Baada ya Tanzania kuthibitisha mlipuko wa Marburg, WHO yaongeza usaidizi
Baada ya Tanzania kuthibitisha mlipuko wa Marburg, WHO yaongeza usaidizi
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema wanashirikiana na serikali ya Tanzania kudhibiti mlipuko wa homa ya Marbug iliyoripotiwa mkoani Kagera, kaskazini magharibi mwa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Dkt. Tedros amesema hayo leo huko Dodoma, mji mkuu wa Tanzania wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, mkutano ambao pia umehudhuriwa na Rais Samia.
Amesema Rais Samia amempatia taarifa mpya za uthibitisho hii leo kuhusu mlipuko wa homa ya Marburg baada ya uchunguzi kwenye maabara ya Taifa nchini humo.
Msaada wa WHO kudhibiti Marburg Tanzania
Dkt. Tedros amesema, naahidi WHO kuendelea kusaidia ili kudhibiti mlipuko huo. Tangu wagonjwa wa kwanza walioshukiwa kuwa na Marburg waliporipotiwa, Tanzania imeimarisha hatua kwa kuongeza kasi ya kubaini wagonjwa, kuweka vituo vya tiba na maabara tembezi kwa ajili ya kuchunguza sampuli, pia kupeleka timu ya kitaifa ya wahudumu wa afya.
Amepongeza jinsi Tanzania iliimarisha hatua za kudhibiti Marburg baada ya mlipuko wa kwanza mwezi Machi mwaka 2023 akisema uwekezaji wa serikali wakati wa mlipuko uliopita umejenga uwezo na ninatumai utawezesha Tanzania kudhibiti mlipuko wa sasa haraka iwezekanavyo.
Ili kusaidia hatua za Tanzania, Dkt. Tedros ametangaza kuwa WHO inaipatia nchi hiyo dola milioni tatu kutoka mfuko wa dharura wa shirika hilo, ikiwa ni nyongeza ya mchango wa awali wa dola 50,000 wa kusaidia uchunguzi.
Hadi sasa hakuna tiba au chanjo dhidi ya homa ya marburg, ijapokuwa kuna kadhaa ziko kwenye matengenezo.
Kwa upande wake Rais Samia amesema “mlipuko huu haupaswi kusababisha hofu ya kimataifa au vizuizi vya biashara na usafiri. Tanzania iko wazi kwa biashara.”
WHO yapongeza uwekezaji wa Tanzania kwenye afya
Katika mkutano huo, Mkuu wa WHO amepongeza serikali ya Tanzania kwa juhudi za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
"Tunatambua uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kuimarisha mfumo wa afya na kuandaa taifa kwa dharura za kiafya," amesema.
Ametoa mfano wa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 akisema hatua hizi zimeelezwa kuwa muhimu katika kujenga uthabiti wa sekta ya afya nchini.
Ushirikiano wa kimataifa
Mkurugenzi Mkuu wa WHO ameshukuru washirika wa kimataifa, wakiwemo Muungano wa Ulaya, serikali ya Marekani, Uingereza, na wadau wengine wa afya kwa ushirikiano wao wa karibu na serikali ya Tanzania katika kukabiliana na mlipuko huu.
Uwekezaji katika afya kwa wote
WHO pia imesifu programu ya Serikali ya Tanzania ya kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya afya kupitia mpango wa Mafunzo kwa Wahudumu wa Afya Jamii uliozinduliwa mwaka 2023.
Dkt. Tedros amesema mpango huo umeongeza idadi ya wahudumu wa afya wenye ujuzi na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.