Misaada inaendelea kumiminika Gaza lakini mahitaji bado ni makubwa: OCHA/ WHO
Misaada inaendelea kumiminika Gaza lakini mahitaji bado ni makubwa: OCHA/ WHO
Misaada ya kibinadamu imeanza kuingia Gaza kwa kiwango kikubwa kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyowezesha kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Palestina, huku familia zikirejea pamoja.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa bado kuna mahitaji makubwa katika eneo hilo lililoathirika vibaya, yamesema leo Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu.
Ikiwa ni siku ya tatu tangu kusitishwa kwa mapigano, yaliyotangazwa kuanza Jumapili, Januari 19, ofisi ya Umoja wa Mataifa kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA imekaribisha ongezeko kubwa la msaada wa kibinadamu unaoingia Gaza, baada ya miezi 15 ya mashambulizi makali ya Israel.
Malori ya misaada yalianza kuingia Gaza “dakika chache baada ya makubaliano kuanza kutekelezwa Jumapili,” amesema msemaji wa OCHA, Jens Laerke.
Ameongeza kuwa “Hadi sasa katika siku hizi mbili za kwanza hakuna ripoti za uporaji au mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada.”
Mamia ya malori ya misaada yaingia Gaza
Zaidi ya malori 900 ya misaada yaliingia Ukanda wa Gaza Jumatatu, huku makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas yakiheshimiwa, kulingana na mamlaka za Israel na wadhamini wa makubaliano hayo, amba oni Marekani, Qatar, na Misri.
Wakati vita vilipokuwa vikiendelea, vilivyoanzishwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, 2023, usafirishaji wa misaada kwenda Gaza ulipungua hadi malori 50 kwa siku.
“Hatimaye, misaada kwa kiwango kikubwa inaingia,” amesema Bwana. Laerke akiongeza kuwa “Hatimaye, mateka zaidi wameachiliwa na wanaweza kuungana na familia zao, na hatimaye, wanawake na watoto waliokuwa kizuizini wameachwa huru. Huu ni mwangaza mkubwa wa matumaini, dhaifu lakini muhimu, makubaliano haya lazima yadumu.”
Kukabiliana na majeraha ya kimwili na kiakili
Vipaumbele vya haraka kwa wakazi wa Gaza ni pamoja na “kupata chakula, kufungua maduka ya mikate, kupata huduma za afya, kuimarisha hospitali, kukarabati mitandao ya maji, kukarabati makazi, na kuunganisha familia,” amesema msemaji huyo wa OCHA mjini Geneva.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameeleza kwa muda mrefu kuwa watu wote wa Gaza zaidi ya milioni mbili wanategemea mahitaji haya muhimu.
Watoto, ambao ni takriban nusu ya idadi ya watu katika ukanda huo, “wanategemea mlo mmoja tu kwa siku,” OCHA imesema katika taarifa yake.
“Lazima na tutafanya hivyo kuongeza usambazaji wa misaada kupitia fursa hii. Njaa imeenea, watu hawana makazi, magonjwa na majeraha ni mengi. Watoto wametenganishwa na familia zao na kuna wingu kubwa la msongo wa kiakili unaoikumba Gaza, ambalo linahitaji kushughulikiwa.”
Dharura ya afya inaendelea
Kwa mujibu wa shirika la Afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, mahitaji ya haraka ya afya yanapaswa kushughulikiwa haraka katika Ukanda wa Gaza, ambako nusu ya hospitali hazifanyi kazi, nyingine zinafanya kazi kwa sehemu tu, na sehemu kubwa ya vituo vya afya vimeharibiwa.
“Lengo ni kujaribu kutoa huduma za afya haraka iwezekanavyo kwa watu wa Gaza, kwa kuzingatia huduma za dharura, afya ya uzazi na watoto, pamoja na maeneo mengine,” amesema msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic.
Ameongeza kuwa “Tusiwasahau wengine, kuna wagonjwa 12,000 ambao bado wanahitaji kuhamishwa kutoka Gaza ili kupata matibabu wanayohitaji. Tunahitaji kuhakikisha kwamba watu hawa wanaweza kwenda na kupokea matibabu.”
Ameendelea kusema kuwa “Tumekuwa tukizungumza juu ya watu 25,000 waliopata majeraha yanayobadilisha maisha. Watu hawa wanahitaji huduma za ukarabati ambazo hazipatikani kwa sasa.”