Ukosefu wa ushirikiano wa kimataifa unaiweka dunia rehani kwa majanga ya mabadiliko ya tabianchi na AI: Guterres
Ukosefu wa ushirikiano wa kimataifa unaiweka dunia rehani kwa majanga ya mabadiliko ya tabianchi na AI: Guterres
Masuala ya UM
Viongozi wa kimataifa wa masuala ya kisiasa na biashara wanaokutana Davos Uswisi kwa ajili ya jukwaa la kiuchumi duniani WEF, leo wamekabiliwa na ukweli mchungu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, akilaani ukosefu wa ushirikiano wa kimataifa katika dunia inayokosa mwelekeo, ikikabiliwa na hatari mbili kubwa ambazo ni mabadiliko ya tabianchi na akili mnemba au AI isiyodhibitiwa.
Akizungumza katika Jukwaa hilo la kila mwaka la Kiuchumi Duniani Katibu Mkuu amewaonya viongozi wa dunia na wakuu wa biashara kuhusu vitisho viwili vinavyoongezeka kwa ubinadamu mabadiliko ya tabianchi na akili mnemba au AI isiodhibitiwa amesema “Kunapokuja suala la tishio la kimataifa nyuklia sio tishio pekee. Leo hii tunakabiliwa na matishio mawili makubwa ambayo yanahitaji kupewa uziti Mkubwa wa kimataifa na hatua kwa sababu yanatishia kubadili kabisa maisha tunayoyajua, janga la mabadiliko ya tabianchi na upanuzi wa kasi wa wigo wa akili mnemba.”
Dunia yakosa mwelekeo, ushirikiano nao hakuna
Akikosoa ukosefu wa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto hizi kubwa, Guterres ametoa wito wa kuchukua hatua za pamoja haraka ili kushughulikia dunia aliyoiita dunia inayokosa mwelekeo “Hebu tukabili ukweli , leo hii watu wengi wanapoitazama dunia hawaoni ushirikiano mkubwa wala maarifa ya kutosha . Licha yah atua zilizopigwa uwekezaji katika nishati jadidifu , teknolojia na masuala ya kiafya ni dunia na matatizo yetu mengi yanazidi kuwa mbaya”
Bandari kuu ziko hatarini kutwamishwa na maji ya bahari
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Guterres amelinganisha uraibu wa dunia kwa nishati ya mafuta na mnyama wa Frankenstein, akisisitiza madhara yake makubwa.
Amebainisha kuwa baadhi ya bandari kuu za mafuta duniani ziko hatarini kutokana na viwango vya bahari kuongezeka, jambo linalosababishwa na uchomaji wa makaa ya mawe, mafuta, na gesi asilia.
Katibu Mkuu amekemea viwanda na taasisi za kifedha zinazosuasua kwenye ahadi zao za tabianchi, akisema hii ni kukosa maono na usaliti wa sayansi na watumiaji wanaotafuta uendelevu.
Akili mnemba (AI) ni sawa na upanga wa makali mawili
Akizungumzia hatari na fursa za AI, Guterres ameelezea kama upanga wa makali mawili. Ingawa inatoa matumaini katika kubadilisha sekta za afya, kilimo, na elimu, ameonya kuhusu hatari kubwa ikiwa haitadhibitiwa.
Amesema AI isiyodhibitiwa inaweza kuvuruga uchumi, kudhoofisha imani kwa taasisi, na kuongeza ukosefu wa usawa.
Guterres amehitimisha kwa kutoa wito wa mshikamano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto hizi muhimu akisema “kubadili mwelekeo wa taasisi kunahitaji kubadili fikra kwa sababu tunakabiliwa na changamoto kubwa zinazoweza kuiangamiza dunia na sishawishiki kwamba viongozi wanalielewa hili.”
Amesisitiza umuhimu wa kurekebisha mifumo ya utawala wa kimataifa ili kukabiliana ipasavyo na migogoro ya kisasa, akionya kuwa utashi wa kisiasa ni muhimu lakini bado haupo katika kiwango cha kutosha.
Ujumbe wake ni bayana kwamba sasa ni wakati wa kuchukua hatua za pamoja na za haraka.