Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Goma: Katibu Mkuu UN atoa neno huku Mratibu wa masuala ya kibinadamu akizikumbusha pande zinazopigana

Gari la kivita UN lenye mwanajeshi ndani ya mnara linafanya doria ya usiku katika barabara moja huko Goma, DRC.
MONUSCO/Kevin N. Jordan Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakishika doria katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. (Maktaba)

Goma: Katibu Mkuu UN atoa neno huku Mratibu wa masuala ya kibinadamu akizikumbusha pande zinazopigana

Amani na Usalama

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asubuhi hii ya Jumapili tarehe 26 Januari kwa saa za New York, Marekani ametoa taarifa kueleza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na anarudia tena kulaani vikali mashambulizi ya kundi la M23 na maendeleo yake kuelekea Goma katika mkoa wa Kivu Kaskazini kwa msaada wa Vikosi vya Ulinzi vya Rwanda.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba katika saa 48 zilizopita, walinda amani wawili wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini DRC, MONUSCO kutoka Afrika Kusini na mmoja kutoka Uruguay wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu walilopewa na Baraza la Usalama. Walinda amani kumi na moja wamejeruhiwa na wanatibiwa katika hospitali ya Umoja wa Mataifa huko Goma.
 
“Katibu Mkuu anatoa salamu za rambirambi zake za dhati kwa familia za walinda amani waliopoteza maisha, pamoja na serikali na watu wa Afrika Kusini na Uruguay, na anawatakia walioumia kupona haraka. Anatoa heshima kwa ujasiri wa walinda amani wote wa Umoja wa Mataifa wanapotekeleza jukumu lao la kulinda raia na kuwalinda dhidi ya vurugu za makundi ya silaha, kwa kushirikiana na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) na Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SAMIDRC).” Imeeleza taarifa hiyo.
 
Katibu Mkuu anakumbusha pande zote zinazohusika na mzozo wajibu wao chini ya sheria za kibinadamu za kimataifa. Anakumbusha kuwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita. Anatoa wito kwa mamlaka husika kuchunguza tukio hili na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika haraka.
 
Aidha Katibu Mkuu Guterres amerudia wito wake wa kuheshimu makubaliano ya usitishaji mapigano. Anatoa wito kwa M23 kusitisha mara moja vitendo vyote vya uhasama na kuondoka katika maeneo waliyochukua. Aidha, anatoa wito kwa Vikosi vya Ulinzi vya Rwanda kusitisha msaada wao kwa M23 na kuondoka kwenye ardhi ya DRC. Anathibitisha tena msaada wa Umoja wa Mataifa kwa mchakato wa Luanda na kutoa wito wa kuanza mara moja kwa mazungumzo katika mfumo huo.
OCHA
 
Naye Mratibu wa Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,DRC, Bruno Lemarquis, ameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mapigano karibu na mji wa Goma na athari zake zinazoongezeka kwa raia imeeleza taarifa iliyotolewa na ofisi yake,  OCHA-RDC leo Januari 26 jijini Kinshasa, DRC.
 
Taarifa hiyo imeeleza kuwa tangu mashambulizi mapya ya M23 karibu na Goma tarehe 23 Januari 2025, mamia ya maelfu ya watu wamelazimika tena kukimbia kutoka maeneo mbalimbali ya mapigano, huku uwezo wa mapokezi na msaada ukiwa tayari umejaa. Maeneo kadhaa ya kuhifadhi wakimbizi katika pembezoni mwa Goma, ambayo yalikuwa na zaidi ya watu 300,000, yamekuwa matupu ndani ya masaa machache.
 
Wahudumu wa kibinadamu, wakiwemo wafanyakazi muhimu ambao bado wanaendelea kufanya kazi Goma, wanajitahidi kukidhi mahitaji ya raia walio hatarini zaidi licha ya kuzorota kwa usalama katika maeneo ya kuhifadhi wakimbizi na baadhi ya vitongoji vya mji huo.
 
Ukosefu wa usalama kutokana na mapigano karibu na maeneo yenye watu wengi na matumizi ya silaha nzito yanaweka raia katika hatari isiyokubalika. Hospitali za Goma zimezidiwa uwezo wa kutoa huduma za dharura, licha ya msaada kutoka kwa mashirika ya kibinadamu kama ICRC na MSF.
 
Hadi tarehe 24 Januari 2025, Hospitali Kuu ya Ndosho mjini Goma ilikuwa ikiwahudumia wagonjwa 256 walioumia, wakiwemo raia 90, wengi wakiwa na majeraha makubwa kutokana na risasi na mashambulizi ya mizinga. Hii inazidi uwezo wa vitanda 146 vya hospitali hiyo, hata baada ya msaada wa wahisani wa kibinadamu.
 
“Kwa niaba ya jumuiya ya kibinadamu nchini Congo, ninatoa wito kwa pande zote katika mgogoro kusitisha mara moja ongezeko la mapigano. Vurugu hizi zinaongeza mateso ya watu mashariki mwa Kongo na kuzidisha hali mbaya ya raia. Kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alivyosisitiza tarehe 23 Januari 2025, utulivu wa haraka unahitajika.” Amesema Lemarquis.
Kiongozi huyo ameoneza akisema Jumuiya ya kibinadamu inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za kukabiliana na hali hii mbaya ya kibinadamu na usalama. Huku tukisubiri kusitishwa kwa mapigano, tunatoa wito wa kuwepo mapumziko ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika zaidi ili kuruhusu uokoaji wa majeruhi na raia kutoka maeneo ya mapigano.
 
Aidha kwa niaba ya jumuiya ya kibinadamu, amezikumbusha pande zote zinazohusika katika mapigano kuhusu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu: raia na miundombinu ya kiraia haipaswi kulengwa kamwe.
 
“Pande zote zinapaswa kuhakikisha upatikanaji wa msaada wa kibinadamu bila vizuizi kwa wote wanaohitaji na kuhakikisha usalama wa raia wanaokimbia maeneo ya mapigano. Raia wanapaswa kupata msaada wa kibinadamu kwa usalama na kwa heshima. Hii inahitaji wahudumu wa kibinadamu kubaki karibu iwezekanavyo na watu walioathirika katika hali zinazowezesha utoaji wa msaada unaookoa maisha.” Amesema.
 
Amehitimisha akitoa wito kuwa pia, ni muhimu kuruhusu kurejeshwa kwa huduma za msingi katika mji wa Goma, ikiwa ni pamoja na maji, umeme, na huduma za afya, ili kukidhi mahitaji ya msingi ya watu walioathirika na mgogoro.