Urithi wa Lulu Bahrain: Harakati za kufufua utamaduni wa enzi enzi
Urithi wa Lulu Bahrain: Harakati za kufufua utamaduni wa enzi enzi
Bahrain imekuwa ikihusishwa kwa muda mrefu na lulu, maji yake yenye kina kifupi na maeneo tajiri ya chaza yamekuwa msingi wa uchumi wa kisiwa hicho kwa maelfu ya miaka. Kamusi ya Kiingereza ya Oxford inafafanua uvuvi wa lulu kama shughuli au kazi ya kuzamia au kuvua chaza wa lulu.
Urithi wa lulu wa taifa hili la Ghuba siyo tu sehemu ya historia yake – ni sehemu muhimu ya asili yake ya kitamaduni, kulingana na Mohamed Alslaise, mzamiaji wa lulu na mtafiti wa Taasisi ya Bahrain ya Lulu na Vito (DANAT).
“Ninasema mara zote hivi: wabahraini wote wana stadi ya uzamiaji lulu katika damu yao. Karibu familia zote zilizohamia kutoka Ghuba ya Kiarabu na pwani ya Iran kwenda Bahrain zilikuwa na wazamiaji,” Bwana Alslaise amewaeleza wanahabari wa Umoja wa Mataifa waliokuwa Manama, mji mkuu wa Bahrain na mji mkubwa zaidi.
Bwana Alslaise, ambaye ana shauku kubwa ya kuhifadhi na kufufua desturi hii ya kale, anasema kuwa familia nyingi nchini Bahrain zina mtu ambaye alikuwa mzamiaji wa lulu au alihusika katika sekta ya uvuvi wa lulu.
Lulu katika ghuba ya uajemi
Uvuvi wa lulu katika Ghuba ya Uajemi uliunda uchumi wa Bahrain kwa maelfu ya miaka. Ugunduzi wa lulu zitokanazo na chaza wa kufugwa nchini Japani katika miaka ya 1930 ulisababisha kuporomoka kwa kasi na kuvuruga sekta ya lulu, ambayo ilifikia kilele chake mwanzoni mwa karne ya 20.
Lulu Kama sehemu ya utamaduni wa Bahrain
“Tamaduni nyingi za Bahrain zimeunganishwa na sekta ya uvuvi wa lulu. Kwa mfano, nyimbo za kuzamia lulu,” anasema Bwana Alslaise. “Simulizi za lulu zimepitishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Bado tunaimba nyimbo zile zile, ambazo ziliimbwa awali kuinua morali kwenye boti.”
Adnan Ali Zuweid, ambaye amekuwa akizamia kwa miongo lakini alistaafu miaka mitatu iliyopita, anasema, “Kazi ya kuzamia lulu, mbali na kuwa njia ya maisha, pia ni yenye manufaa kwa mwili. Kuna maeneo maalum ya kuzamia huko Bahrain. Hapo awali, mababu zetu walizamia wakati maalum wa siku na mwaka, kawaida kati ya Aprili na Julai. Sasa, tunazamia wakati wowote wa mwaka kwa sababu ya maendeleo katika mbinu za utafutaji. Tunapenda kazi hii, na watoto wetu wataendelea nayo.”
Njia ya Lulu ya Bahrain
Eneo la kihistoria la lulu ya Bahrain, inayojulikana kama Njia ya Lulu, imetajwa kuwa eneo la Urithi wa dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Njia hii hii inashuhudia urithi wa lulu na utajiri ulioundwa katika eneo la Ghuba kwa maelfu ya miaka.
Kwa mujibu wa UNESCO, eneo hilo lina majengo 17 katika mji wa Murharraq, takribani dakika 40 kutoka mji mkuu Manama. Maeneo matatu ya chaza baharini, sehemu ya ufukwe, na ngome ya Qal’at Bu Mahir kwenye ncha ya kusini ya Kisiwa cha Muharraq, ambako boti zilianza safari za kuelekea maeneo ya chaza.
Eneo hilo pia lina duka, maghala, msikiti, na nyumba za wafanyabiashara tajiri. Kwa mujibu wa UNESCO, sehemu hiyo ni mfano kamili wa utamaduni wa lulu na utajiri uliotokana na sekta hiyo wakati uchumi wa Ghuba ulipotawaliwa na biashara kuanzia karne ya pili hadi Japani ilipoanzisha lulu za kilimo.
Kufufua uvuvi wa chaza wa lulu
Kulingana na Bwana Alslaise, tangu mwaka 2017 mamlaka za Bahrain zilipoanzisha leseni za kuzamia lulu, watu wengi waliokuwa hawajui chochote kuhusu uvuvi wa lulu wameanza kujifunza.
“Sasa, miaka saba baadaye, Wabahraini wengi wameungana tena na urithi huu. Tulianzisha mfumo mpya wa kuzamia. Hata mbinu zetu za kuzamia na kuuza lulu zimebadilika. Mfumo huu mpya, ulioundwa na kizazi kipya, umewaleta Wabahraini wengi katika sekta ya lulu. Zaidi ya wazamiaji 1,000 sasa wamesajiliwa na huzamia mara kwa mara kujipatia kipato.”
Kutwama kwa lulu kwatwamisha ujenzi wa boti
Kuporomoka kwa sekta ya lulu pia kumeathiri sekta ya ujenzi wa meli ya Bahrain. Abdulla, mbunifu wa meli za mbao kwa zaidi ya miaka 35, anasema, “Bahrain inajulikana kwa sekta ya ujenzi wa meli, ambayo ilikuwa sehemu muhimu ya uvuvi wa lulu. Kuna aina mbalimbali za meli, kulingana na muundo, lakini sasa meli ndogo ndogo zinatumika kwa uvuvi wa lulu kutokana na kupungua kwa mahitaji.”
Teknolojia na uendelevu
Bwana Alslaise anakubali wasiwasi kuhusu vizazi vipya kuharibu maeneo ya chaza kwa kutumia teknolojia ya kisasa kama vile vifaa vya kupiga mbizi vya scuba, lakini anasema, “Scuba inakuzuia kwa muda fulani – unaruhusiwa kuzama mara tatu tu kwa siku kutokana na hatari za ugonjwa wa kupungukiwa na shinikizo la damu.”
Akiwa na matumaini kuhusu siku zijazo, anahitimisha, “Mungu akinipa afya, nitaendelea kuzamia lulu. Ni kazi inayoridhisha sana.”