Baraza la Usalama lakutana kujadili hali ya Goma, DRC
Baraza la Usalama lakutana kujadili hali ya Goma, DRC
Amani na Usalama
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana asuhuhi hii katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kujadili kuzorota kwa hali ya usalama katika mji wa Goma na viunga vyake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mgogoro huu kati ya wapiganaji wa M23 dhidi ya jeshi la DRC, FRDC, mashariki mwa DRC, ambao umesababisha mamilioni ya watu kuhama makazi yao na kuvuruga utulivu wa kikanda, umefikia viwango vya hatari, na kusababisha miito ya hatua za haraka. Wanadiplomasia na wataalam wanaonya kuwa kushindwa kuchukua hatua za dhati kunaweza kuongeza mateso na kuhatarisha zaidi utulivu wa nchi jirani.
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN: 'Tumenaswa'
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita, amehutubia Baraza la Usalama kuhusu yanayoendelea, wakati kundi lisilo la kiserikali la M23 likisonga mbele katika miji ya mashariki huku kukiwa na ripoti za vifo na majeruhi wa raia na walinda amani.
“Leo, licha ya msaada unaoendelea wa MONUSCO kwa FARDC, vikosi vya M23 na Rwanda vimepenya katika eneo la Munigi pembezoni mwa mji wa Goma, na kusababisha hofu kubwa na wakazi kukimbia,” amesema.
Barabara zimefungwa, na uwanja wa ndege hauwezi tena kutumika kwa shughuli za uokoaji au misaada ya kibinadamu. M23 imetangaza kuwa uwanja wa ndege wa Goma “umefungwa” na kutoa madai ya uongo kwamba FARDC imetumia uwanja huo kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya raia.
“Tumenaswa,” amesema.
“Ninatoa wito kwa Baraza hili kuchukua hatua sasa ili kulinda raia, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, na wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa,” amesema.
Naibu Mkuu wa Misaada: Mgogoro Unahitaji Hatua za Haraka
Joyce Msuya, Naibu Mkuu wa ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa,OCHA, ameliarifu Baraza kuhusu hali ya kibinadamu ilivyo.
Zaidi ya watu milioni 21 wanahitaji msaada kote nchini, amesema. Katika Kivu Kaskazini na Kusini, mamia ya raia wameuawa, na maelfu kwa maelfu wamekimbia makazi yao. Hospitali za Goma zimeelemewa, na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu ni mgumu.
Amehimiza pande zote kuepuka kutumia mabomu na silaha nzito katika maeneo yenye watu wengi na kuheshimu sheria zinazolinda raia.
“Pande zote lazima zichukue tahadhari ya kulinda raia na mali zao,” amesisitiza.
Ili kushughulikia mgogoro wa kibinadamu unaozidi kuwa mbaya, ameomba Baraza litumie ushawishi wake kuhakikisha pande zinaheshimu sheria za kimataifa na kulinda raia pamoja na miundombinu inayohusiana.
Pia ameomba ufadhili wa kutosha kusaidia juhudi za kibinadamu. Hadi sasa, dola milioni 17 zimeelekezwa kwenye mipango ya kuokoa maisha, lakini zaidi zinahitajika.
Aidha, amewataka wanachama wa Baraza kutumia ushawishi wao kumaliza mgogoro huo. “Kiwango cha mateso katika DR Congo kinahitaji umakini wa haraka,” amesema. “Maisha ya wanawake na watoto hayawezi kuendelea kupuuzwa.”
Endelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hili linaloendelea wakati viongozi wa dunia wakijaribu kutafuta suluhisho la mgogoro huu mgumu.