduma za afya

Bi Russel amesema mgogoro wa afya Sudan umeongezeka huku hospitali zikikosa kufanya kazi.
Ameongeza kuwa “nchini Sudan, zaidi ya asilimia 70 ya hospitali katika maeneo yaliyoathiriwa na vita hazifanyi kazi kwa sasa kutokana na uharibifu, uharibifu wa miundombinu, au ukosefu wa vifaa. Hospitali nyingine zinatumika kama makazi au kwa madhumuni mengine, jambo linalozuia utoaji wa huduma muhimu za afya.”

UNICEF inasema mgogoro unaoendelea umezuia usambazaji wa vifaa vya matibabu, chanjo, na uchanjaji wa kawaida, na kuendelea kuzidisha mgogoro wa kibinadamu na kuweka maisha ya watu wengi, hasa watoto, katika hatari kubwa.

Pia shirika hilo limesema uvunjaji wa Sheria za kimataifa wakati mashambulizi dhidi ya hospitali yakiendelea.
Kulingana na sheria za kimataifa za kibinadamu, hospitali zinapaswa kuwa na ulinzi maalum na hazipaswi kushambuliwa amesema mkuu huyo wa UNICEF. Ameongeza kuwa mashambulizi dhidi ya hospitali yanaathiri uwezo wa kutoa huduma muhimu za matibabu na msaada kwa raia, ikiwa ni pamoja na watoto. Mashambulizi haya yanavunja sheria na kuzuia huduma za maisha kwa watu wa kawaida.

Wito wa kukomesha haraka machafuko

Bi. Russell amesisitiza kuwa ghasia nchini Sudan lazima ziskomeshwe mara moja. Alionya kuwa mashambulizi haya yana madhara ya moja kwa moja na ya muda mrefu kwa afya ya watoto na upatikanaji wa huduma za matibabu.

"Vita lazima vikome sasa. Watoto Sudan hawawezi kusubiri tena," amesisitiza, akitoa wito kwa pande zote za mgogoro kuhakikisha ulinzi wa raia, hasa watoto, na kuruhusu upatikanaji wa huduma za matibabu za kuokoa maisha.

Amehitimisha taarifa yake kwa kusema “Shambulizi hili linatufanya tukumbuke hitaji la haraka la kusitishwa kwa ghasia na ulinzi wa vituo vya afya nchini Sudan ili kulinda maisha ya watoto na raia wengine wasio na hatia waliokwama katikati ya vita vinavyoendelea.”