Hali ya usalama mjini Goma, DRC ni tete na hatari
Hali ya usalama mjini Goma, DRC ni tete na hatari
Jean-Pierre Lacroix, Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, amesema hali ya usalama kwenye mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni tete na ni hatari kubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani kwa njia ya video kutokea Damascus, Syria aliko kwa ajili ya ziara ya masuala ya amani na usalama.
M23 wanazidi kusonga mbele
Bwana Lacroix amesema, “nieleze mwanzoni kabisa kwamba wenzetu huko Goma wametueleza kuwa eneo la Goma na viunga vyake hali ni tete na mambo yanabadilika kwa kasi kubwa. Ni wazi na ni dhahiri na mnajua kuwa waasi wa M23 na wanajeshi wa Rwanda wanaendelea kusonga mbele.”
Amesema mapigano hayo ni M23 upande mmoja na upande mwingine ni jeshi la serikali, FARDC wakiungwa mkono na kundi la Wazalendo.
Vifo vya walinda amani wa MONUSCO na SAMIDRC
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu chini ya ujumbe wa Umoja huo nchini DRC, MONUSCO wameendelea na doria ambapo Bwana Lacroix ametumia kikao hicho kuthibitisha vifo vya walinda amani watatu wa MONUSCO; mmoja kutoka Uruguay na wawili kutoka Afrika Kusini.
Ametuma salamu za rambirambi kwa serikali za Uruguay na Afrika Kusini pamoja na familia za walinda amani hao waliouawa huku akitakia ahueni ya haraka walinda amani wengine 12 waliojeruhiwa wakati wa makabiliano na waasi wa M23.
Ametaja pia SAMIDRC ambao ni ujumbe wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC nchini DRC, umepata madhara kwani baadhi ya wanajeshi wake wameuawa na wengine wamejeruhiwa.
Sitisho la mapigano haraka
Bwana Lacroix amesema kwa kuzingatia hali ya sasa, jambo muhimu ni sitisho la mapigano haraka iwezekanavyo ili kulinda raia ambao tayari mamia kwa maelfu tayari wamefurushwa Goma.
Tangu Jumamosi MONUSCO ilianza kuhamisha kwa muda kutoka Goma, wafanyakazi na familia zao, na kazi hiyo inaendelea kwa njia ya barabara na anga. Usalama wa watumishi wake ni kipaumbele.
MONUSCO inaendelea na jukumu la kulinda raia na wapiganaji waliojisalimisha kwa kadri ya uwezo wake kwa mujibu wa sheria za kibinadamu.
Ametamatisha mkutano wake akisema kuwa Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi za kikanda za kuleta amani DRC na hivyo “inakaribisha la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kuwa na mkutano wa viongozi tarehe 28 mwezi huu wa Januari, halikadhalika kikao cha Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika (AU) ambacho pia kinafanyika kesho Januari 28.”
Bwana Lacroix amesema wanategemea pia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuendelea kupatia kipaumbele suala la DRC.
Makombora yameangukia hospitali ya wazazi - OCHA
Bruno Lemarquis ambaye ni Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu na pia Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC amezungumza pian a wanahabari kutokea Kinshasa, mji mkuu wa taifa hilo la Maziwa Makuu na kusema kuwa hali ya kibinadamu Goma inatisha.
“Mapigano yamesambaa katika maeneo yote ya Goma, mji wenye watu milioni moja. Tayari watu 300,000 wamekimbia mji huo na hata kambi za wakimbizi wa ndani zimesalia tupu kwani watu wanaokimbia mapigano,” amesema Lemarquis ambaye pia ni Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini DRC.
Mjamzito na mtoto mchanga wameuawa
Akielezea zaidi kuhusu mashambulizi amesema, “asubuhi hii makombora mazito yalielekezwa katikati ya jiji la Goma. Mathalani kombora moja liliangukia kwenye hospitali wazazi ya Goma na kuua na kujeruhi raia akiwemo mama mjamzito na mtoto mchanga.”
Hospitali zimezidiwa uwezo kwani zinahaha kutibu majeruhi. Hospitali Kuu ya Ndosho imezidiwa uwezo wake kwani wiki iliyopita ilipokea majeruhi 259 wakiwemo raia 90, na leo Jumatatu Kamati ya Kimataifa Msalaba Mwekundu, (ICRC) inaripoti kupokelewa kwa majeruhi wengine 117, wengi wao wakiwa na majeruhi makubwa.
Kama hiyo haitoshi, amesema huduma za msingi kama vile maji na umeme zinapatikana kwa shida, huku huduma ya intaneti akisema ilikatwa saa saba mchana.
Kwa mujibu wa Lemarquis, DRC ina wakimbizi wa ndani milioni 6.5 ambapo theluthi moja ni katika jimbo la Kivu Kaskazini pekee, ambao sasa wamelazimika kukimbia tena kutokana na mapigano ya sasa.