Kinachoendelea Goma DRC ni jinamizi la kibinadamu linalohitaji hatua za haraka: UN
Kinachoendelea Goma DRC ni jinamizi la kibinadamu linalohitaji hatua za haraka: UN
Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa leo yameonya juu ya janga la kibinadamu linaloendelea kukua Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kunusuru Maisha ya watu.
Mashirika hayo yamesema raia wako katika hatari kubwa huku misaada muhimu ya kibinadamu inayihitajika ikishindwa kuingia na kuwafikia.
“Hali imefikia pabaya huku mapigano makali kati ya kundi la waasi la M23 linailoungwa mkono na Rwanda na majeshi ya Congo yakitishia maisha ya raia. Huku chakula na maji vikikosekana na ufikiaji wa misaada kuzuiliwa, saa 24 zijazo zitakuwa muhimu kwa watu waliokwama katikati ya mapigano,” wamesema maafisa wa Umoja wa Mataifa.
Mapigano makali na mateso vyatawala
Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA Jens Laerke, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo ameripoti kwamba “Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, unatikisika kwa risasi za silaha ndogo na mizinga, huku maiti nyingi za watu zikiwa zimelala barabarani."
Ripoti hizi zinaonyesha uzito wa ghasia zinazoukumba mji hu. Laerke pia amesisitiza kuhusu visa vya ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji, uporaji wa mali, ukiwemo wa ghala la misaada, na mashambulizi kwenye vituo vya afya.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO, Hospitali zimefurika na hatari ya magonjwa inazidi kuongezeka.
Limeongeza kuwa hospital nyingi za mji huo zimezidiwa uwezo kutokana na wimbi kubwa la wagonjwa kukabiliana na majeruhi waliokuwa wakifikishwa kwa wingi.
Dkt. Adelheid Marschang, mratibu wa hatua za dharura kutoka WHO, amesema kwamba wengi wa wagonjwa wanatibiwa majeraha ya risasi na vipande vya chuma, huku hatari ya maambukizi ikiongezeka. Aidha, wanawake na wasichana wanakutana na ukatili mkubwa, ikiwa ni pamoja na ubakaji, huku ripoti zikionyesha visa vingi vya ubakaji wakati wakienda kusenya kuni.
Kwa mujibu wa WHO mfumo wa afya ambao tayari ulikuwa dhaifu unakutana na changamoto zaidi, kwani eneo hilo pia linakabiliana na tishio la kuenea kwa magonjwa kama vile kipindupindu, homa ya matumbo, malaria, na aina mpya ya virusi vya homa ya nyani au mpox.
Limeongeza kuwa “Hali hii inazidisha wasiwasi kwa umma, ikifanya kuwa vigumu zaidi kufuatilia na kutibu magonjwa.”
Uhaba wa chakula na misaada mingine ya kibinadamu
Kwa upande wake msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, Shelley Thakral, amesisitiza kuhusu uhaba wa chakula katika mji wa Goma, ambapo ghasia zimeongeza bei za vyakula.
Amesema “Mapigano hayo yamefunga barabara, bandari, na uwanja wa ndege wa Goma, na kusababisha kusitishwa kwa usambazaji wa misaada.”
WFP imesitisha misaada ya chakula kwa muda katika maeneo ya Goma na Thakral afisa huyo ameonya kuwa, kulingana na muda wa ghasia hizi, usambazaji wa chakula mjini Goma unaweza kuathiriwa vibaya zaidi.
Ameendelea kusema kwamba “Wakati familia zikiendelea kukimbia ghasia, wanakutana na changamoto zisizoelezeka, wengi wakilazimika kuvuka ziwa Kivu kwa mashua zisizo salama, wakichukua hatari kubwa katika njia hiyo.”
Ghasia zinazoendelea zinasababisha athari kubwa kwa usalama wa raia na wafanyakazi wa huduma za afya amesema Dkt. Marschang akisisitiza kuwa hatari kwa wanawake wajawazito, ambao wanakutana na viwango vya juu vya vifo vya uzazi, na hatari kubwa kwa wanawake na wasichana katika eneo hilo. "Mashambulizi dhidi ya huduma za afya yanakiuka sheria za vita. Huduma za afya lazima zilindwe wakati wote," amesema, akilaani ripoti za kupigwa risasi kwa wafanyakazi wa huduma za afya na wagonjwa, wakiwemo watoto wachanga, kukwama katikati ya mapigano.
Janga hili la kibinadamu linahitaji hatua za haraka
Wakati huu mapigano yakizidi kuendelea Goma na viunga vyake, mashirika ya misaada ya kibinadamu yanatoa wito wa hatua za haraka ili kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya wale waliokwama katikati ya ghasia.
Yamesema “Saa 24 zijazo zitakuwa muhimu kwani mji wa Goma na wakazi wake wanakutana na vitisho vya ghasia, kufurushwa, uhaba wa chakula, na hatari za kiafya”.
Umoja wa Mataifa na washirika wake wanatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano ili misaada iweze kufika kwa watu wanaohitaji na kuchukua hatua za kulinda raia na vituo vya afya dhidi ya madhara zaidi.
Mashirika hayo yamesema mgogoro unaoendelea Goma unaonyesha hitaji la dharura la hatua za kimataifa ili kuzuia vifo zaidi na kupunguza mateso ya watu waliokwama katikati ya moja ya migogoro ya kibinadamu inayoendelea kukua zaidi duniani.