Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yatiwa hofu na hali ya usalama Mashariki mwa DRC baada ya M23 kutwaa Minova

Mvulana akienda kuchota maji katika kambi ya Minova ya wakimbizi wa ndani Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
OCHA/Eve Sabbagh Mvulana akienda kuchota maji katika kambi ya Minova ya wakimbizi wa ndani Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

MONUSCO yatiwa hofu na hali ya usalama Mashariki mwa DRC baada ya M23 kutwaa Minova

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, umethibitisha kuwa waasi wa M23 wametwaa baadhi ya maeneo jimboni Kivu Kusini, miongoni mwao ikiwa mji wa Minova, ikisema hali hiyo inatia wasiwasi mkubwa.

Msemaji wa MONUSCO Ndèye Khady Lo amethibitisha hayo kwenye mahojiano yake kwa njia ya simu na Idhaa ya Kifaransa ya Umoja wa Mataifa kutokea, Kinshasa, mji mkuu wa DRC.

Bi. Ndèye amesema MONUSCO ina wasiwasi mkubwa na kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama mashariki mwa DRC kwani M23 katika siku za karibuni imekuwa inazidi kuongeza miji inayoshikilia jimboni Kivu Kaskaizni, na kwamba, “tangu Januari 18, kundi hilo limetwaa maeneo mengine Kivu Kusini, na kusababisha vifo huku watu 250,000 wakifurushwa makwao. Kufuatia kuondoka kwa MONUSCO jimboni Kivu Kusini mwezi Juni mwaka 2024, walinda amani wa Umoja wa Mataifa hawako tena jimboni humo.”

Akifafanua maeneo hasa ambayo M23 wametwaa jimboni Kivu Kusini, Msemaji huyo wa MONUSCO amesema, “wanashikilia Minova kwenye bandari ya Kasunyu, bandari ambayo ni ya kimkakati kwa usafirishaji ziwani na pia uchimbaji wa madini.”

Mara ya kwanza mzozo wa sasa unaingia Kivu Kusini

Akielezea ni kwa vipi kutwaliwa kwa mji huo wenye bandari kutaleta madhara, Bi. Ndèye amesema, “hili ni jambo kubwa na linatia hofu kwa sababu ni mara ya kwanza mzozo huu wa sasa unasambaa hadi Kivu Kusini, jimbo ambalo ni jirani na Kivu Kaskazini. Minova ni mji ulio jirani na barabara muhimu sana ya usambazaji kuelekea Goma na Sake, iliyoko jimboni Kivu Kaskazini. Kutwaliwa kwake kunaweza kuathiri vibaya mamilioni ya watu wanaoishi Kivu Kaskazini, ambako tayari zaidi ya watu milioni 2.8 wamefurushwa, na wengi wao wanasaka hifadhi kwenye viunga vya Goma na Sake.”

Makazi ya wakimbizi wa ndani ya Lushagala Kivu Kaskazini nchini DRC
© UNHCR/Guerchom Ndebo Makazi ya wakimbizi wa ndani ya Lushagala Kivu Kaskazini nchini DRC

Kivu Kaskazini sasa inakabiliwa na shinikizo

Jimboni Kivu Kaskazini, kwa mujibu wa msemaji huyo, mapigano yanaendelea kati ya jeshi la serikali, FARDC na kundi la M23 na makundi mengine yaliyojihami hasa karibu na mji wa Sake.

Hata hivyo, amesema Operesheni Springbok, iliyozinduliwa mwezi Novemba mwaka 2023 kwa ushirikiano kati ya FARDC na MONUSCO inaendelea kuimarisha ulinzi kuelekea miji hiyo ya kimkakati ambayo ni Goma na Sake.

Mapigano ya Jumanne wiki hii huko Bweremana kijiji kilichoko Kivu Kaskazini yalisababisha vifo vya watu 10, na watu wengine kukimbilia mji wa Kalehe jimboni humo, lhali wengine kuelekea Goma na Rusayo jimboni Kivu Kaskazini.

MONUSCO iliondoka Kivu Kusini lakini mashirika ya UN yangaliko

Licha ya MONUSCO kuondoka Kivu Kusini kufuatia ombi la serikali la kutaka MONUSCO ianze kuondoka taratibu nchini humo, mashirika ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi bado yanaendelea kutoa huduma.

“Hata hivyo hayapati usaidizi wa ulinzi kutoka MONUSCO,” amesema Msemaji huyo akirejelea wito wake kwa M23 kusalimisha silaha na kuheshimu makubaliano ya sitisho la mapigano yaliyotiwa saini Agosti 4, 2024.

Halikadhalika amezitaka pande kinzani kwenye mzozo mashariki mwa DRC kurejelea ahadi yao kupitia mchakato wa Luanda wa kusongesha majadiliano kati ya DRC na Rwanda.