Mashariki ya Kati inapitia mabadiliko makubwa ni lazima watu wake wanaibuke kwa amani na utu: Guterres
Mashariki ya Kati inapitia mabadiliko makubwa ni lazima watu wake wanaibuke kwa amani na utu: Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema Mashariki ya Kati inakabiliwa na mabadiliko makubwa yaliyojaa hali ya sintofahamu, lakini pia matumaini, na akasisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa inapaswa kutumia kila juhudi kusaidia kuunda mabadiliko haya kwa misingi ya haki zaidi, utu, haki za binadamu, na amani kwa watu wote wa eneo hilo.
Akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hii leo mjini New York Marekani Bwana Guterres amesema eneo hilo linabadilika na haijulikani matokeo yake yatakuwa nini.
"Tunawajibika kusaidia kuhakikisha kwamba watu wa Mashariki ya Kati wanatoka katika kipindi hiki cha misukosuko wakiwa na amani, utu, na matarajio ya matumaini yanayojengwa kwenye hatua za vitendo."
Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unafanyika chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ahmed Attaf, ambaye nchi yake inashikilia uenyekiti wa Baraza hilo mwezi huu. Jumla ya maafisa na wajumbe 69 wanatarajiwa kuhutubia mkutano huo.
Ukurasa mpya kwa Lebanon
Guterres amesisitiza kwamba "alfajiri mpya inachomoza nchini Lebanon, akitumaini kwamba serikali itaundwa hivi karibuni ambamo Walebanon wote watahisi wanawakilishwa, na serikali yenye uwezo wa kuhakikisha usalama kwa raia wake wote."
Katibu Mkuu ndio kwanza amerejea kutoka Lebanon ambako alishuhudia mwenyewe "athari za kibinadamu za kusikitisha na uharibifu uliosababishwa na mzozo kusini mwa nchihiyo”. Ameongeza kuwa Waisraeli pia walikuwa waathirika na walipata hasara na kuhama makazi, na ameeleza matumaini kwamba kila mtu katika pande zote mbili angeweza kurudi kwenye maeneo yao ya makazi hivi karibuni, akisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa utafanya kila iwezalo kupunguza mateso na kusaidia urejeshaji wa hali ya kawaida.
Bwana Guterres amesema usitishaji mapigano nchini humo ni dhaifu, lakini bado kunashikiliwa.
Amesisitiza umuhimu wa kumaliza hali ya uwepo wa Israeli kusini mwa nchi hiyo, kama ilivyoainishwa katika makubaliano, na "kwa Jeshi la Lebanon kuwepo katika maeneo yote ya Lebanon mchakato ambao tayari umeanza kusini kwa msaada wa UNIFIL.”
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo "wanahitaji kuimarisha uwezo ikiwa ni pamoja na usafishaji wa mabomu na kuondoa vilipuzi ambavyo havijalipuka pamoja na kuboresha utekelezaji wa majukumu yao kulingana na mamlaka yao."
Azimio la Baraza la Usalama 1701 linasema wazi kwamba eneo kati ya Mstari wa Bluu na Mto Litani lazima liwe huru dhidi ya wafanyakazi wowote wa kijeshi, mali za kijeshi na silaha isipokuwa zile za Serikali ya Lebanon na UNIFIL, na liliwataka wahusika kutekeleza azimio hilo kikamilifu.
Tishio la msingi kwa Palestina
Bwana Guterres amesema makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza yalitoa "mwangaza wa matumaini licha ya changamoto nyingi”. Umoja wa Mataifa unafanya sehemu yake kuhakikisha upanuzi wa haraka wa shughuli za kibinadamu amesema, akibainisha kwamba zaidi ya malori 630 ya misaada ya kibinadamu yaliingia Ukanda wa Gaza jana, yakiwemo angalau 300 kuelekea kaskazini.
Katibu Mkuu amewasihi wahusika kuhakikisha kwamba makubaliano haya yanaongoza kwenye kuachiliwa kwa mateka wote na kusitisha mapigano kwa kudumu Gaza, akiongeza kuwa hii inapaswa kutafsiriwa kuwa angalau hatua nne zinazoendelea:
- Mosi mashirika ya Umoja wa Mataifa "ikiwa ni pamoja na mhimili wa hatua zetu ya kibinadamu, UNRWA" lazima yaweze kufanya kazi bila vikwazo.
- Pili upanuzi wa utoaji wa misaada ya msingi na huduma unahitaji hali salama na mazingira mazuri ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuruhusu vifaa vya kinga na mawasiliano na kurejesha utulivu wa umma.
- Tatu, watu lazima wapate misaada ya kuokoa maisha na pia bidhaa za kibiashara kuruhusiwa kuingia Gaza.
- Na nne Raia lazima walindwe, na wale wanaotaka kurudi kwenye jamii zao lazima wawe na njia salama ya kufanya hivyo.
Bwana Guterres pia amegusia suala la utawala na usalama katika Ukanda wa Gaza, akisisitiza kwamba Mamlaka ya Palestina imeonyesha utayari wa kuchukua jukumu na majukumu yake huko Gaza.
Ameomba "msaada wa pamoja kwa ajili ya kuanzisha mipango itakayowezesha muungano wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutawala wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.”
Hata hivyo, alibainisha kuwa hali katika Ukingo wa Magharibi inaendelea kuzorota kutokana na mapigano, mashambulizi ya anga, upanuzi wa makazi haramu na ubomoaji wa nyumba. "Ninatiwa wasiwasi mkubwa na tishio la msingi kwa uadilifu na muunganiko wa eneo linalokaliwa la Palestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi."
Amesema idhini za makazi zimeongezeka na maafisa waandamizi wa Israeli wanazungumza hadharani kuhusu kuunganisha rasmi sehemu au yote ya Ukingo wa Magharibi katika miezi ijayo
Guterres amesisitiza kuwa "Kuunganishwa kwa aina yoyote kutakuwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Ni wazi kuwa utulivu mkubwa zaidi Mashariki ya Kati unahitaji hatua zisizoweza kupingika za kuelekea suluhisho la mataifa mawili."
Syria iko njia panda
Syria imekuwa kwa karne nyingi "njia panda ya ustaarabu na sasa iko katika njia panda ya historia" kufuatia kuanguka kwa utawala wa kikatili wa zamani, kulingana na Katibu Mkuu, ambaye amesema "Hatuwezi kuruhusu mwanga wa matumaini kubadilika kuwa jahanamu ya machafuko."
Guterres amekaribisha hatua zilizochukuliwa na nchi kuonyesha mshikamano na watu wa Syria, na akasema kazi muhimu zaidi ya kushughulikia vikwazo "haitaweza kuepukika, hasa kwa kuzingatia mahitaji ya kiuchumi ya dharura ya nchi hiyo. Kukuza mchakato jumuishi wa mpito wa kisiasa ni njia bora zaidi ya kuhakikisha kwamba Syria inapokea msaada zaidi.”
Mamlaka ya Palestina
Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje na Wapalestina wanaoishi ughaibuni, Farsin Aghabakian, amesema "Kuna mwangaza wa matumaini ambao sasa unaonekana, tunatumaini kwamba utaendelea na kufanikisha kusitishwa kabisa kwa mapigano na kuepusha kurudi kwa uchokozi, kuondolewa kabisa kwa vikosi vya uvamizi kutoka Ukanda wa Gaza, kuanzishwa kwa njia ya kisiasa kulingana na maazimio ya uhalali wa kimataifa yanayolenga kumaliza uvamizi, na utekelezaji wa maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki kulingana na azimio la Baraza Kuu linalotaka uvamizi uishe ndani ya mwaka mmoja."
Ametoa wito wa utekelezaji wa maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, yakiwemo Azimio la Baraza la Usalama namba 2735.
Amesisitiza kwamba Ukanda wa Gaza ni sehemu isiyoweza kutenganishwa ya eneo la Palestina lililokaliwa, na kwamba Nchi ya Palestina ina mamlaka ya kisheria na kisiasa juu ya Ukanda wa Gaza na maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa tangu 1967, pamoja na Jerusalem Mashariki, akirudia kukataa kwake kabisa "jaribio lolote la kuchukua sehemu za ardhi yetu au kuwafukuza watu wetu."
Waziri huyo wa Palestin ameongeza kuwa "Tunathibitisha kwamba serikali ya Palestina iko tayari kuchukua jukumu la usimamizi wa Ukanda wa Gaza pamoja na Ukingo wa Magharibi, kwa kushirikiana na nchi na mashirika rafiki, ikiwa ni pamoja na kurudisha utoaji wa huduma za msingi za afya na elimu, maji na umeme, na kuhakikisha kurudi kwa watu waliokimbia kwenye nyumba zao na kujiandaa kwa awamu ya ujenzi upya".
Amethibitisha dhamira yao ya kusimamia mipaka kwa kushirikiana na Muungano wa Ulaya na Misri kulingana na makubaliano ya 2005, na kupongeza msaada wowote katika mafunzo na vifaa kwa polisi na vikosi vya usalama vya Palestina.
Amesema wanatarajia kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kwa ajili ya utekelezaji wa maazimio ya uhalali wa kimataifa yanayohusiana na suala la Palestina na suluhu ya mataifa mawili, ambao utafanyika Juni huko New York, akiongeza kuwa "Tunatoa wito kwa nchi zote zitakazoshiriki kuchukua hatua za kivitendo na za uamuzi kumaliza uvamizi, kuunga mkono uhuru wa nchi ya Palestina na kufanikisha amani ya haki."
Kauli ya Israeli
Reut Shabbir Ben-Naftali, mratibu wa masuala ya kisiasa katika ujumbe wa kudumu wa Israeli kwenye Umoja wa Mataifa, amesema mateka waliokuwa wakishikiliwa Gaza walikumbana na "mateso yasiyoweza kuelezek kwa siku 472, wakiwemo wanawake watatu walioachiliwa jana, ambao "wanaonyesha nguvu na uthabiti wa watu wa Israeli, na wanawakilisha alama za ujasiri wa milele mbele ya ukatili usioweza kuelezeka."
Ben-Naftali amesema Baraza la Usalama lazima likabiliane na "hali halisi isiyofurahisha kwamba kushindwa kwake kuwawajibisha Hamas kunaweka mfano hatari na ni ishara kwa dunia kwamba mashirika ya kigaidi yanaweza kufanya kazi bila adhabu na kutumia maisha ya watu wasio na hatia kama turufu, bila hofu ya matokeo makubwa."
Ameongeza kuwa vitendo vya Israeli vimebadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kimkakati ya Mashariki ya Kati. "Hatutaacha mpaka vitisho vya Hamas vimeondolewa kabisa, na kamwe hatutasahau gharama iliyolipwa na watu wasio na hatia," amesema.
Mtazamo wa Algeria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ahmed Attaf, amesema kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza yalikuwa "yamechelewa sana katika muktadha wa utekelezaji wa mradi wa Israeli huko Gaza hasa na katika eneo zima kwa ujumla.”
Amwsema Gaza siyo tena ilivyokuwa baada ya kuathiriwa na "uhalifu uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 46,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu yake na uwezo wake wote.”
Ameongeza "Iwapo Baraza hili hapo awali lilishindwa kutendea haki watu wa Palestina na kutambua haki zao, halipaswi kupoteza fursa hii ya kihistoria leo kubeba jukumu lake lote lililopewa na Katiba ya Shirika letu."
Amebainisha kuwa jukumu hili siyo tu kushughulikia athari za "uvamizi ambao Gaza imekumbana nao," bali linakwenda mbali zaidi kushughulikia kiini cha mgogoro, ambacho ni kutekeleza mradi wa kitaifa wa Palestina.
"Mkataba wa kusitisha mapigano siyo mwisho wa safari, bali ni hatua ya kuanzia, na ni fursa ambayo mafanikio au kushindwa kwake kunategemea jinsi inavyotumika na kujengwa juu yake," ameongeza waziri wa Algeria.
Ametaka Baraza la Usalama kulenga juhudi zake katika hatua tatu kuu:
- Kuthibitisha mkataba wa kusitisha mapigano na kufuatilia utekelezaji wake.
- Kuhakikisha kwamba "mipango ya siku zijazo katika Ukanda wa Gaza" inazingatia matakwa ya Wapalestina, kuimarisha makubaliano yao, na kulinda matarajio yao ya kusonga mbele katika utekelezaji wa mradi wao wa kitaifa.
- Kujenga juu ya mkataba wa kusitisha mapigano kwa kuzindua mchakato wa kisiasa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa unaolenga kutatua mgogoro wa Palestina na Israeli.
Isemavyo Marekani
Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Dorothy Shea, amesema kuwa mgogoro wa Gaza ulipaswa kumalizika muda mrefu uliopita, akisisitiza kwamba "hatupaswi kamwe kusahau maisha yaliyopotea kutokana na shambulio la kigaidi la Hamas la Oktoba 7, na ukatili uliowakumba watu wasio na hatia katika vita vilivyofuata."
Amesema kundi hilo halipaswi kuruhusiwa kutawala siasa za Gaza "na kuendelea kucheza nafasi ya mharibifu kwa niaba ya watu wa Palestina."
Ameendelea kusema kwamba Hamas "inatumia kwa hila mateso ya Wapalestina" kwa kutumia miundombinu ya raia kwa madhumuni ya kijeshi, huku "ikijifanya kuwa mwathirika" na kutoa ombi kwa jamii ya kimataifa kwa niaba ya Wapalestina na Gaza wakati ikiwahatarisha.
Shea amekaribisha kauli za hivi karibuni za uongozi wa Palestina, ambazo zilibainisha kuwa Hamas "inaweka maslahi ya Tehran juu ya maslahi ya watu wa Palestina na hivyo kusababisha uharibifu huko Gaza.”
Shea amesema vita ya Israeli ni dhidi ya Hamas, "siyo dhidi ya raia wa Palestina, ambao kundi la kigaidi linadai uwongo kuwakilisha."
Amesisitiza kuwa viongozi wa kanda hiyo watahitaji kufanya maamuzi magumu kusaidia kuunda "hali mpya katika siku za usoni,”akiongeza kuwa nchi yake itafanya kila iwezalo "kusaidia Waisraeli na Wapalestina kuchukua fursa hii pamoja na kupata amani kupitia makubaliano haya."